Loading...

Milango ya uwekezaji nchini iko wazi kwa yoyote - Dkt. Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uwekezaji kutoka nchini Uingereza (British International Investment) Bw. Nick O’Donohe leo Juni 18, 2024 Jijini Dodoma.

Bw. O’Donohe ambaye ameambatana na ujumbe wa wataalam ameeleza nia ya Uingereza kuendelea kuwekeza nchini Tanzania hususan katika miradi ya nishati jadidifu na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme hapa nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko amesema Tanzania kwa sasa inaangazia zaidi katika kuendeleza nishati jadidifu kuzalisha umeme ikiwemo maji, jotoardhi, jua, upepo na tungamotaka. Dkt. Biteko amefafanua kuwa tayari kama nchi kuna kazi kubwa imeshafanyika ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu hususan upepo, jua na maji na hatua inayofuata ni kuvutia wawekezaji ili kutekeleza miradi hiyo.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa milango ya uwekezaji hapa nchini iko wazi kwa yoyote mwenye nia ya kuwekeza na amewasihi wataalam ndani ya Serikali kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi linapokuja suala la uwekezaji na kupata taarifa za fursa za uwekezaji zilizopo Serikalini.

Kwa upande wake Bw. Nick O’Donohe ameeleza kuwa Kampuni anayoiongoza ni mwekezaji wa miaka mingi barani Afrika na kwa Tanzania wameanza kuwekeza tangu mwaka 1949.

Bw. O’Donohe aliongeza kuwa kwenye sekta ya nishati kampuni hiyo imewekeza hapa nchini kupitia Kampuni ya Globeleq ambayo inaimiliki kwa asilimia 70. Kampuni ya Globeleq ni mmiliki mwenye hisa nyingi kwenye kampuni ya Songas inayozalisha umeme na kufanya biashara na Tanesco.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Mbelwa Kairuki, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Balozi John Ulanga, Wakuu wa Taasisi za EWURA, TANESCO NA TPDC pamoja na Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.






Milango ya uwekezaji nchini iko wazi kwa yoyote - Dkt. Biteko Milango ya uwekezaji nchini iko wazi kwa yoyote - Dkt. Biteko Reviewed by Zero Degree on 6/19/2024 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.