Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi visiwani humo baada ya matokeo ya uchaguzi uliopita kufutwa.
Uchaguzi huo sasa utafanyika Jumapili Machi 20, 2016. Tangazo hilo limetolewa na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.
Bw. Jecha amesema tarehe hiyo iliamuliwa na tume baada ya mkutano hapo jana.
“Uchaguzi huo utahusisha uchaguzi wa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani na hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wala mikutano ya kampeni,” amesema Jecha.
“Wagombea wote walioteuliwa hapo awali wataendelea kuwa wagombea katika uchaguzi huu.”
Chama cha Wananchi (CUF) kimekuwa kikipinga kurudiwa kwa uchaguzi. Chama hicho mapema mwezi huu kilionya kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha vurugu.
Viongozi wa chama hicho walisusia maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi wiki iliyopita.
Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa tayari kimewashauri wanachama wake visiwani wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, tangazo lililoshutumiwa vikali na viongozi wa CUF.
Source: GPL
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi.
Reviewed by Zero Degree
on
1/22/2016 07:09:00 PM
Rating: