Loading...

Waziri ataka KUFANYIKE UCHUNGUZI WIZI WA MUDA WA MAONGEZI katika simu.


“Malalamiko hayo ni ya wateja wanaojiunga na vifurushi kuto kuwa na uhakika wa jinsi makato yao ya muda wa maongezi na vifurushi vya intaneti yanavyofanyika na wale wanaoibiwa fedha zao na matapeli wanaoingilia mawasiliano ya simu zao, mbaya zaidi wanapotoa taarifa hazishughulikiwi kwa haraka,” Waziri Ngonyani.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ichunguze iwapo kuna wizi unaofanywa na kampuni za simu kwa wateja wake.

Ngonyani alitoa maagizo hayo jana katika hafla ya uzinduzi wa duka la ‘Airtel EXPO’ linalotoa huduma mbalimbali za simu na elimu ya matumizi ya vifaa vya mawasiliano akisema amepokea malalamiko ya aina mbili kutoka kwa Watanzania wanaotumia huduma za kampuni za simu nchini.

Ngonyani alisema kutokana na mazingira hayo, imekuwa ikijengeka taswira kwamba, watumishi wa kampuni za simu wanahusika katika wizi huo. Aliiagiza TCRA kuchunguza tuhuma hizo huku akiwataka wananchi kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka hayo ili kutafuta ufumbuzi.

Kwa mujibu TCRA, Watanzania milioni 32 wanatumia huduma simu za mkononi, sawa na asilimia 67 huku takriban wateja milioni nane wakitumia za intaneti.

Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema malalamiko yote ya wateja wao yamekuwa yakitafutiwa ufumbuzi kwa njia mbalimbali.

“Wateja wote tunawasaidia kupitia kituo cha huduma kwa mteja ambacho kinafanya kazi wakati wote. Kwa upande wetu, wateja wanasikilizwa,” alisema.

Msemaji wa TCRA, Innocent Mungy alisema wamepokea maagizo ya naibu waziri na wataanza kuyatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya TCRA ya 2003 na ile ya Mawasiliano na Posta ya 2010.

“Lakini pia tuna kanuni zinazotusaidia katika utekelezaji wa sheria hizo, kwa hiyo agizo hilo litashughulikiwa, lakini siwezi kusema lini,” alisema.

Mungy alisema malalamiko ya wateja kuhusu hisia za kuibiwa yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi kila siku na kupokewa sehemu husika ili kutafutiwa ufumbuzi.

“Kwanza malalamiko yanayohusu kampuni fulani yanapokewa na kampuni husika ili kujibiwa, kabla ya TCRA hatujahusika kumaliza malalamiko ya mteja huyo,” alisema.

Hata hivyo, alisema bado elimu inahitajika zaidi katika matumizi ya ofa za vifurushi vya intaneti na muda wa maongezi.

“Kuna mambo mengine yanachangiwa na simu zetu za kisasa, kwani unaweza kuliwa fedha zako kwa kosa la kujiunganisha au kutokujua jinsi ya ulaji wa vifurushi kwenye simu,” alisema.

Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba alitoa adhabu ya faini ya Sh125 milioni kwa kampuni tano za simu za mkononi kwa kushindwa kuweka mazingira salama kwa wateja. Kampuni hizo ni Airtel, Tigo, Smart, Halotel na Zantel ambazo zilitakiwa kulipa faini kwa sababu zilishindwa kutii agizo la mamlaka hiyo ya kulinda wateja wake huku vitendo vya utapeli wa kutuma ujumbe wa udanganyifu na ulaghai kwenye mitandao vikiendelea.



Source: Mwananchi
Waziri ataka KUFANYIKE UCHUNGUZI WIZI WA MUDA WA MAONGEZI katika simu. Waziri ataka KUFANYIKE UCHUNGUZI WIZI WA MUDA WA MAONGEZI katika simu. Reviewed by Zero Degree on 1/15/2016 03:13:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.