Loading...

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chipu wajisaidia porini.


Sumbawanga. Wanafunzi 1,045 wa Shule ya Msingi Chipu, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa na walimu wao wanajisaidia porini kwa mwaka mmoja baada ya vyoo kufurika vinyesi.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Arord Mkwama, mwishoni mwa wiki iliyopita alisema ametoa taarifa za tatizo hilo katika ofisi ya mkurugenzi kwa muda mrefu.

Mwalimu Mkwamba ambaye pia ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chipu, alisema amekuwa akisubiri fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo vya shule na katika nyumba mbili za walimu.

“Shule hii inakabiliwa na changamoto kadhaa lakini kubwa ni kukosa vyoo, pia walimu wanakabiliwa na changamoto.

“Kati ya nyumba tisa za walimu, mbili hazina vyoo kwa kipindi kirefu sasa na mbili nyingine vyoo vyake vimejaa na havifai kwa matumizi ya binadamu,” alisema Mwalimu Mkwama.

Mkazi wa kijiji hicho, Sunday Kuboja, alisema kwa ushirikiano na wazazi wenzake wamekubaliana kuwa baada ya wiki moja kama Manispaa ya Sumbawanga haitatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo watawakataza watoto wao kwenda shule hadi vitakapojengwa.

“Kadhia ya wanafunzi na walimu wa shule hii ni kukosa pahala pa staha pa kujisaidia. Mwaka 2013 wazazi tulilazimika ‘kutapisha vyoo’ vya shuleni hapo kwa kuwa vilikuwa vimejaa, lakini sasa vimefurika tena na wanafunzi hawawezi kuvitumia kwa sababu vimetapakaa kinyesi sakafuni,” alisema Kuboja.

Mkazi mwingine, Filbeth Ntinda alisema watoto wao wanalazimika kutoroka shuleni na kurudi kujisaidia nyumbani.

Naye Lucia Sawe, alisema kijiji hicho kiko katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.

Wanafunzi Edward Ntalasha na Maria Mbokosi wa darasa la saba, walisema wanafunzi wa shule ya awali wanakanyaga vinyesi na mikojo wanapokwenda kujisadia chooni kwa kuwa hawaelewi lolote kutokana na umri wao kuwa mdogo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Deus Masanja alisema waliwahimiza wananchi kufyatua tofali zaidi ya 35,000 na kuchimba mashimo kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, lakini kikwazo ni saruji, mabati na nondo kwa ajili ya kuanza ujenzi.



Source: Mwananchi
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chipu wajisaidia porini. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chipu wajisaidia porini. Reviewed by Zero Degree on 1/18/2016 06:38:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.