Loading...

Simba: Mapinduzi imetupa fundisho.


Dar es Salaam. Kaimu kocha mkuu wa Simba, Jackson Mayanja ameridhishwa na kiwango cha timu yake, lakini ameendelea kuumizwa kichwa na safu yake ya ushambuliaji ambayo amedai bado inahitaji kufanyiwa marekebisho.

Kocha huyo raia wa Uganda aliiongoza Simba kwenye Ligi Kuu kwa mara ya kwanza juzi ilipokabiliana na Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Hamis Kiiza.

Licha ya kupata ushindi huo, washambuliaji wa Simba bado walionekana kuwa butu pale wanapolikaribia lango la Mtibwa Sugar, tatizo ambalo hata Mayanja amelibaini huku akiahidi kulifanyia kazi zaidi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja ambaye ameajiliwa Simba kama kocha msaidizi alisema kwa muda mfupi aliokaa na Simba, ameridhishwa na mabadiliko ya timu yake hasa kwenye kumiliki na kutawala mpira, lakini kinachomuumiza kichwa mpaka sasa ni safu yake ya ushambuliaji ambayo imeendelea kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi wanazotengeneza.


“Sina shaka kabisa na kiwango cha uwanjani kwani kila mmoja ameona jinsi timu ilivyocheza vizuri katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa, ingawa bado kuna suala moja ninalohitaji kulifanyia kazi ambalo ni kushindwa kufunga. Kumbuka unaweza kucheza vizuri, lakini kama hamfungi mabao inakuwa ni kazi bure,” alisema Mayanja.

Mayanja alisema kwa kuwa ndiyo kwanza ameanza jukumu la kuinoa timu hiyo, ana imani atafanikiwa kulimaliza tatizo hilo ndani ya siku chache zijazo kwani wachezaji wa Simba wamekuwa wakishika upesi kile anachowaelekeza mazoezini.

Tatizo la ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Simba limeonekana kuwa sugu katika siku za hivi karibuni, licha ya timu hiyo kuwa na washambuliaji mahiri kama Dan Lyanga, Rafael Kiongera, Musa Mgosi, Hamis Kiiza na Ibrahim Ajibu.

Kocha Mayanja ana kaimu ukocha mkuu katika klabu ya Simba baada ya Dylan Kerr raia wa Uingereza aliyekuwa kocha mkuu kutimuliwa na viongozi wa Simba ambao hawakufurahishwa na mwenendo wa klabu hiyo katika Ligi Kuu Bara ambayo inashika nafasi ya tatu huku pia ikifanya vibaya katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar baada ya kutolewa katika hatua ya nusu fainali.



Source: Mwananchi
Simba: Mapinduzi imetupa fundisho. Simba: Mapinduzi imetupa fundisho. Reviewed by Zero Degree on 1/18/2016 06:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.