Loading...

Tanzania yaendelea kutangaza na kukuza Kiswahili na utamaduni wake kimataifa


Lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania vimeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali wa kimataifa waliotembelea banda la Tanzania katika Wiki ya utamaduni na Kiswahili inayoendelea kwenye maonesho ya biashara ya dunia (Expo 2025) yanayofanyika Osaka.

Viongozi waandamizi wa mataifa mbalimbali, wametembelea banda hilo ikiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japani, Bw. Koichiro Gemba, Mfalme wa Lesotho, Mhe. Letsie III na Mhe. Prudence Sebahizi, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda.

Viongozi hao wameonesha kuvutiwa kwa kiasi kikubwa na lugha ya Kiswahili na Utamaduni kupata nafasi katika Maonesho hayo ya Dunia yenye hadhi kubwa.

Akizungumza wakati alipotembelea banda hilo Mhe. Sebahizi alieleza kufurahishwa na namna lugha ya Kiswahili ilivyopewa nafasi katika maonesho hayo ya dunia na kudai Kiswahili kinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuwaunganisha Waafrika katika juhudi zao za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza na maofisa wa taasisi za Tanzania zinazoshiriki katika maonesho hayo, ikiwemo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mhe. Sebahizi amesema kuwa lugha ya kiswahili inakidhi kwa matumizi miongoni mwa Waafrika.

Viongozi hao pia walipata fursa ya kujionea vivutio vya kitamaduni kama vile mavazi ya jadi, sanaa za mikono, bidhaa za kipekee kama kahawa ya Kilimanjaro, Madini ya Tanzanite, viungo vya asili vya Zanzibar na machapisho mbalimbali ya Kiswahili huku Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka BAKITA ikiwavutia wengi.

Ushiriki huu wa Tanzania katika maonesho hayo ambayo kwa upande wa Tanzania yanaratibiwa na TanTrade, ni sehemu ya juhudi endelevu za kuitangaza lugha ya Kiswahili kama urithi wa Afrika na dunia, sambamba na utamaduni wake tajiri, ili kuimarisha uhusiano ya kimataifa na kuvutia wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo kupitia nguvu ya lugha na utambulisho wa kitaifa.

Kilele cha wiki hii ya Utamaduni na Kiswahili katika maonesho hayo kitafanyika tarehe 7 mwezi wa 7, ambapo kwa kawaida huwa ni Maadhimisho ya Siku Kiswahili Duniani (MASIKIDU), ambapo kutakuwa na utoaji wa vyeti na tuzo mbalimbali kwa wadau walioshiriki kwa hali na mali kukikuza, kukieneza, na kukiendeleza Kiswahili nchini Japani.







Tanzania yaendelea kutangaza na kukuza Kiswahili na utamaduni wake kimataifa Tanzania yaendelea kutangaza na kukuza Kiswahili na utamaduni wake kimataifa Reviewed by Zero Degree on 7/04/2025 05:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.