Loading...

Lowassa: Najiandaa kwa uchaguzi 2020.


Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa (kulia), akizungumza na wafanyabiashara wa Kariakoo wa Timu Mabadiliko walipomtembelea ofisini kwake Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema hajakata tamaa na ana nguvu za kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza na viongozi tisa wa wafanyabishara wa Kariakoo wanaojiita wapenda mabadiliko ambao walimtembelea ofisini kwake jana, Lowassa alisema mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine.

Lowassa, ambaye aliongeza ushindani kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kuihama CCM na kugombea urais kwa tiketi ya Chadema, alisema bado miaka mitano kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika na kwamba muda huo si mrefu kwa maandalizi.

Lowassa, ambaye aliweka rekodi ya kuwa mgombea urais wa upinzani aliyepigiwa kura na wengi baada ya kupata kura milioni 6.07, alisema maandalizi ya uchaguzi mwingine yameshaanza na akawataka wafuasi wa chama hicho kutokata tamaa.

“Niko salama, niko ‘fit’ na nina morali,” alisema Lowassa ambaye wapinzani wake kwenye Uchaguzi Mkuu walikuwa wakidai kuwa ana matatizo ya kiafya.

“Kama tulivyoshinda uchaguzi uliopita na huu wa mwaka 2020 tutashinda,” alisema.

Alitoa mfano wa mwanasiasa mmoja wa Marekani ambaye aligombea urais mara tano na kushindwa, lakini baadaye alishinda na kuwa rais.

“Nami sitakata tamaa, nitaendelea kugombea kwa sababu watu wananipenda,” alisema Lowassa.


Akizungumzia matokeo ya uchaguzi, Lowassa alisema kama angepinga matokeo ya urais hadharani, kungetokea maafa kwa sababu anaamini alipigiwa kura zilizotosha kuwa rais.

Alisema Katiba mbaya ndiyo iliyomfanya atumie busara na kukaa kimya.

“Ningeamua kupinga matokeo hayo hadharani watu wangechinjana kwa visu na yangetokea maafa makubwa, nikaona ya nini; nikaamua kutumia busara na kunyamaza kimya,” alisema na kuongeza: “Nilitafakari na kutumia busara nikaona hata kama nitaenda Ikulu lakini watu wengi wakawa wamekufa, ingekuwa haina maana.”

Alisema anashukuru kwa uamuzi huo kwani Serikali iko madarakani na nchi iko salama ingawa yeye na watu wengi wanaamini kwamba matokeo hayakuwa sahihi.

Lowassa alisema baadhi ya mambo mabaya katika Katiba ya sasa ni kuwa matokeo ya urais hayawezi kupingwa mahakamani.

“Hii ni dosari kubwa ambayo inahitaji wabunge kupambana haswa,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Severini Mushi alisema timu ya mabadiliko ya wafanyabiashara hao bado imeshikamana licha ya matokeo ya urais kuonyesha kwamba Lowassa ameshindwa.

“Tulisikitika, lakini bado tumeshikamana na hatukati tamaa,” alisema Mushi na kuongeza:

“Baadhi ya wafanyabiashara wenzetu hadi leo hawaamini kama kweli Lowassa ulishindwa uchaguzi.”

Kuhusu uamuzi wa Serikali kuzuia wanasiasa wa upinzani kufanya mikutano ya kushukuru wananchi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, Lowassa alisema atafanya ziara muda ukifika.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi nitapita mikoani kuwashukuru, hivi sasa bado tuko kwenye mazungumzo na vyombo vya dola,” alisema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipiga marufuku ziara za wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu kuwashukuru wananchi, akisema hazina tija na akataka walioshinda tu ndiyo wafanya hivyo. Kabla ya agizo lake, makamanda wa polisi wa baadhi ya mikoa walishapiga marufuku mikutano ya kisiasa.

Lowassa ilikuwa aanze ziara ya kuzunguka nchi nzima mwezi uliopita, lakini haikuwezekana kutokana na maagizo hayo.

