Loading...

Ukawa wapinga uteuzi wa kamati uliofanywa na Spika wa Bunge.


Spika Job Ndugai

Dodoma. Spika Job Ndugai amefanya uteuzi wa wajumbe wa kamati 18 za Bunge, uteuzi ambao umepingwa na viongozi wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa kwa maelezo kuwa umefanyika bila kuzingatia masuala muhimu.

“Tumeagiza wabunge wote wa Ukawa kutoshiriki kuchagua wenyeviti wa kamati hizi,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika mara baada ya kutangazwa kwa kamati hizo.

“Ilikuwa tuzungumze leo (jana) na wanahabari, lakini tumeahirisha hadi kesho (leo) kwa sababu tumebaini uteuzi huu hauko sawa. Tunataka kufanya uchambuzi wa kina.”

Licha ya Ukawa kutangaza kutoshiriki, Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya aliwaeleza waandishi mara baada ya kutangazwa kwa kamati hizo kuwa uchaguzi wa wenyeviti na makamu wa kamati hizo ungeanza mara moja kwenye vikao vya ndani.

Jana jioni, viongozi wa vyama vya upinzani, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Magdalena Sakaya (CUF), na Tundu Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, walikutana kujadili uteuzi huo, baadaye kuitisha kikao cha ndani cha wabunge wote wa Ukawa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa.

Hoja ya Ukawa ilianza baada ya kupata fununu ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo kwa mujibu wa taratibu za mabunge ya Jumuiya za Madola, lazima ziongozwe na wabunge kutoka Kambi ya Upinzani.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, ibara ya 116 (11); wenyeviti wa kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya umma (PAC na Laac) watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani. “Sisi tulitaka tupendekeze wabunge wa upinzani wanaopaswa kugombea uenyekiti katika kamati hizo mbili, si kupangiwa. Tumekuwa tukipangiwa muda mrefu na kubaini kuwa wenyeviti wa kamati hizo wanawekwa na CCM,” alisema Sakaya.

Katika uteuzi huo, wabunge wa upinzani walioteuliwa kuwa wajumbe wa kamati za PAC na Laac ni wale ambao hawana majina makubwa na wageni katika chombo hicho cha kutunga sheria, jambo ambalo Ukawa waliligusia na kupinga jinsi uteuzi ulivyofanyika.

Katika ufafanuzi wake, Mnyika alisema:“Tumebaini udhaifu mkubwa si katika PAC na Laac, bali katika uteuzi wa kamati zote. Hili jambo halikubaliki kabisa.”

Alisema ili kuweka mambo sawa,ni lazima wakutane na wabunge wote wa Ukawa na kuwafafanulia kasoro zilizopo katika uteuzi huo na kisha kuja na tamko la pamoja.

Taarifa zaidi zililieleza kuwa wabunge wazoefu, wenye msimamo na uelewa mkubwa kuhusu masuala mbalimbali, wameteuliwa kuwa wajumbe wa kamati nyingine badala ya PAC na Laac. Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililla alisema uchaguzi wa viongozi wa kamati ungeweza kusitishwa kama wangekuwa wametoa taarifa ya kuomba usifanyike.

“Kama hawakusema halafu kule kwenye kamati hawaonekani na akidi ikatimia watakaokuwa katika uchaguzi wataendelea tu. Kama akidi itatimia hakuna kanuni inayowauzia wabunge wengine wasifanye uamuzi unaotakiwa,” alisema. “Kwa hoja yao hainisumbui sana. Kama wangekuwa wamemwandika barua Spika kulalamika na kumwomba asitishe uchaguzi katika kamati,

lingekuwa jambo jingine, lakini mpaka sasa (jana jioni) hatujaona hayo mazungumzo.”

Alisema wabunge wa CCM ni wengi kuliko wa upinzani na katika kila kamati wapo zaidi ya nusu na akidi ni theluthi moja.

“Kwa maana hiyo wabunge wa CCM wanaweza kufanya uamuzi na kupata wenyeviti na makamu wenyeviti,” alisema. Kuhusu kamati ya PAC na Laac, alisema uchaguzi utafanyika, ila wabunge watachagua makamu wenyeviti tu.


Source: Mwananchi
Ukawa wapinga uteuzi wa kamati uliofanywa na Spika wa Bunge. Ukawa wapinga uteuzi wa kamati uliofanywa na Spika wa Bunge. Reviewed by Zero Degree on 1/22/2016 12:32:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.