Museveni: Siwezi kuaachia madaraka kirahisi.
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda
Ntungamo. Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amesema hawezi kuachia madaraka kwa sababu mazao yake yote aliyoyapanda ndiyo yanaanza kutoa matunda.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo, Museveni alisema akiachia madaraka kwa sasa atakuwa hajawatendea haki raia wa Uganda.
“Wale wanaosema, ‘muache aende, muache aende’ wanapaswa kufahamu kwamba huu siyo wakati wa kufanya hivyo,” alisema Museveni wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika wilaya ya Ntungamo
“Huyu mzee aliokoa nchi hii, mnaweza kumtaka aondoke? Ninawezaje kuacha shamba la migomba ambayo nimeipanda mwenyewe na limeshaanza kutoa matunda?” alihoji Museveni na kuongeza:
“Lazima tuzingatie maendeleo, wakati wangu utafika na nitaondoka.”
Wagombea saba watashiriki kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini humo Februari 18 mwaka huu ili kumuondoa Museveni madarakani.
Kiongozi huyo aliyekaa madarakani tangu mwaka 1986, anachuana vikali na wapinzani wake, Dk Kizza Besigye na Amama Mbabazi, aliyekuwa waziri mkuu.Mbabazi alisema akishinda urais atapitisha kipengele cha muda wa rais kukaa madarakani wa vipindi viwili.
“Wakati yeye (Museveni) aliponiambia kwamba hangestaafu na kuniomba nimuunge aendelee kuwania urais , nilisema hapana na sasa niko hapa,” alisema Mbabazi kwenye mkutano wa kampeni nchini humo
“Katika siku100 za kwanza nikiwa rais, tutarejesha vipindi vya rais kukaa madarakani katika katiba na tutafanya tuwezalo kuhakikisha kuwa katika miaka mitano ya kwanza tutafanya juu chini kuandaa kizazi chenye umri mdogo ili kitwae madaraka Uganda,” alisema Mbabazi.
Source: Mwananchi
Museveni: Siwezi kuaachia madaraka kirahisi.
Reviewed by Zero Degree
on
1/12/2016 02:49:00 PM
Rating: