Loading...

Wahukumiwa kifungo cha mwaka moja Jela kwa kuingia nchini kinyume na sheria.


Ngara. Mahakama ya Wilaya ya Ngara, imewahukumu adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh500,000 raia watatu wa Burundi kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Wilaya ya Ngara, Endrew Kabuka baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulioongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Respicius John.

Awali, upande wa mashtaka ulidai kuwa watu hao, Mose Ndivanze (25) na Machumi Andrew (50) wakazi wa Giteranyi na mwenzao Nyabenda Emily (20) mkazi wa Muyinga nchini humo, waliingia nchini siku na muda usiojulikana kinyume cha sheria.

“Watuhumiwa walitiwa mbaroni Desemba 30, mwaka jana wakiwa eneo la Kijiji cha Mugoma,” alidai Respicius huku akiiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao.

Watuhumiwa walikiri kosa na kupelekwa gerezani kutumikia adhabu zao baada ya kushindwa kulipa faini na watarejeshwa nchini mwao wakimaliza vifungo.

Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara, Yohana Andrew (38) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kujaribu kujinyonga kwa kutumia mkanda wa mashine ya kusaga.

John alidai mbele ya Hakimu Kabuka kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 23, mwaka jana.

Alidai mtuhumiwa alitiwa mbaroni Machi 25, mwaka jana na kufikishwa kituo cha polisi kwa mahojiano, lakini alitoroka kabla ya polisi kufanikiwa kumkamata tena Novemba 10, mwaka jana.

Upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na mtuhumiwa alirejeshwa mahabusu hadi Januari 21, mwaka huu.



Source: Mwananchi
Wahukumiwa kifungo cha mwaka moja Jela kwa kuingia nchini kinyume na sheria. Wahukumiwa kifungo cha mwaka moja Jela kwa kuingia nchini kinyume na sheria. Reviewed by Zero Degree on 1/17/2016 08:25:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.