Loading...

Mashindano ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 yazinduliwa.


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Novatus Makunga akizindua rasmi mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 Mjini Moshi. 



Wengine ni wadhamini wakuu wa mbio hizo kutoka kushoto, Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo, Meneja Mauzo wa Kampuni ya Bia Tanzania-Kilimanjaro na Tanga, Richard Temba, Mwenyekiti wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro, Listone Metacha na Meneja Masoko wa Kampuni ya mafuta ya GAPCO, Caroline Kakwezi. Uzinduzi huo ulifanyika Kibo Palace Homes.




Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania, Caroline Kakwezi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2016 Mjini Moshi.



Wadhamini wa Kilimanjaro Marathon 2016 wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mbio hizo Mjini Moshi.



Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo akizungumza wakati wa uzinduzi huo.



Meneja Mauzo wa Kampuni ya Bia Taanzania-Kilimanjaro na Tanga, Richard Temba akizungumza wakati wa uzinduzi huo.



Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga akizungumza wakati wa uzinduzi huo.



Mkurugenzi wa Wild Frontiers, John Addison ambaye ndio muandaaji wa mbio hizo akitoa neno la shukrani wakati wa uzinduzi huo.


Mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 zimezinduliwa Mjini Moshi huku ikiwa imebaki takriban mwezi mmoja kabla yam bio hizo kufanyika.

Uzinduzi huo ulifanyika Kibo Palace Homes Mjini Moshi na kuhudhuriwa na wadadhamini wa mbio hizo na wadau mbalimbali wa riadha kuonesha ukubwa wa tukio hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, Meneja wa Mauzo wa TBL Kilimanjaro na Tanga, Richard Temba alisema mbio hizo zitafanyika Februari 28, 2016 wilayani Moshi na zitahusisha wanariadha wa ndani na nje ya nchi kutoka pande mbalimbali za dunia.

“Tumeonelea ni vizuri kuzindua mbia hizi rasmi hapa Moshi ambako zitafanyika ili kuashiria kuwa mambo yameiva,” alisema.

“Kilimanjaro Premium Lager imeingia mwaka wake wa 14 kama mdhamini mkuu wa mbio hizi, kwa mafanikio makubwa na kuyafanya kuwa moja ya mbio kubwa zaidi za marathon barani Afrika, kwani kwa sasa hujumuisha zaidi ya wanariadha 7,000 kutoka nchi zaidi ya 45 kote duniani,” alisema Temba.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wadhamini wengine wa mashindano hayo ni Tigo kwa 21km, Gapco kwa 10 km-viti vya magurudumu na baiskeli ya kunyonga kwa mkono na Grand Malt-5km. Wadhamini wengine ni pamoja na KK Security, TPC Limited, FNB, Kibo Palace, Kilimanjaro Water, CMC Automobile, Rwandair na Keys Hotel.

Alisema Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya Tsh milioni 500 katika mashindano haya na kuwa hapo baadaye watatangaza mchanganuo mzima wa zawadi zitakazotolewa.

Alitoa shukurani za pekee kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) zamani kikiitwa MUCCoBS kwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo.

Akizindua mbio hizo Mjini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga aliwapongeza Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wengine na waandaaji kwa kujielekeza vyema kila mwaka, akiongeza kuwa mashindano yametokea kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya kimichezo ndani na nje ya nchi.

“Mashindano haya pia yamekwenda mbali zaidi katika kukuza utalii kwani wanariadha wa kimataifa na wageni wao hufanya utalii baada ya mashindano na hiyo kufaidisha uchumi wa nchi,” alisema huku akisisitiza kuwa mbio hizo zitatoa fursa nyingi sana hasa za kibiashara.

Aliwataka wanariadha wa Tanzania kuhakikisha wanajiandaa vyema ili watwae zawadi nyingi zaidi kwa kadiri zilivyopangwa kwa kila mbio. Aliongeza kwamba wizara yake inaunga mkono kabisa ubunifu kama huo na kuzitaka kampuni nyingine kufuata nyayo hizo kwa kudhamini mashindano hayo ya kila mwaka.
Aliwapongeza waandaaji, Wild Frontiers, waratibu wa kitaifa-Executive Solutions, Chama cha Riadha Tanzania (RT) na wizara yenye dhamana ya michezo kwa kuhakikisha siku zote kwamba tukio hili linafanikiwa.

“Mbio hizi zimeleta mwamko mpya katika riadha hapa nchini kwa kuwapa fursa vijana wetu wanaochipukia kuweza kujipima na wanariadha mashuhuri kimataifa. Changamoto hii imekuwa na faida kubwa ambapo vijana wetu wameweza kutambua uwezo wao na kuweza kujiamini zaidi wanapoenda kushiriki mashindano mbalimbali kwenye nchi za kigeni,” alisema.

Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alisema kwamba kampuni yake imefurahishwa kupata fursa ya kudhamini mbio za nusu marathoni kwa kilometa 21 kwa mwaka wa pili mfululizo.

“Natoa rai kwa washiriki wajiandae vizuri ili safari hii tuweze kunyakuwa mataji mengi,” alisema Kinabo.

Meneja Masoko wa Gapco Tanzania Caroline Kakwezi ambaye kampuni yake inadhamini mbio za kilometa 10 kwa wanaotumia viti vya magurudumu na wale wanaonyonga baiskeli kwa mikono ambazo wanazidhamini, alisema zimekuwa na mvuto mkubwa na ushindani mkubwa pia na kwamba katika mwaka wao wa tano katika udhamini wameshuhudia mbio hizo zikikuwa.

“Tunawashukuru wateja wetu wote kwa kuendelea kutuunga mkono safari hii tutaoa usafiri, malazi na chakula kwa washiriki wote kutoka Dar es Salaam katika mbio hizi za walemavu na yote haya hayawezekani bila ushirikiano tunaopata kutoka kwa wateja wetu,” alisema.



Source: GPL
Mashindano ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 yazinduliwa. Mashindano ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 yazinduliwa. Reviewed by Zero Degree on 1/22/2016 07:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.