Loading...

Chama cha ADC, kimesema kipo tayari kwa uchaguzi Zanzibar.


Wafuasi wa ADC katika moja ya mikutano ya kampeni ya chama hicho.

Dar es Salaam. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimesema kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio utakaofanyika visiwani Zanzibar.



Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya chama hicho, Ayubu Kimangale wakati akizungumzia uchaguzi wa Zanzibar unaotarajia kufanyika hivi karibuni.

“Sisi ADC hata kesho tukiambiwa tushiriki uchaguzi tupo tayari kwa sababu hatuwezi kupata matokeo mengine zaidi ya sanduku la kura,” alisema Kimangale.

Kimangale alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na mvutano baina ya CUF na CCM kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Kwa upande wake CCM imewataka wanachama kujiandaa kwa uchaguzi huo mwezi ujao, huku CUF ikisisitiza haitashiri na kushinikiza kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kwa madai kuwa iliibuka mshindi katika urais.

Oktoba 28, mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha alitangaza kufutwa kwa uchaguzi huo wa rais, wawakilishi na madiwani kwa madai kanuni zilikiukwa.

Wakati huo huo; Bodi ya Wadhamini ya ADC, imetangaza majina saba ya kamati teule itakayoongoza chama hicho kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

Kimangale alisema jana kuwa kamati hiyo itakuwa na wajumbe wanne kutoka Tanzania Bara na watatu Zanzibar.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Jumapili Kaliki (mwenyekiti), Khamis Mohamed Kombo (makamu mwenyekiti) na Zamila Mrisho (katibu). Wengine ni Mvita Mangupili, Ibrahin Pogora, Rose Swai na Mtumwa Faiz Sadiki.

Aliwataka viongozi wa kanda, mikoa, kata, matawi na wanachama kupokea uamuzi huo wa bodi na kushirikiana na kamati hiyo.





Source: Mwananchi
Chama cha ADC, kimesema kipo tayari kwa uchaguzi Zanzibar. Chama cha ADC, kimesema kipo tayari kwa uchaguzi Zanzibar. Reviewed by Zero Degree on 1/18/2016 10:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.