Idara/Vitengo vya mazingira vyasisitizwa kutekeleza majukumu yao
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Idara na Vitengo vya Mazingira katika wizara na taasisi za Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi yanayolenga kuleta suluhisho la athari za mazingira nchini.
📌 Taaasisi za mazingira zatakiwa kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa
📌 Kupanda mti pekee haitoshi kutunza mazingira
📌 Kila mtanzania ana jukumu la kuhakikisha anatunza na kuhifadhi mazingira
Akizungumza wakati wa kuzindua Mabanda ya Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa Mwaka 2024 yaliyofanyika leo Juni 3, 2024 jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeweka Vitengo vya Mazingira ili vifanye kazi ipasavyo kwa kuwa kila shughuli ina namna yake ya kuathiri mazingira na kuzuia athari zinazo tofautiana.
“Nataka nisisitize jambo hili muhimu sana kila wizara ina Kitengo cha Mazingira ni bahati mbaya kumbe kuna wakati vitengo hivi katika wizara na taasisi vimewekwa watu ambao wanadhani ni kama hawana shughuli ya kufanya, hawatengewi bajeti na hivyo hakuna shughuli ya kufanya, kazi hii imeachwa kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira pekee”, amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “Imefika mahali ukitaka kujua kuhusu mazingira basi umuone Waziri wa Mazingira peke yake wakati kila wizara ina Kitengo cha Mazingira na wajibu wake ni kuhakikisha kwamba mazingira yanahifadhiwa hata hapa kwenye uzinduzi wa mabanda ya maonesho vitengo vya baadhi ya wizara na taasisi havipo hapa wanadhani wana majukumu kuliko mazingira.”
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo |
Aidha, Dkt Biteko amewaeleza viongozi na watumishi wa Serikali kuwa mazingira ni kila kitu huku akitolea mfano uwepo wa nguzo za umeme, ujenzi wa miradi ya barabara na hospitali nayo ni sehemu ya mazingira kwa kuwa ina uhusiano wa moja kwa moja na mazingira kwa kuharibu au kulinda na kuwa suala la mazingira linapaswa kusemwa na watu wote Serikalini katika ngazi zote ikiwemo za wakuu wa mikoa na wilaya.
Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa kutunza mazingira si kupanda miti tu bali kulinda na kuhifadhi ni jambo muhimu na lenye gharama zaidi. Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa wizara ambao Vitengo vyao vya Mazingira havikushiriki Maonesho hayo ya Wiki ya Mazingira vijulikane ili vielezwe namna ya kutekeleza majukumu yao.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa rai kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mazingira kitakachofanyika Juni 5, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa Watanzania kutembelea mabanda 42 ya maonesho ili kupata elimu kuhusu utunzaji wa mazingira pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu teknolojia mpya za utunzaji wa mazingira na biashara ya hewa ya ukaa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa wake umeendelea kutekeleza maagizo na shughuli mbalimbali zinazolenga kutunza mazingira na kuwa waliweka azimio la kuhakikisha wanatenga maeneo ya kuuza hewa ya ukaa na tayari Wilaya ya Mpwapwa imefanikiwa kukidhi vigezo vilivyowekwa katika kufanya biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya utunzaji wa mazingira. (Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati)
Idara/Vitengo vya mazingira vyasisitizwa kutekeleza majukumu yao
Reviewed by Zero Degree
on
6/03/2024 09:38:00 PM
Rating: