Loading...

Deni la kiasi cha TSh1.13 bilioni kuziponza Polisi, Magereza.


Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru.
       
Moshi. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (Muwsa), imetoa siku 14 kwa taasisi tatu za Serikali mkoani Kilimanjaro, kulipa malimbikizo ya madeni yanayofikia Sh1.13 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru amesema leo kuwa baada ya muda huo kumalizika, watalazimika kuzikatia huduma ya maji taasisi hizo.

Amesema Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), inadaiwa Sh528.6 milioni, Chuo cha Mafunzo cha Polisi (MPA) Sh401.9 milioni na Magereza Sh203.7 milioni.

Msiru amesema changamoto kubwa inayoikabili Mamlaka yake kwa sasa ni pamoja na ya kutolipwa madeni yake na taasisi za Serikali, hali inayoathiri utekelezaji wa mipango yao ya kuboresha huduma za maji mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo, amesema juhudi zimefanyika kufuatilia madeni hayo, lakini Serikali imeshindwa kuyalipa licha ya mwaka jana kuanza kulipa kidogo, lakini baadaye ilisitisha bila maelezo.

“Tunajiuliza hii mamlaka itajiendeshaje wakati fedha zote zimeshikiliwa na taasisi hizo? Februari 28, 2015, bodi ya wakurugenzi ilikutana na uongozi wa MPA lakini imeonekana kuwa uwezo wa kulipa madeni yao haupo,” amesema.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa katika vikao hivyo ilibainika kuwa Hazina ndiyo inayostahili kulipa malimbikizo hayo lakini hakuna mwanga wa kulipwa na wamelazimika kutoa notisi hiyo.

“Tuna miradi mingi ya kutekeleza ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha. Fedha za miradi hiyo tunayo lakini zimeshikiliwa na taasisi za Serikali,” amesema Msiru.

Mkuu wa MPA, Matanga Mbushi amesema wenye wajibu wa kulipa madeni hayo ni Hazina ambao tayari wameshawaandikia barua ya kuwakumbusha.

Amesema Muwsa wanapaswa wawe na subira kwani deni hilo liko kwenye mchakato wa kulipwa, lakini kama watasitisha huduma watalazimika kufunga chuo chenye polisi wanafunzi 3,989.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Mungi amesema asingeweza kulizungumzia kwa kina suala hilo, lakini amesisitiza kuwa inayodaiwa ni Serikali kupitia Idara ya Polisi.

Naye Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, Venant Kayombo amesema taasisi yake inadaiwa madeni ya maji na umeme ambayo yataanza kulipwa kulingana na fedha watakazokuwa wakitumiwa kutoka Hazina kama walivyoanza kufanya.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Deni la kiasi cha TSh1.13 bilioni kuziponza Polisi, Magereza. Deni la kiasi cha TSh1.13 bilioni kuziponza Polisi, Magereza. Reviewed by Zero Degree on 1/06/2016 08:36:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.