Deo Filikunjombe: Kijue chanzo cha kifo cha shujaa huyu wa Tanzania!!!
Filikunjombe alikodi chopa hiyo kutoka kampuni ya ndege ya Sun Drew inayomilikiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka na ilikuwa inafanyiwa ukarabati na kampuni ya Laid Loris.
Dar es Salaam. Uchunguzi wa awali kuhusu ajali ya chopa iliyogharimu maisha
ya aliyekuwa mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na wenzake watatu, unaonyesha
ilitokana na hitilafu ya injini, Mwananchi imebaini.
Katika ajali hiyo iliyotokea Oktoba 16 kwenye pori la Selous, mbali ya
Filikunjombe, rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa na wengine wawili
waliokuwamo ndani ya chombo hicho kilichokuwa na namba za usajili 5Y-DKK na
namba za utengenezwaji 7027 Eucereuil, pia walifariki dunia.
Filikunjombe alikodi chopa hiyo kutoka kampuni ya ndege ya Sun Drew
inayomilikiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka na ilikuwa
inafanyiwa ukarabati na kampuni ya Laid Loris.
Baada ya ajali hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa
ushirikiano na Wizara ya Uchukuzi waliita timu ya wachunguzi wa ndege kutoka
Ufaransa ambayo ilitua nchini Oktoba 20. Timu hiyo ya watu wanne ilijumuisha mtu
mmoja kutoka kampuni ya Airbus Industries ya Marseilles ambao ni watengenezaji
wa chopa hiyo; mtu mmoja kutoka kampuni ya Turbo Meca, waliotengeneza injini; na
watu wawili kutoka BEA, kitengo cha uchunguzi wa ndege kutoka Serikali ya
Ufaransa.
Timu hiyo ilibaini hitilafu hiyo, ikibainisha kuwa baada ya injini kufeli,
chopa hiyo ilianza kushuka hadi ikaanguka na kulipuka. Sababu za kulipuka kwake
zimetajwa na wachunguzi hao kuwa ni madumu matano ya mafuta ya ujazo wa lita 20
yaliyokuwa ndani ya chopa hiyo.
Mchunguzi Mkuu wa Ajali za Ndege wa Wizara ya Uchukuzi, Omar Mhina aliiambia
Mwananchi kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kufeli
kwa injini.
“Katika uchunguzi wa awali, tulichukua injini na kugundua kuwa ilipata
hitilafu. Hiyo ndiyo lugha ya kwanza tunayoweza kusema wakati tukisubiri
uchunguzi mwingine,” alisema Mhina katika mahojiano na Mwananchi.
Mhina alisema wameshaichukua injini kutoka pori hilo la Selous na kwamba
wanatarajia kuipeleka kwa watengenezaji wake kwa ajili ya kufunguliwa na kujua
kiini cha kufeli kwa injini hiyo.
Alisema waliwasiliana na wamiliki wa chopa hiyo nchini Kenya, lakini
hawajapata ushirikiano wa kuridhisha mpaka sasa. Lakini Mwananchi ilizungumza na
opereta mkuu wa chopa hiyo wa Kenya, na rubani wa kampuni ya Sun Drew, Kapteni
Charles Wachira ambaye alisema TCAA hawajawasiliana na Mamlaka ya Anga ya Kenya
(KCAA) kwa ajili ya uchunguzi wa ajali hiyo.
“Mimi ni kapteni wa ndege lakini siwezi kufanya lolote kama sijapata baraka
kutoka TCAA na KCAA. Wao ndio walitakiwa wawasiliane kwanza kabla ya sisi Sun
Drew kuchukua hatua zozote, ni suala baina ya serikali na serikali,” alisema
Wachira.
Kapteni huyo amesema akipata ruhusa kutoka KCAA atakuja nchini kwa ajili ya
uchunguzi wa chanzo cha ajali ya chopa hiyo.
Kauli ya Musyoka
Lakini Kalonzo alisema kampuni yake imeshampa baraka zote, Kapteni Wachira
ili kushirikiana na Tanzania kubaini chanzo cha ajali hiyo na kwamba
kilichochelewesha ujio huo ni kusubiri kumalizika kwa shughuli za uchaguzi
zilizokuwa zikifanyika Tanzania.
