Marekani yalaani kufutwa kwa matokeo Zanzibar
Marekani imelaani hatua ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais pamoja na wajumbe wa bunge la wawakilishi visiwani humo.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa ubalozi huo nchini Tanzania, Marekani ilisema imeshtushwa na hatua hiyo na kutoa wito tume hiyo iondoe tamko hilo.
Zec imeahidi kutangaza tarehe mpya ya marudio ya uchaguzi huo.
Katika kufutilia mbali matokeo ya urais wa Zanzibar, tume ya uchaguzi ya Zanzibar-ZEC ilisema shughuli nzima ya upigaji kura visiwani iligubikwa na kasoro nyingi.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha amesema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao".
"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika."
Amesema hilo ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapiga kura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura".
Kadhalika, amesema kura hazikupata ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba ambako amesema kuwa baadhi ya mawakala wa baadhi ya vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.
Hata hivyo, taarifa ya ubalozi wa Marekani inasema kufutilia mbali matokeo hayo kunasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani.
Aidha Taarifa hiyo inasema kuwa hatua hiyo ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar inakwenda kinyume kabisa na tathmini ya waangalizi wa uchaguzi kutoka ubalozi wa Marekani, jumuiya ya ulaya, jumuiya ya madola na jumui ya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa haki.
Source: BBC
Marekani yalaani kufutwa kwa matokeo Zanzibar
Reviewed by Zero Degree
on
10/29/2015 10:42:00 AM
Rating: