Bomoabomoa yahamia Manispaa ya Shinyanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Shinyanga. Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeanza kubomoa majengo yaliyojengwa kwenye maeneo yasiyostahili na ya hifadhi ya barabara.
Wamiliki wa majengo na nyumba hizo wametakiwa kuanza kubomoa kwa hiyari kabla Serikali haijaanza kutekeleza kazi hiyo.
Hata hivyo, kazi hiyo ilianza jana kwa ukumbi wa starehe unaojulikana kwa jina la Dragon Pub uliopo Shinyanga mjini unaodaiwa sehemu ya jengo lake kujengwa kwenye hifadhi ya Barabara ya Uhuru kuelekea Soko la Nguzo Nane.
Mmoja wa wakurugenzi wa ukumbi huo, Humprey Geofrey alisema anashangaa kuona manispaa hiyo ikibomoa jengo lao wakati ndiyo waliotoa kibali cha kujenga na kuwapatia leseni ya biashara.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Lewis Kalinjuna alisema kazi ya kubomoa majengo yaliyojengwa katika maeneo yasiyostahili ni endelevu.
“Sisi tunabomoa katika maeneo yote yasiyo sahihi, mfano hawa wanaojenga katika maeneo ya hifadhi ya barabara na maeneo ya wazi lazima watavunjiwa tu,” alisema Kalinjuna.
Alitoa wito kwa wakazi wa Manispaa hiyo kutekeleza agizo la kuwataka kubomoa nyumba na majengo hayo kwa hiyari yao kabla tingatinga la manispaa halijafanya kazi yake. “Wakipuuza wataingia hasara mara mbili, ni bora wakasalimisha mali zao mapema,” alisisitiza.
Source: Mwananchi
Bomoabomoa yahamia Manispaa ya Shinyanga.
Reviewed by Zero Degree
on
1/17/2016 08:19:00 PM
Rating: