Loading...

Utapeli TIBA MBADALA wabainika.


WAKATI idadi ya watu wanaoamini katika tiba ya mitishamba badala ya hospitali ‘Tiba Mbadala’ inayotolewa na kliniki mbalimbali nchini ikizidi kuongezeka, Oparesheni Fichua Maovu ya Global Publishers ‘OFM’ imebaini udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya matabibu katika tiba hizo, Risasi Jumamosi linakumegea.




Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na WatotoDk. Hamis Kigwangalla alipotembelea Kituo ya Tiba Asilia ya Fore Plan Clinic kilichopo Ilala -Bungoni, Dar wiki chache zilizopita.




Baadhi ya madawa

Kwa mujibu wa mhudumu wa kliniki maarufu jijini Dar (jina lipo), madawa mengi yanayotolewa kwa wagonjwa si ya asili kama yanavyotangazwa, ni mchanganyiko wa vumbi la miti pori isiyo na sumu na dawa za kisasa zinazopatikana hospitalini ambazo husagwa.


Majani ya Mlonge

“Sikia, tunafahamu kinachoendelea tunakaa kimya kwa sababu tunapata riziki. Katika dawa mia moja utakazoambiwa ni za asili, mbili au tatu ndiyo kweli zimetokana na mitishamba moja kwa moja, nyingine siyo,” alisema mhudumu huyo.

KWANI INAKUWAJE?

“Kwa mfano kuna watu wanakuja kwa maumivu ya miaka mingi ya mgongo au mwili, kinachofanyika ni kuchukua vidonge vya kisasa vinavyotibu au kupunguza maumivu na kuvichanganya na vumbi la miti hiyo halafu mgonjwa anapewa. Sasa kama mtu atapata nafuu kidogo, anaona ni kweli jamaa ni wataalam.

WATU WAMIMINIKA
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, watu wengi, hususan wanawake, wamekuwa wakimiminika kwenye kliniki mbalimbali zinazotoa tiba mbadala wakiamini watapata nafuu, hasa kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakiteseka kwa miaka mingi bila kupata nafuu mahospitalini.


Quatam Magnetic Analyzer

KIFAA CHALALAMIKIWA

Uchunguzi wa OFM umebaini kuwa kuna kifaa kinaitwa Quatam Magnetic Analyzer, matabibu wengi hawana ujuzi wa kukitumia lakini wanakitumia kuwarubuni watu kuwa kinatoa majibu ya magonjwa ya mwili mzima.


NINI MADHARA YAKE

Gazeti hili liliwasiliana na daktari bingwa mmoja wa (jina kapuni) na kumsimulia kinachotokea kwa tiba mbadala ambapo alisema kama ni kweli, wanaokwenda kutibiwa katika baadhi ya kliniki hizo, wana hatari ya kuyafanya magonjwa yao kuwa sugu au kuambukizwa mengine.

“Dawa za hospitalini zina vipimo vilivyowekwa kwa matumizi ya binadamu na kila dawa ina ujazo wake kulingana na matumizi. Mfano dawa ya kuponya uvimbe, haitakiwi kuwa katika mchanganyiko ambao haujaandikiwa na daktari.
“Unapochanganya na unga wa miti, unaweza kuua nguvu ya dawa na kumfanya mgonjwa kutopata nafuu au kuzua kingine, maana hujui nini kinazaliwa pale ambacho kinaweza kusababisha ugonjwa mpya au hata saratani.”

HUYU HAPA MTOA TIBA

Mtoa tiba mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mloe, akiwa hajui yupo na OFM, alikiri kuwa baadhi ya watoa tiba ni waongo katika kutoa huduma hiyo kwa lengo la kujiingizia mamilioni ya shilingi.

“Haya mambo yapo hapa Bongo. Tunawapa madawa yaleyale ya hospitalini, lakini sisi tukiwa tumeyachakachua na kuyaweka kwenye makopo kisha kuyapachika majina. Tunafanya mchanganyiko huo ili ulete maana halisi ya tiba mbadala.

“Kwa mfano anayeugua kisukari, unampa mchanganyiko utakaompa nafuu, akija mara ya pili unamuonesha dawa nyingine ambayo unamhakikishia itamaliza tatizo lake na unamtajia bei kubwa, anatoa akiamini atapona na sisi tunapata pesa,” alisema tabibu huyo.


TABIBU JJ MWAKA

Hivi karibuni, tabibu wa tiba mbadala, Juma Mwaka Juma ‘JJ Mwaka’ aliingia katika figisufigusi na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto baada ya naibu waziri wa wizara hiyo, Dk. Hamis Kigwangalla kuibuka kwenye kliniki yake, Ilala jijini Dar kwa kufanya ukaguzi.

Katika ziara hiyo ya ghafla, inadaiwa, Mwaka aliingia mitini hivyo kutakiwa kuwasilisha wizarani vibali vinavyomruhusu kutoa huduma agizo ambalo alilifanya na kubainika ana sifa. Kuna taarifa yeye na Tabibu Simon Rusigwa wamebainika kuwa na vyeti halali baada ya kuchunguzwa tiba zao.


TABIBU FADHILI

Huyu naye juzikati aliingia kwenye songombingo la kudaiwa kuchunguzwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba, ana harufu ya kukwepa kodi. Lakini mwenyewe alisema yuko sawa, hadaiwi na TRA wala hana magumashi kwenye huduma yake.

Juzi, saa 8: 14 mchana, Risasi Jumamosi lilimtafuta Dk. Kigwangalla ili kumsikia anasemaje juu ya kuwepo kwa madai hayo. Hata hivyo, simu yake iliita bila kupokelewa.


Source:GPL


Comment & Share this story!!
Utapeli TIBA MBADALA wabainika. Utapeli TIBA MBADALA wabainika. Reviewed by Zero Degree on 1/02/2016 03:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.