Loading...

Wabunge kutoka Chadema na ACT-Wazalendo Lissu, Zitto waibwaga Serikali bungeni.


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (katikati) akiteta jambo na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (kushoto) na wa Ubungo, Saed kubenea kwenye ukumbi wa Bunge jana mjini Dodoma.

Dodoma. Wabunge wa upinzani jana waliibwaga Serikali bungeni baada ya kufanikiwa kuilazimisha iwasilishe Mpango wa Pili wa Maendeleo kama Katiba inavyotaka badala ya Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo uliowasilishwa asubuhi kinyume na sheria.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ndio walioongoza ushindani huo wa kisheria uliomlazimisha mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kukiri kwenye kikao cha jioni kuwa Serikali ilifanya makosa na kukiahirisha.

Baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari, wabunge hao wawili kutoka ACT-Wazalendo na Chadema walisema kutokana na makosa hayo, Rais John Magufuli anatakiwa amwajibishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango.

Katika hoja zao, Lissu na Zitto Kabwe walisema kitendo cha Serikali kuwasilisha mwelekeo wa mpango wa maendeleo ni kinyume na Katiba ya nchi na Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo zinataka shughuli ya kwanza ya Serikali baada ya uchaguzi iwe ni kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ili kwenda na mpango wa utekelezaji.

Sakata hilo lilitokea baada ya Dk Mpango kuwasilisha mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na taarifa ya mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia kuhusu mpango huo.

Pamoja na upinzani kuwa ilishaandaa maoni yake kuhusu mwelekeo huo, msemaji mkuu wa kambi hiyo wa Wizara ya Fedha, David Silinde aligoma kuwasilisha taarifa ya kamati kwa maelezo kuwa kanuni na Katiba zimekiukwa hivyo atawasilisha pale Serikali itakapowasilisha mpango badala ya mwelekeo wa mpango.

“Kwa kuwa Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba imekiukwa pamoja na kanuni ya 94 (1) ya Bunge, kambi ya upinzani haitawasilisha maoni yake kuhusu Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitano mpaka Serikali iwasilishe mpango wake,” alisema Silinde.

Kauli hiyo ilimlazimu Chenge kuahirisha kikao hicho saa 6:25 mchana mpaka saa 10:00 jioni ili kutoa nafasi suala hilo kujadiliwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge ili kubaini kasoro.

Bunge liliporejea jioni, Chenge alikiri kuwa Serikali ilikosea katika mambo mawili ilipowasilisha mpango huo.

Alisema kwanza wabunge walipaswa kukaa kama Kamati ya Mipango kuujadili na pili kama Serikali ilitaka mpango huo ujadiliwe bila ya kupitia kamati, Bunge lilitakiwa litengue kwanza vifungu vya kanuni za uendeshaji wa shughuli zake.

Kutokana na hayo kutofanyika, Chenge alimtaka Dk Mpango kutumia Kanuni ya 58 kuiondoa hoja hiyo ya mwelekeo wa mpango wa maendeleo, jambo ambalo alilifanya na Bunge kuahirishwa.

Ilivyokuwa asubuhi

Baada ya Ghasia, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kumaliza kusoma taarifa ya kamati yake, Zitto aliomba mwongozo na kuhoji utaratibu uliotumika.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mikutano ya Bunge inayofanyika baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, Serikali hutakiwa kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja na kujadiliwa kwa siku tano, kuidhinishwa na kutungiwa sheria ya utekelezaji, jambo alilosema halikufanyika.

“Unatakiwa kuletwa mpango wa Taifa wa kila mwaka na kama ni mwanzo wa Bunge, unaletwa wa miaka mitano. Sasa hatujaletewa mpango wa muda mfupi wala mrefu, wala muswada wa sheria ya utekelezaji wa mpango wa muda mfupi na mrefu,” alisema Zitto.

Zitto alipingana na maelezo yaliyotolewa awali na Chenge juu ya kujadiliwa na kupitishwa kwa mpango huo kwa maelezo kuwa yalilenga uwasilishaji wa mpango wa mwaka mmoja si miaka mitano, na kufafanua kuwa mpango wa mwaka mmoja na mitano hujadiliwa kwa masharti ya ibara ya 63 ya Katiba.

Ibara hiyo inasema “Bunge kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamuhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”.

“Hatujafikia bado kujadili mpango wa mwaka mmoja mmoja, tulichokijadili sasa ni mpango wa miaka mitano ambao itabidi tuutungie sheria halafu ndiyo tuje kwenye utaratibu ambao wewe (Chenge) unaueleza. Maelezo yako yamekiuka kanuni hayafuati taratibu. Waziri hajatuletea mpango ameleta mwelekeo wa mpango,” alisema Zitto. Zitto alimshauri Chenge kukutana na Kamati ya Kanuni kujadili suala hilo ili kulinusuru Bunge kujadili mpango ambao haupo.

Kwa upande wake, Lissu alitumia ratiba ya shughuli za Bunge kuimarisha hoja ya Zitto.

“Orodha ya shughuli za Bunge inaonyesha kwamba Waziri wa Fedha atawasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitano, lakini amekuja kutusomea Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka mitano,” alisema Lissu.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 94 (1), Bunge litakaa kama kamati ya mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba, kuhoji ulipo mpango huo na muswada wa utekelezaji wake.

Alisema kauli ya Chenge kuwa baada ya mjadala wa mpango huo, kamati ya Bajeti ndio itapelekewa mpango sio ya kweli kwa maelezo kuwa kwa mujibu wa kanuni, Kamati ya Bajeti haina jukumu la kujadili mpango wa maendeleo.

Katika majibu yake, Chenge alisema angetolea ufafanuzi miongozo hiyo baadaye na kumtaka Silinde awasilishe taarifa ya upinzani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Lissu alisema hali haikuwa hivyo Bunge lililopita.

“Wanataka kufunika kombe kama alivyokuwa anajaribu kufanya Chenge. Miaka mitano iliyopita tuliletewa Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo 2011/12-15/16 na tukaletewa mpango wa muda mfupi wa mwaka mmoja 2011/ 12, lakini safari hii hawajafanya hivyo,” alisema.

Alisema zimetengwa siku tano za kujadili mpango ambao haupo, jambo litakalowafanya wabunge wapoteze muda wao.

Alisema hayo yanatokea kwa sababu ya Bunge kukubali kupangiwa wajumbe wa kamati zake, jambo ambalo limesababisha kamati kuwa na watu ambao wameshindwa kubaini kasoro hizo.

“Wameshindwa kukumbuka kuwa bungeni unajadiliwa mpango si mwelekeo kwa sababu wengi ni wapya,” alisema mwanasheria huyo mkuu wa Chadema.

Lissu alisema Serikali imejenga hoja ya kutetea kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kusitisha kuonyesha moja kwa moja wa matangazo ya Bunge ili kukwepa aibu za namna hiyo.

Naye Zitto alisema wakati kikao kinaanza walimtahadharisha Chenge, lakini hakutaka kuwasikiliza.

“Ghasia alikuwa akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa mwaka mmoja. Hata kama ungekuwa mpango wenyewe, haiwezekani kujadili mpango wa mwaka mmoja kabla ya mpango wa miaka mitano,” alisema Zitto.

Alisema ni hatari kwa Serikali kuonyesha kasoro kubwa wakati ikiwasilisha mpango wake wa kwanza wa miaka mitano.

Miongozo mingine

Mbali na mwongozo ulioahirisha shughuli za chombo hicho, awali Jesca Kishoa (viti maalum-Chadema), Said Kubenea (Ubungo) na James Ole Millya (Simanjiro) waliomba miongozi mitatu tofauti ambayo Chenge aliikataa, ukiwemo wa kuhoji utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow la kutaka mmiliki wa kampuni ya umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Kubenea alihoji kitendo cha wabunge wanawake wa upinzani kudhalilishwa kwa kuchaniwa nguo zao za ndani na kukatiwa shanga, wakati wakiondolewa bungeni na polisi wanaume juzi katika sakata la kupinga TBC kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.



ZeroDegree.
Wabunge kutoka Chadema na ACT-Wazalendo Lissu, Zitto waibwaga Serikali bungeni. Wabunge kutoka Chadema na ACT-Wazalendo Lissu, Zitto waibwaga Serikali bungeni. Reviewed by Zero Degree on 1/30/2016 02:33:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.