Lowassa aibukia bungeni Dodoma.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
Dodoma. Jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa limeibuka bungeni baada ya mbunge mmoja kuiuliza Serikali kuwa haioni haja ya kubadili sheria ili viongozi wa zamani wa kitaifa wasipewe stahiki zao iwapo wanahama vyama baada ya kutoka madarakani.
Mbunge huyo wa Dimani, Hafidh Ali Tahir alihoji kama Serikali haioni kuwa iko haja ya kufanyia marekebisho sheria ya kuwapa stahiki zao baadhi ya mawaziri wakuu wastaafu waliohama vyama vyao kwa kuwa zilitokana na nguvu za vyama walivyovihama.
“Msingi wa swali langu ulikuwa ni kuangalia suala la ulafi wa madaraka na hii si kwa mawaziri wakuu wastaafu pekee, bali hata huko upande wa upinzani kuna mbunge aliwahi kuwa katibu mkuu wa wizara mbalimbali, naomba ufafanuzi,” alisema Hafidh huku akimtaja Lowassa kuwa aligombea urais kwa tiketi ya upinzani baada ya kuihama CCM.
Hata hivyo, Serikali ilimtetea Lowassa kuwa uamuzi wake wa kugombea urais baada ya kuihama CCM ulikuwa halali na ndiyo maana bado anastahili kulipwa posho kama stahiki zake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki alijibu kuwa kitendo cha Lowassa kugombea urais ni haki yake ya msingi kama ilivyo kwa Watanzania wengine.
“Haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa au kujihusisha na masuala ya siasa ni ya kikatiba, na kwa kuwa haki hizi haziwezi kuzuiwa au kuingiliwa, ni wazi kuwa suala la kufanyia marekebisho sheria ya mafao kwa viongozi wa kitaifa waliostaafu, bado haliwezekani,” alisema Kairuki.
Alisema kuwazuia mawaziri wakuu wa zamani au viongozi wengine wastaafu wa kitaifa kujiunga na chama chochote cha siasa, itakuwa kinyume na Katiba ya nchi.
Waziri Kairuki alisema Lowasa hajapoteza stahiki zake isipokuwa kama angepata nafasi hiyo, kungekuwa na uamuzi mwingine.
Hata hivyo, hoja hiyo ilionekana kupigiwa kelele na wabunge wengi, akiwamo kiongozi wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe ambaye alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi wanaotumia mwamvuli wa CCM kuwanyima haki wanasiasa wa upinzani.
Lakini Waziri Kairuki alisema kama watumishi wataingilia masuala ya kisiasa, watakuwa wanakiuka sheria. Hata hivyo, alisema wanapokuwa kwenye utumishi hutakiwa kutekeleza Ilani ya CCM, hivyo hawana budi kufanya hivyo.
Source: Mwananchi
Lowassa aibukia bungeni Dodoma.
Reviewed by Zero Degree
on
1/28/2016 01:11:00 PM
Rating: