Zanzibar bado hakijaeleweka mpaka sasa!!
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, akisema kulikuwapo na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na kuahidi kuwa ungeitishwa uchaguzi mpya ndani ya siku 90.
Zikiwa zimepita siku 44 tangu atangaze uamuzi huo, hakuna maelekezo yoyote kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo kutoka ZEC, huku kukiwa hakuna taarifa rasmi za maendeleo ya vikao vinavyodaiwa kufanywa baina ya uongozi wa CCM na CUF, vyama vyenye upinzani mkali visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Salum Kassim Ali aliiambia Mwananchi jana kuwa hawajapata maagizo yoyote ya kutakiwa kuanza maandalizi ya uchaguzi.
Ingawa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kina, Kassim Ali alisema wakati akijibu maswali ya gazeti hili kuwa hakuna kinachoendelea hadi sasa.
Haya ni mahojiano baina ya Kasimu Ali na Mwananchi communications:
"Kassim Ali: Wewe unauliza kununua pampasi wakati hujui mtoto atazaliwa lini? Badala ya kuuliza uchaguzi upo au haupo unauliza vitu vingine?” alihoji Kassim Ali alipoulizwa na gazeti hili uchaguzi wa marudio utafanyika lini.
Mwananchi: Haya basi, uchaguzi utafanyika lini?
Kassim Ali: Mimi si msemaji wa ZEC.
Mwananchi: Lakini tunafahamu kwamba ZEC ina sehemu mbili, sehemu ya uchaguzi inayoongozwa na Mwenyekiti Jecha, na sehemu ya utawala inayoongozwa na mkurugenzi ambaye ni wewe.
Kassim Ali: Hilo ni sahihi.
Mwananchi: Na maandalizi yote ya uchaguzi hufanywa kwa maelekezo ya Mwenyekiti Jecha.
Kassim Ali: Ndiyo
Mwananchi: Kwa sasa mna maelekezo yeyote ya kufanya maandalizi ya uchaguzi wa marudio?
Kassim Ali: Hatuna maelekezo yoyote."
Kabla ya Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad alitangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo na kuitaka ZEC imtangaze mshindi.
Kitendo hicho pamoja na vurugu ambazo Jecha alidai zilifanyika ndani ya ZEC na wakati wa kuandikisha wapigakura, ndvyo vilivyomfanya atangaze kufuta uchaguzi, uamuzi ambao unapingwa na CUF inayodai kuwa mwenyekiti huyo hana mamlaka ya kufuta uchaguzi na kwamba alichukua uamuzi huo bila ya kushirikisha wajumbe wenzake.
Kuhusu taarifa kwamba Jecha amekuwa haonekani ofisini, mkurugenzi huyo wa uchaguzi wa ZEC alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba kama kuna taarifa zimeenea kuhusu jambo hilo, ziandikwe hivyo hivyo.
“Aliyekuambia hayupo ofisini ni nani? Andika hayo hayo ya mitaani,” alisema.
Akizungumzia suala hilo la tarehe ya uchaguzi wa marudio, ofisa uhusiano wa ZEC, Idrissa Jecha alisema kuwa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar haizungumzii uchaguzi wa marudio bali tarehe ya kupiga kura baada ya wagombea kuteuliwa na Tume.
Alisema kifungu cha 51 cha sheria hiyo kinasema tarehe ya kupiga kura inatakiwa kuwa si chini ya siku 60 au si zaidi ya 90 tangu siku wagombea walipoteuliwa na ZEC.
Akizungumzia sintofahamu ya uchaguzi wa Zanzibar, Kamishna wa ZEC, Ayoub Bakari Hamad alisema hakuna kazi wanayofanya hivi sasa na kwamba mara ya mwisho walikutana Novemba mosi chini ya Jecha na tangu hapo hawajukutana tena.
Hamad alisema tangu wakati huo hajamuona wala kusikia alipo mwenyekiti huyo. Alisema kwa kawaida hukutana mara moja kwa mwezi, lakini panapokuwa na mambo ya kufanya hukutana mara kwa mara.
Kuhusu marudio ya uchaguzi wa Zanzibar, alisema hawana taarifa yoyote na wala hakuna maelekezo ya kufanya maandalizi ya uchaguzi huo.
“Unajua sisi (ZEC) tulikuwa marubani ndani ya ndege, lakini ndege yetu imetekwa nyara na tangu hapo sisi tumekuwa abiria tu. Hatujui mwelekeo wa ndege mpaka mteka nyara atakaposema,” alisema.
“Hatushirikishwi kwa lolote, ni sawa na abiria asiyetakiwa ndani ya ndege.”
Jecha hakuweza kupatikana nyumbani kwake, ofisini au kwa njia ya simu alipotafutwa kuzungumzia suala hilo. Baadhi ya watu wake wa karibu waliongea na Mwananchi walisema namba haipo hewani kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu, Hassan Ali waandishi wa habari walikwenda kijijini kwa mwenyekiti huyo Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, mkoani Kaskazini Unguja lakini hawakufanikiwa kumpata.
Walichukua uamuzi huo baada ya kuarifiwa kuwa Jecha hakuwepo nyumbani kwake, Mtaa wa Saateni na Makadara Mjini Unguja anakoishi na familia yake.
Majirani wa mitaa hiyo, akiwamo Mzee Saleh Nassor ambaye alidai huonana na Jecha mara kwa mara mtaani, hawakuwa na jibu la uhakika kuhusu mwenyekiti huyo.
“Labda nendeni mkamtafute Kibeni (pia Mkoa wa Kaskazini Unguja) alikojenga, mnaweza mkamuona huko kama analindwa,” alisema Mzee Saleh.
Kijijini kwake, baadhi ya wakazi walisema hawajamuona kwa kipindi kirefu.
Mzee mmoja wa makamo aliyejitambulisha kwa jina la Mwalimu Juma, ambaye anazungumza Kiswahili cha Kitumbatu, alisema : “Haya ya Jecha yanakuwa ya nchi nzima maana kijijini hayuko na mjini amehama na si twamtaka aje hapa atuamulie hicho kitendawili cha uchaguzi.”
Akizungumzia suala hilo, mhadhiri wa moja ya vyuo vikuu vya Zanzibar, Dk Said Abdalla alisema: “Kisaikolojia wananchi wa pande zote za kisiasa wanaumia kwani nchi haiendi na siyo chama.”
Credits: Mwananchi
Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!
Zanzibar bado hakijaeleweka mpaka sasa!!
Reviewed by Zero Degree
on
12/13/2015 02:23:00 PM
Rating: