Loading...

Karume na jitihada za kuondosha ubaguzi Z’bar.

Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Hahaha! Haha! Ha! Aliangua kicheko cha kushangaza kilichojaa kebehi na kejeli, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, mara tu alipopokea taarifa kwamba Mswahili mmoja miongoni mwa watendaji na swahiba wake wa karibu alikataliwa posa katika moja ya familia tajiri ya watu wenye asili ya Bara Asia, waliokuwa wakiishi maeneo ya Mwera, nje kidogo ya mji wa Unguja, alikokwenda kumposa binti mwanafamilia hiyo.



Mzee Karume hakuishia kicheko hicho kilichohanikiza kwa swahiba yake Mwanamapinduzi huyo bali aliongeza kutoa wasia akisema, “Eeh! Bwana wee! Nenda kapose kwa watu wa saizi yako ‘kiasi chako’ usikurupuke kwengine si maji yako bwana …” Anasimulia mzee Mohammed Makame mkutubu katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye anasema habari hizo alisimuliwa na Mzee Shamsi aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Afro Shirazi.

Wasia na kebehi hiyo ya Mzee Karume kwa Mwanamapinduzi mwenzake zilikuja si zaidi ya mwaka mmoja tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, ambapo sasa ni miaka 52 ya maadhimisho yake.

Fikiria, mwanamapinduzi huyo ni moja ya nguzo za asasi iliyotawala visiwani wakati huo, Chama cha Afro Shirazi, ASP, zama hizo watawala wake wakiwa wamejawa na joto la umapinduzi, ujabari, na tamaa ya kila kilichorandaranda na kunawiri mbele yao.

Watu wa Unguja na Pemba hawakuchukulia kwa wepesi wala hawakudharau kicheko cha yeyote miongoni mwa wanamapinduzi hata iwapo kiliendana na wosia, wakielewa kwamba muda wowote kingeliweza kugeuka machozi ya mamba au ushauri wa mfalme ambao ni amri, na hatimaye kuleta fadhaa na simanzi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa kicheko hicho cha wanamapinduzi na vicheko vinginevyo ambavyo hatimaye viliishia maamuzi mazito ambayo ni pamoja na kile kilichojulikana kuwa ni Kanuni ya Rais ‘Presidential Decree No 6’ ya mwaka 1966.

Jina la kanuni ‘sheria’ hiyo ni Sheria ya Ndoa Maalum na Usajili (ya Marekebisho ya Sheria ya Dini) ya Mwaka 1966 (Marriage (Solemnization and Registration Decree).

“Ni miongoni mwa sheria 40 kandamizi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, alisema Jaji Francis Nyalali na pia ilinakili Ripoti ya Tume yake ya uchunguzi juu ya Marekebisho ya Katiba, mwanzoni mwa miaka ya 90.

Pamoja na kero mbali mbali zilizofungamana, kanuni hiyo ya sheria ilitoa mwanya wa kulazimisha ndoa za mabavu, za kuteza nguvu, hata iwapo mposaji alikataliwa au kupingwa na familia ‘alikopiga hodi’ kumtaka binti yao, jeuri ya cheo na madaraka ilitumika kukomesha na kuadabisha, si wakubwa tu wa kaya bali pia hata wadogo ndani yake walikiona cha mtemakuni.

Binti alilazimishwa kuolewa pasi na ridhaa yake wala ridhaa ya walii ‘mzazi, mlezi au msimamizi’ wake, alitwaliwa kwa nguvu na hatimaye waliobaki walihilikishwa, kupitia kivuli cha kanuni hiyo, pindipo mtu hakuujua upenyo wa kukimbilia.

Kuliiibuka wakati fulani wazee waliutumia sana usemi wa Waswahili wa Pwani, ‘usalama wa Barawa wa kwenda mbio na mali ikatwawa’, nahisi huo ndio ulikuwa muda wake mwafaka, kwani pamoja na mzazi au mlezi kukimbia ikiwezekana hata kukimbilia ughaibuni kunusuru maisha yake na wanawe, lakini hatimaye mali yake kutwaliwa.

Kanuni hiyo, mathalan katika Kifungu cha 17 A (1) kinasema kuwa: “Hakuna mtu atakayeridhiwa kukataa ndoa iliyokusudiwa isipokuwa katika mazingira ambayo upande wowote wa ndoa hiyo umekabiliwa na: (a) kutiwa hatiani kwa kosa la wizi (b) magonjwa ya uasherati au (c) matatizo ya uendawazimu.”

Haikuwa rahisi kwa familia tajiri au zilizojihisi kuwa na hadhi fulani kuridhia kumuozesha binti yao kwa thamani ya ridhaa tu kwamba wapo waliokuja kubisha hodi, kuepuka kitanzi cha kanuni hiyo ikizingatiwa kwamba, ndoa iliyokamilika haitegemei vigezo hivyo pekee.

Zipo familia nyingi wahanga wa hayo, zimeupokea kuwa ni ‘msala usioepukika’ ingawa upande wa pili ni ‘kikombe cha udhia na machungu’ licha ya kuwa hakuna ambaye angeliweza kukataa mwanzoni mwake hasa akiwa tumboni kwamba asizaliwe na wazazi fulani.

Ukimaizi kwa mbali utabaini kuwa kawaida ya ndoa, licha ya miongoni mwa wanandoa wahusika kukabiliwa na moja ya hitilafu zilizoainishwa hapo juu, bali pia ipo misingi ya lazima ambayo ni pamoja na ukomavu wa akili hasa kwa muoaji, kivutio na hisia za maono au motisha za kila mmoja, wachilia mbali uwezo wa matunzo, huduma na nasaba, kama siyo kabila la wanaopendelea fungamano la taasisi hiyo.

Katika Kifungu cha (2) kimeelezwa kwamba: “Yeyote atakayekaidi, kupinga au atakayekiuka Kanuni hiyo angelikuwa ametenda kosa la jinai na angelihukumiwa kifungo cha gerezani kisichopungua miaka 6 au kulipa faini isiyozidi 15,000 au hukumu zote mbili, na ikibidi mzazi au mlezi huyo kuchapwa viboko 24 mahakamani.”

Ni makubwa machungu na maumivu ya kanuni hizo, na upande mwingine tija ya kitambo miongoni mwa walioneemeka nayo, ambapo tunashuhudia mpaka sasa baadhi ya watu wanaendelea kusotea maisha nje ya nchi, pale walipoanza kusakwa kwa kukataa au hata kukaidi kuwaozesha binti zao kwa watu ambao hawakuwaridhia.

Nilipokuwa nimejichimbia kupitia vitabu vya Kanuni hizo mikononi mwa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, katika jengo lao lililopo kati ya mitaa ya Mazizini na Mombasa Unguja, nilizima kidogo, nikasita na kisha nikaamua si vyema kutaja kila athari ya machungu hayo, bali ni maji yaliyokwishamwagika hayazoleki.

Baada ya kanuni hiyo kupitishwa, Zanzibar ilishuhudia ndoa nyingi za mchanganyiko wa waafrika na waarabu au waafrika na wahindi.

Kwa upande wa faida, si vibaya tukisema kuwa kanuni hiyo ilisaidia kuondosha ubaguzi kwa kiasi kikubwa na hicho ndicho kizazi cha Wazanzibari wa leo, kizazi chotara ambacho kimsingi hakipaswi tena kuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile kama wanataka kujinasibu kuwa wao ni Wazanzibari.




Source: Mwananchi
Karume na jitihada za kuondosha ubaguzi Z’bar. Karume na jitihada za kuondosha ubaguzi Z’bar. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 02:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.