Kalonzo alisema walituma mwakilishi ambaye ni mjumbe wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Peter Mathuki kupeleka salamu za rambirambi na kuhudhuria msiba wa
Kapteni Silaa.
“Ni lazima tushiriki katika hili kwa sababu ni pigo kubwa kwetu na kwa
serikali yenu. Tayari Kapteni Wachira amekuja huko ili kushirikiana na Mamlaka
ya Anga ya Tanzania,” alisema Kalonzo.
Mafuta yalilipua
Chanzo kingine cha ajali hiyo kilichoelezwa na timu hiyo ni madumu matano ya
mafuta ya ndege yaliyokuwa yamepakiwa ndani.
“Walikuwa wamebeba hayo madumu yenye mafuta ya akiba kwa kuwa walikuwa
wametokea Ludewa ambako hakuna mafuta; unajua chopa hazikai na mafuta kwa muda
mrefu ndiyo maana walibeba mafuta ya akiba,” alisema mtoaji habari
wetu.
Kadhalika chanzo hicho kimesema viti vya ndege vilionekana kuanguka na
kuvunjika na watu waliokuwamo walivunjika uti wa mgongo na miguu. Hata kama
wasingeungua, wangepoteza maisha kutokana na madhara ya kuanguka
kwake.
Ripoti ya BEA
Ripoti ya awali ya Kitengo cha uchunguzi wa ajali za ndege cha Serikali ya
Ufaransa (BEA) iliyochapishwa kwenye tovuti yake imeeleza kuwa chopa hiyo
ilionekana ikianguka kutoka angani, ikiwa tayari haina nguvu na ikifuka moshi.
Kadhalika chopa hiyo ilionekana kwa muda mrefu ikiruka umbali wa chini na baada
ya kuanguka, ililipuka.
Turbomeca
Lakini mkuu wa kitengo cha wanafizikia wa kampuni ya Turbomeca iliyotengeneza
injini ya ndege hiyo, Delpgine Robelin alikataa kutoa maelezo akisema kuwa ni ya
siri. “Hii ni siri kubwa. Hakuna taarifa zozote zinazoweza kutolewa,” inasema
barua pepe ya Robelin akijibu barua pepe ya Mwananchi iliyoomba kupata ripoti ya
awali ya uchunguzi wa ajali hiyo.
Mawasiliano angani
Uchunguzi umebaini pia Kapteni Silaa hakuwasiliana na kitengo cha usalama wa
anga na mawasiliano ya ndege cha TCAA. Kuhusu tatizo la chopa. Mhina amesema Kapteni Silaa aliwasiliana na kitengo
hicho wakati ndege ipo ardhini, ikipaa na ilipofika juu, lakini baada ya hapo
hakukuwa na mawasiliano yoyote.
“Kabla hajaruhusiwa kwenda eneo jingine la anga (area control route) ndipo
alipokata mawasiliano na hakuwasiliana hata na ndege nyingine kueleza kama ana
tatizo,” alisema.
“Kwa kawaida chopa zinatakiwa kuwasiliana zikiwa angani, lakini hakuna chopa
yoyote iliyotoa taarifa kama waliwasiliana na Kapteni Silaa,” alisema Mhina na
kuongeza: “Iwapo chopa ina matatizo ya injini, kuna namna ambayo marubaini
wanaweza kudhibiti ili kusitokee madhara, lakini haijulikani kwa nini Kapteni
Silaa alishindwa kudhibiti hali hiyo.”
Msikilize Shahidi
Mhina alisema kwamba mmoja wa mashuhuda aliiambia timu ya wachunguzi kwamba
alianza kuona chopa hiyo ikifuka moshi wakati iko hewani. “Lakini haikuwa
ikiungua, hapana, ilifuka moshi hadi ilipoanguka ndipo ikawaka.”
Deo Filikunjombe: Kijue chanzo cha kifo cha shujaa huyu wa Tanzania!!!
Reviewed by Zero Degree
on
11/23/2015 11:28:00 AM
Rating: