Bomoabomoa YAHAMIA mkoani IRINGA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, January Makamba
Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewaamuru watu waliojenga nyumba mabondeni, maeneo ya wazi na kando ya barabara kinyume na sheria kuanza kuzibomoa.
Kasesela alitoa amri hiyo wakati akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo uliofanyika juzi mjini hapa.
Alisema moja ya malengo ya ofisi yake ni kuhakikisha Mji wa Iringa unakua na kufikia hadhi ya jiji na kwamba, hauwezi kufikia hadhi hiyo bila ya kujengwa kwa mpangilio.
“Sheria inasema umbali kutoka kwenye chanzo cha maji hadi eneo linalopaswa kujengwa nyumba ya kuishi ni mita 60, pia waliojenga kwenye maeneo ya wazi nao lazima waondoke. Kazi hii itakwenda sambamba na kuangalia kama wamepewa vibali na watumishi wetu ili hatua zichukuliwe dhidi yao,” alisema Kasesela.
Akizungumzia hilo, Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alishauri kazi ya kubomoa nyumba pindi itakapoanza iende sambamba na uchukuaji hatua dhidi ya wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na maofisa watendaji wa mitaa na kata kwa kuwa ni chanzo cha ujenzi holela.
“Kwa utafiti nilioufanya nimebaini watu wanaochangia kasi ya ujenzi holela ni wenyeviti wa Serikali za mitaa, maofisa watendaji wa mitaa na kata, kwani watu wengi waliojenga maeneo yasiyoruhusiwa ukifuatilia watakuonyesha nyaraka za mauziano zilizosainiwa na wahusika hawa,” alisema Kimbe na kuongeza:
“Pindi kazi ya kubomoa itakapoanza, wahusika ambao ni wenyeviti wa Serikali za mitaa, maofisa watendaji wa mitaa na kata nao wachukuliwe hatua za kisheria ili tukio kama hilo lisijirudie,” alisema.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema watu wengi wamejenga nyumba zao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kutokana na uhaba wa viwanja unaotokana na baadhi ya watu kumiliki mashamba makubwa.
Aliitaka Serikali kuyafuta mashamba hayo kwa kutumia Sheria ya Mipango Miji inayotaka watu ndani ya manispaa kuwa na uwezo wa kumiliki eka tatu tu za shamba badala ya hali ilivyo sasa kwani baadhi wanamiliki eka zaidi ya 20.
“Katika hili tuwe wakweli, wapo watu wanamiliki zaidi ya ekari 20 za mashamba ndani ya Manispaa ya Iringa, Sheria za Mipango Miji zinasema mtu ndani ya mji anapaswa kumiliki eka tatu tu,” alisema Msigwa.
Novemba 17, mwaka jana, Serikali ilitangaza kampeni maalumu ya kubomoa nyumba, vibanda vya biashara pamoja na kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya wazi kinyume cha sheria.
Bomoabomoa hiyo ilianza Novemba 18 katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam, huku mkakati huo ukitarajiwa kuendelea nchi nzima.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Desemba 22, mwaka jana alisema Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007 na Sheria ya Mazingira namba 4 ya mwaka 2004, zinakataza kujenga kwenye maeneo hatarishi kama vile mabondeni.
Lukuvi alisema kuanzia Januari hii, wizara yake itatoa ramani za mitaa kwenye ofisi za Serikali za Mitaa ili watendaji waweze kusimamia uvamizi wa maeneo. “Watendaji wakipewa ramani za mitaa yao watayafahamu maeneo ya wazi na zinakopita barabara na hivyo kuwa rahisi kuchukua hatua dhidi ya wavamizi,” alisema Lukuvi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, January Makamba alisema tatizo la uharibifu wa mazingira limekuwa na athari kwa maisha ya binadamu.
Alisema watu wanavamia vyanzo vya maji na kujenga nyumba huku wengine wakikata miti hovyo.
Makamba alisema hekta milioni moja za miti zinakatwa kila mwaka, jambo ambalo linatishia nchi kugeuka jangwa.
Alisema kuanzia mwaka huu, wizara yake itachukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaojenga kwenye kingo za maji, fukwe na kwenye vyanzo vya maji.
Kazi ya bomoa bomoa kwa Mkoa wa Dar es Salaam hasa katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, lilisitishwa na Mahakama ya Ardhi baada ya Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akishirikiana na wakazi 681 wa eneo hilo, kufungua kesi mahakamani kupinga ubomoaji wa nyumba bila kutoa njia mbadala za makazi.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi, nayo iliweka zuio la kubomoa nyumba zilizopo katika Wilaya ya Kinondoni hasa zile ambazo wamiliki walipeleka ombi lao mahakamani.
Jaji aliyesikiliza shauri hilo, Panterine Kente aliweka bayana kuwa Mahakama ya Ardhi haijaweka zuio la bomoabomoa kwa Tanzania nzima, bali kwa wale tu waliopeleka maombi ya shauri la zuio la kubomolewa nyumba zao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea na uwekaji wa alama za X na ubomoaji wa nyumba zilizopo katika maeneoa hatarishi na sehemu zisizostahili.
Source: Mwananchi
Bomoabomoa YAHAMIA mkoani IRINGA.
Reviewed by Zero Degree
on
1/12/2016 02:53:00 PM
Rating: