REA yawanoa Wabunge kuhusu upatikanaji mikopo ya mafuta vijijini
Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), umetoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge kuhusu mikopo ya Ujenzi wa Vituo vidogo vya mafuta vijijini inayoratibiwa na Wakala huo.
📌 Wabunge wapongeza kwa fursa ya mitaji kwa wananchi vijijini
📌Kapinga asema Serikali inaangalia namna bora ya kuiendeleza mikopo husika
Wajumbe wa Kamati waliohudhuria semina hiyo jijini Dodoma ni kutoka katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Bajeti.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa elimu hiyo, Kaimu Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Mhandisi Michael Kyessi amesema lengo la mradi huo, ni kuwawezesha watanzania waliopo vijijini, kuachana na uhifadhi usio salama wa mafuta na kueleza wananchi wengi wa vijijini wanahifadhi mafuta kwenye madumu ambayo siyo salama kwa afya zao.
Amefafanua kuwa, dhamira ya Serikali ni kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini, pia kulinda maisha ya Watanzania pamoja na afya zao.
Ameeleza kuwa, mradi huo, utaweka mfumo rafiki ambao utaongeza ajira na mapato ya Serikali na kulinda mazingira kwa ujumla.
Mhandishi Kyessi, amesema kuwa mkopo huo unaweza kutolewa kwa mtu binafsi, kampuni, au vikundi vya wajasiriamali vijijini vilivyosajiliwa na Serikali au kijiji au Mamlaka husika.
Vigezo vingine ni vibali vya ujenzi( construction approval) kutoka Halmashauri ya Wilaya na EWURA na au Mji au stakabadhi ya malipo ya kibali husika.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga, ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa elimu hiyo na kueleza kuwa Watanzania wengi wanauhitaji wa kufanya biashara hiyo lakini wanashindwa kwasababu ya ukosefu wa mtaji lakini kwauwepo wa mradi huo Watanzania wengi wataweza kufanya biashara hiyo.
Pia, amewataka Wabunge wachukue elimu hiyo na kwenda majimboni mwao kuwaelemisha wananchi wao ili waweze kuchangamkia fursa hiyo ambayo itaweza kuwakwamua watanzania kiuchumi.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali itaendelea kufanya tathimini ya namna bora zaidi wa kuendeleza mradi huo ili uweze kuleta tija na Watanzania wafaidike na mradi huo.
Pia, amewaahidi Wabunge hao, kuwa Serikali itachukua michango waliyoitoa wakati wa semina hiyo na kwenda kuifanyia kazi ili kuboresha mradi huo ambao unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mafuta vijijini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema jukumu la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha vijiji vinapata nishati zote kwa wingi ili wananchi waweze kufaidika na miradi ambayo inatekelezwa na Wakala.
Aidha, amewashukuru Wabunge hao kwa kutoa maoni mbalimbali na kuahidi kuendelea kupokea maoni ambayo yatasaidia kuboresha mradi huo.
REA yawanoa Wabunge kuhusu upatikanaji mikopo ya mafuta vijijini
Reviewed by Zero Degree
on
6/03/2024 03:44:00 PM
Rating: