Loading...

Madereva wa Ilemela wagoma kufanya kazi, chanzo kikiwa ni polisi kushusha nauli.


Mwanza. Madereva wa mabasi yaendayo Kata ya Igombe, Manispaa ya Ilemela, Mwanza wamegoma kwa saa saba kupeleka wasafiri kwa madai ya kushushwa kwa nauli na ofisa mmoja wa polisi kitengo cha usalama barabarani kutoka Sh1,500 hadi Sh700.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Wenceslaus Gumha aliingilia kati suala hilo juzi akishauri huduma hiyo iendelee na kwamba hakuna polisi anayeruhusiwa kupanga nauli.

“Naomba madereva mfanye kazi, hili suala litapatiwa ufumbuzi haraka na bei elekezi itapangwa, tutafuatilia Sumatra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) ili kupata ufumbuzi,” alisema Gumha.

 Mgomo huo uliofanyika juzi kuanzia saa tano asubuhi hadi saa moja usiku, ulisababisha wasafiri kushinda vituoni bila kujua namna la kufanya, huku wakiilalamikia Serikali kwa kushindwa kusimamia vyema haki za wananchi.

Baadhi ya wasafiri hao, Hamisa Nuru, John Mgunda na Jalida Kamalanzi walisema walishinda njaa kwa saa saba na watoto wao.

“Hili la leo (juzi) hatutalisahau, yaani watu tunashinda njaa, hatuna pa kwenda kwa sababu ya usafiri, tunaiomba Serikali ishughulikie jambo hili,” alisema Nuru.

Madereva wa magari hayo walisema tatizo ni polisi ambao walijipangia bei bila kuwapa taarifa na kufikia muafaka, kwani barabara inayotumika ni mbovu na umbali wake ni kilomita 38.

Walisema awali nauli ya kutoka Mjini kwenda Igombe ilikuwa Sh700, wakati wakitumia barabara ya uwanja wa ndege, lakini ilipofungwa, walianza kutumia Barabara ya Nyakato na nauli ilipanda hadi Sh1,500 kutokana na umbali uliopo.

Uongozi wa Sumatra mkoani hapa umeahidi kushughulikia tatizo hilo ili kuondoa kero kwa wasafiri.

Mwenyekiti wa Madereva Kanda ya Ziwa, Hassan Dede alisema tatizo ni la Sumatra ambao hawataki kutoa bei elekezi.

Dede alisema kila siku hulipia ushuru wa Sh1,000, fedha ambazo alisema hazijulikani zinapokwenda kwani barabara ni mbovu.

“Tatizo ni la Sumatra, tangu lini polisi wakapanga bei ya nauli? Tatizo mamlaka husika ipo kimya, jambo hili tutalifanyia kazi hadi haki yetu ipatikane.”

Credits: Mwananchi



ZeroDegree
Madereva wa Ilemela wagoma kufanya kazi, chanzo kikiwa ni polisi kushusha nauli. Madereva wa Ilemela wagoma kufanya kazi, chanzo kikiwa ni polisi kushusha nauli. Reviewed by Zero Degree on 12/26/2015 04:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.