Loading...

Kigogo Kenya aingia matatani kwa kumfuata Magufuli Dar!!


Nairobi. Gavana wa Jimbo la Siaya, nchini Kenya, Cornel Rasanga ameingia matatani akidaiwa kutumia Sh20 milioni za nchi hiyo (karibu Sh400 milioni) kutoka katika mfuko za Serikali kwa ajili safari ya kuhudhuria sherehe za kumwapisha Rais John Magufuli.

Dk Magufuli alipishwa Novemba 5, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 25.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kenya (PAC), Nicholas Gumbo amemtuhumu Rasanga kwa kutumia fedha hizo kutoka kwenye mfuko wa Serikali wa safari.
“Gavana wa Rasanga lazima awaambie wananchi wa Siaya, imekuwaje akatumia Sh20 milioni kwenda Tanzania kwa ajili ya shughuli ya Dk Magufuli?

“Sidhani kama Dk Magufuli ana uhusiano wowote na wananchi wa Kaunti ya Siaya kiasi cha Gavana kutumia fedha hizo za umma kwenda Tanzania,” alisema Gumbo.

Gumbo alisema Dk Magufuli anafahamika kuwa ni rafiki mkubwa wa kiongozi wa Cord, Raila Odinga ambaye pia alihudhuria sherehe hizo.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika.

Akizungumzia tuhuma hizo, Rasanga alisema madai yalitolewa na Gumbo ambaye ni Mbunge wa Rarieda, ni uzushi na alikuwa anataka kujikweza kisiasa.

“Hii ilikuwa safari binafsi. Hatukutumia fedha za Serikali kama inavyoelezwa,” alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation.

Gavana huyo alisema alikwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Dk Magufuli kwa mwaliko binafsi wa Rais hiyo wa Tano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema ziara yake Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano katika Ukanda wa Ziwa Victoria.

“Ukweli ni kwamba Rais wa Tanzania aliwahi kutembelea Siaya na tulijadiliana masuala mbalimbali ikiwamo usafiri hasa katika Ziwa Victoria,” alisema Rasanga na kuongeza:
“Dk Magufuli anatokea Kanda ya Ziwa na mpango wake mkubwa ni kuimarisha bandari katika Ziwa Victoria na kuchaguliwa kwake kuwa Rais kutarahisisha zaidi utekelezaji wa mipango yake.

“Hakuna sababu ya kuingiza siasa katika safari hii. Tuko katika mipango mizuri tu ya kibiashara na Tanzania ambayo kwa sasa imeanza kupanuka.”

Mwenyekiti huyo wa PAC Kenya alisema safari hiyo ya Novemba 5, ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Hata hivyo, Naibu Gavana, Wilson Ouma alipinga madai ya Gumbo akisema alikuwa na lengo la kumharibia bosi wake.

“Ukweli Gavana Rasanga alitumia fedha zake kwenda Tanzania na uzushi wowote unatakiwa ukomeshwe,” alisema Ouma alipozungumza na Nation.

Akisisitiza, Gumbo alisema ataendelea kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma unaofanywa na maofisa wa Serikali kwa kutumia vyeo vyao.

Magufuli kivutio nchi jirani.

Madai hayo yameibuka wakati kasi ya utendaji wa Rais Magufuli tangu aapishwe ikizidi kuwa kivutio katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini Kenya na katika nchi nyingine jirani.

Kwa kipindi cha takriban siku 20 alizokaa ofisini, Rais Magufuli amechochea utendaji katika utumishi wa umma na kupunguza gharama akianza kwa kukata safari za nje kwa watumishi wa umma na sherehe za uhuru.

Kutokana na utendaji huo, watumiaji wa mtandao wa Twitter walianza kutumia kwa kasi kiunganishi cha “#Magufuli” huku kwa sehemu kubwa, raia wa Kenya wakiongoza mjadala hadi jana jioni.

Raia hao walionekana kuvutiwa na utendaji katika siku za awali za Dk Magufuli huku wakikosoa Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wakidai inazidi kukithiri kwa rushwa.

“Hello Tanzania, Kenya inataka imkodi #Magufuli kwa wikiendi moja,” aliandika kwa Kiingereza mtumiaji wa Twitter mwenye jina la Ezekiel Mogaka kutoka Kenya.

Lakini mtumiaji mwingine mwenye akaunti yenye utambulisho wa Chakkah Dan aliandika; “Rais Magufuli bila shaka (Hayati Baba wa Taifa), Julius Nyerere anatazama chini kutoka peponi akiwa anajivunia utendaji wako.

“Watanzania wanaamka kila siku asubuhi wakiona jambo fulani limetekelezwa na #Magufuli lakini Wakenya wanakwenda kulala na jambo ambalo #Kenyatta kaahidi,” aliandika The Golden Voice.

Kwa mujibu wa mtandao unaofutilia mijadala kwenye Twitter nchini Kenya, #GURUS daily trend, tangu jana asubuhi, kiunganishi “#Magufuli” kilikuwa ni miongoni mwa viunganishi vitano vilivyokuwa vinaongoza kwa kuchangiwa, vingine ni #WhatBalalaShouldDo, #YouDontKnowLifeStruggle, Welcome to Kenya, Turkey na #FagiaKenya.

Katika mijadala hiyo, Wakenya walikuwa wakijaribu kufananisha siku 19 za Rais Magufuli na miaka mitatu ya Rais Kenyatta na kutania kuwa iwapo Rais wa Tanzania angegombea mwaka 2017 nchini humo bila shaka wangemchagua.

Mijadala hiyo ‘haijabamba’ Kenya pekee, Burundi nao hawakuwa nyuma. Mwenye akaunti yenye jina Joseph Siboma aliandika: “Wakati ukomo wa madaraka ukiheshimika Tanzania, namkaribisha #Magufuli atawale kwa vipindi visivyoisha #Burundi.”

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, alisema nchi nyingi za Afrika zinahitaji kuwa na viongozi wanaojali masilahi ya wananchi lakini historia inaonyesha sehemu kubwa ya viongozi waliopo madarakani ni watawala wasiojali watu wao na hawapendi kuharibiwa nafasi zao.

“Sasa inapotokea kuna kiongozi kama Rais Magufuli anayepunguza matumizi ya Serikali bila shaka atakonga nyoyo za wengi. Mtindo wa uongozi wa Rais ni mpya na katika mambo yote aliyoyafanya hakuna wanaopinga zaidi ya kuwapo wachache wanaoonya mwenendo huo uendelee bila kupungua kasi,” alisema Mbunda.    




Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hiyo!!!!!
Kigogo Kenya aingia matatani kwa kumfuata Magufuli Dar!! Kigogo Kenya aingia matatani kwa kumfuata Magufuli Dar!! Reviewed by Zero Degree on 11/26/2015 12:09:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.