Loading...

Dar es salaam: Dk Kigwangalla awafungia geti wafanyakazi wachelewaji.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa adhabu kwa wafanyakazi wote waliofika ofisini baada ya 1:30 asubuhi na kwa kufungiwa geti.

Akiwa katika ofisi za wizara hiyo jana, Dk Kigwangalla aliwataka wafanyakazi waliochelewa kuandika barua za kujieleza sababu za kuchelewa kufika kazini.

Dk Kigwangalla alifika katika eneo la kazi na kukuta mahudhurio ya wafanyakazi yasiyoridhisha hali iliyosababisha kutoa agizo la kufungiwa geti waliochelewa kufika kazini.

Alipomaliza kukagua na kusaini madaftari hayo ya mahudhurio kulingana na idara na vitengo vilivyopo wizarani hapo, Dk Kigwangalla alisema:

“Wafanyakazi wanawajibu wa kuwahi kazini saa 1:30 asubuhi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kutoka saa 9:30 jioni baada ya muda wa kazi, hatuwezi kuendelea kuvumilia tabia ya watu kuendelea kumwibia mwajiri muda wa kufanyakazi. Sisi tumewahi kazini, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wengine, halafu watumishi wanachelewa, tumeonesha mfano, tunawahi na tunachelewa kuondoka,” alisema Dk Kigwangalla.

Idara zilizopo wizarani hapo ni pamoja na Utawala, Kinga, Mafunzo, Tiba, Udhibiti na Uhakiki Ubora, Mganga Mkuu, Uhasibu, Sera na Mipango, Wauguzi na Famasia, Sheria, Mawasiliano serikalini na Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).

Alishangazwa kwa kutokuwa na mfumo wa kuweza kuulinda muda wa mwajiri kwa kuonyesha kila mtumishi anapoingia na kutoka kwa kuchanja kadi mlangoni ili kujua idadi kamili ya mahudhurio ya wafanyakazi.

“Mfumo huu utakomesha tabia ya watumishi kuchelewa kufika kazini na kuondoka mapema kabla ya muda wakazi,” alisema.

“Tutaweka malengo pamoja na kusaini mikataba na watumishi wote katika wizara hii ili wajue kazi zao,” alisema.

Alisema amefikia hatua hiyo ya kusimamia maadili ya kazi ili kukomesha tabia ya uchelewaji kutokana na wizara hiyo kulaumiwa kwa urasimu ilhali watumishi hawawahi kazini.


Credits: Mwananchi


Mshirikishe na mwenzako kuhusu habarihii!!
Dar es salaam: Dk Kigwangalla awafungia geti wafanyakazi wachelewaji. Dar es salaam: Dk Kigwangalla awafungia geti wafanyakazi wachelewaji. Reviewed by Zero Degree on 12/19/2015 02:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.