Lowassa pia alizungumzia bango lililobebwa na vijana wa CCM ambalo lilikuwa na maneno ya kibaguzi wakati wa sherehe za Mapinduzi Zanzibar na kuwataka viongozi wakuu wa chama hicho tawala kukemea jambo hilo kwa kuwa hali hiyo ikiendelea italigawa Taifa.

“Si kila mtu anaweza kukemea ubaguzi huu, ni lazima ajitokeze kiongozi wa juu anayeheshimika alitolee ufafanuzi na kulikemea,” alisema.

Bango hilo liliandikwa “machotara Hizbu, Zanzibar ni ya Waafrika”, lakini tayari mkuu wa mawasiliano na umma wa CCM, Daniel Chongolo ameshatoa tamko la kulaani.

Lowassa alitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumtangaza mshindi wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwa mwaka jana kwani uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Kwa upande wake, mwanachama wa Chadema, Goodluck Ole Madeye ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema wafuasi wa chama hicho waanze maandalizi ya uchaguzi ujao.

“Imekuwa ni tabia ya watu kusubiri Uchaguzi Mkuu unapokaribia ndiyo tunaanza maandalizi, tuanze kujiandaa sasa,” alisema Ole Medeye.

Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema wamejiandaa kikamilifu kwenye uchaguzi wa umeya katika manispaa za Kinondoni na Ilala kwa kuhakikisha Ukawa ndiyo wanashinda.

Alisema waligundua kila rafu `zilizochezwa’ na CCM na kuzifanyia kazi.

“Piga, ua umeya tunachukua Ilala na Kinondoni kwa sababu mbinu zote zimefichuka na madiwani wetu wana ari na moyo wa kuchagua Ukawa,” alisema.

Malalamiko ya Lowassa

Siku tatu baada ya Uchaguzi Mkuu, Lowassa aliilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwakamata wataalamu wa Chadema waliokuwa wakipokea matokeo ya kura za urais, akisema wakati wakikamatwa chama hicho kilikuwa kikiongoza kwa asilimia 60.

Lowassa alisema uvamizi huo ulifanyika kwa makusudi kwa lengo kuchakachua matokeo.

“Wakati tukijua kwamba NEC ndiyo yenye mamlaka pekee ya kisheria ya kutangaza matokeo ya urais, tunapenda kuwataarifu Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba hadi wakati uvamizi huo ulipofanyika kura zetu za urais tulizokuwa tumezikusanya zilikuwa zikionyesha tunaongoza kwa asilimia zaidi ya 60,” alisema Lowassa wakati huo.

Baadaye, Lowassa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji wakatangaza kutokubaliana na matokeo yatakayotangazwa na kuitaka NEC kusitisha kutangaza matokeo ya urais hadi uhakiki ufanyike kwenye vituo vyote vya kupigia kura.

Novemba 14, 2015

Baada ya kushindwa uchaguzi, Lowassa alisema ataendelea kushiriki kikamilifu katika siasa na mapambano ya kudai Katiba Mpya.

Alisema kasi ya ufanyaji siasa itaongezeka kuliko ilivyokuwa awali, akisema kwa sasa anaweza akawa “amepoteza pambano lakini siyo vita”.

Alisema Ukawa itaendelea kudai Katiba Mpya ya wananchi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na tume huru ya uchaguzi na Serikali inayowajibika kwa umma.

Alisema bila ya Katiba mpya, Tanzania haitakuwa na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikteta. Aliwataka wananchi wote kuunga mkono harakati za utafutaji wa Katiba Mpya kwani huo ndiyo utakuwa mwongozo wa mambo yote ya nchi.



Source: Mwananchi
Lowassa: Najiandaa kwa uchaguzi 2020. Lowassa: Najiandaa kwa uchaguzi 2020. Reviewed by Zero Degree on 1/15/2016 03:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.