Loading...

EAC itumie vijana kujiletea maendeleo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kutumia vema idadi kubwa ya watu iliyopo hususani vijana katika kujiletea maendeleo kama itawekeza zaidi katika elimu na afya ya watoto.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Elimu wa Kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sherehe za Mwaka wa Elimu wa Umoja wa Afrika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amesema ongezeko la watu katika mataifa ya Afrika Mashariki inatoa ishara ya ulazima wa kuongeza rasilimali zaidi za kifedha ili kukidhi mahitaji ya elimu bora na afya bora.

Makamu wa Rais amesema muenendo wa idadi ya watu Afrika Mashariki inaweza kuwa baraka kubwa kwa kuendelea kuwa na vijana na watu mahiri wa kujenga uchumi ikiwa rasilimali watu hiyo itatumika kikamilifu.

Pia amesema kutokana na takwimu za Benki ya Dunia Bara la Afrika limekua likipata matokeo ya faida katika elimu ukilinganisha na mabara mengine lakini bado ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara, elimu imekua na ufadhili mdogo zaidi.

Ametoa wito wa hatua zaidi kuchukuliwa na kutumia juhudi zote kutambua kuwa changamoto za elimu barani Afrika zinatokana kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mdogo katika sekta hiyo, jambo ambalo linafanya kuwa vigumu kutoa elimu bora yenye ujuzi unaohitajika ili kukabiliana na maendeleo makuu matatu, ambayo ni ongezeko la idadi ya watu,utandawazi na maendeleo ya teknolojia.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo imelenga kufanya elimu ya lazima kutoka miaka saba iliyopo sasa hadi miaka kumi ifikapo mwaka 2027/2028. Aidha amesema mabadiliko ya mtaala wa elimu nchini yanalenga kuongeza ubora wa elimu pamoja na kuandaa rasilimali watu itakayoendana na mahitajio ya dunia ya sasa kama vile maendeleo ya dijitali, teknolojia pamoja na kutumia vema fursa mbalimbali zilizopo.
EAC itumie vijana kujiletea maendeleo EAC itumie vijana kujiletea maendeleo Reviewed by Zero Degree on 8/13/2024 04:51:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.