Loading...

Miss Tanzania aiponza Benki ya Stanbic.


“Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha Dola milioni 6 za Marekani na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.” Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.


Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare amesababisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuitoza faini ya Sh3 bilioni Benki ya Stanbic baada ya kuhusishwa katika miamala iliyoisababishia Serikali hasara ya Sh1.3 trilioni kati ya mwaka 2012 na 2013.

Sinare ambaye alikuwa ofisa mwandamizi wa Stanbic, kwa kushirikiana na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Bashir Awale walitajwa kuhusishwa na mpango huo wa kifisadi.

Awale alifukuzwa kazi Agosti 2013 baada ya kushindwa kutoa ushirikiano kwa timu ya wachunguzi wa ndani na Sinare alijiuzulu Juni 2013.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya Stanbic Tanzania kwa ushiriki wake wa kuwezesha mkopo wa Serikali wa Dola milioni 600 za Marekani, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango alisema BoT imeiandikia benki hiyo barua za kusudio la kuitoza faini ya Sh3 bilioni.

Alisema sheria inaitaka Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 kitakachoisha Januari 30, 2016.

Mpango alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi, Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.

Ukaguzi wa BoT

Waziri alisema baada ya kuondolewa kazini na kuacha kazi kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Tanzania katika kipindi cha muda mfupi, BoT iliamua kufanya ukaguzi.

Alisema ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha.

Alisema BoT ilituma wakaguzi wake Stanbic na kubaini miamala yenye kutia shaka iliyohusu malipo kwa Kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA).

Alisema kampuni hiyo iliwezesha upatikanaji wa mkopo kwa Serikali ya Tanzania na kwamba Benki ya Standard (sasa ICBC Standard) na Stanbic Tanzania walikuwa wawezeshaji wakuu.

Mpango alisema malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa Stanbic.

Mpango alisema Septemba 29, 2015, BoT ilipokea barua kutoka Taasisi ya Upelelezi wa Makosa ya Kughushi na Rushwa ya Uingereza (SFO) ikiiomba ruhusa ya kutumia ripoti ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa mshirika wa Stanbic Bank Tanzania katika kuwezesha mkopo wa dola za Marekani milioni 600 kwa Tanzania.

“Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa sheria, ripoti za BoT hutolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika,” alisema.

Waziri alisema hata hivyo BoT haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo chake.

Alisema hatimaye Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya ya Dola milioni 32.20 za Marekani na kwamba Dola milioni 7 za Marekani zinalipwa kwa serikali ya Tanzania.

Awali, Mwanasheria wa SFO, Edward Garnier ilieleza Mahakama ya Southwark Crown, London Uingereza kuwa maofisa hao Awale na Sinare waliwataka maofisa wa Tanzania wawapatie Dola milioni 6 za Marekani (Sh1.3 bilioni) ili waweze kufanikisha mkopo wa Dola milioni 600. Dola milioni 6 ni asilimia moja ya mkopo huo wa Dola za Marekani 600.





Source: Mwananchi
Miss Tanzania aiponza Benki ya Stanbic. Miss Tanzania aiponza Benki ya Stanbic. Reviewed by Zero Degree on 1/18/2016 11:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.