Loading...

Yondani airudisha Yanga kileleni.


Dar es Salaam. Bao la mkwaju wa penalti lililofungwa na beki wa kati, Kelvin Yondani lilitosha kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 36 sawa na Azam iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 na African Sports juzi usiku, lakini mabingwa hao watetezi wakiongoza ligi kwa tofauti ya mabao.

Mabingwa hao watetezi wangeweza kupata bao mapema kabla ya penalti ya Yondani, lakini mkwaju mwingine wa penalti waliyopata awali na kupigwa na Amissi Tambwe uligonga mwamba na kudakwa na kipa wa Ndanda, Jeremia Kisubi.

Ndanda iliingia katika mchezo huo kama wanaotafuta sare, kwani ilikuwa wakipoteza sana mpira na kuruhusu Yanga kucheza, lakini hakukuwa na madhara kwa upande wa mabingwa hao.

Kipindi cha kwanza kilikuwa kama kimepoa kwani Yanga walishindwa kupandisha mashambulizi mengi licha ya Ndanda kushindwa kucheza mchezo wa kushambulia kwa makusudi ya kujilinda.

Kiungo wa Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko nusura aipe timu yake bao la kuongoza dakika ya 31, lakini shuti lake la nje ya eneo la hatari liliparaza nguzo na kutoka nje.

Timu hizo zililazimishana kwenda mapumziko bila bao baada ya winga Saimon Msuva kujiangusha katika eneo la hatari akitaka penalti, lakini mwamuzi alikuwa makini na kumzawadia kadi ya njano kwa tukio hilo.

Yanga walirudi kwa kasi wakitaka ushindi kwa ajili ya kurudi kileleni, juhudi zao zilizaa penalti dakika ya 48, wakati Msuva alipoangushwa katika eneo la hatari.

Akijiamini kwamba angeweza kuipa Yanga bao la kuongoza, Tambwe alishindwa kuamini baada ya mpira wake kugonga mtambaa panya na kurudi uwanjani licha ya kipa wa Ndanda, Kisubi kuanguka upande tofauti.

Mabingwa hao waliendelea kuongeza kasi ya ushambuliaji iliyowalipa dakika ya 59, baada ya kiungo mshambuliaji, Deus Kaseke kuangushwa na Hemed Khoja ndani ya eneo la hatari akiwa anaelekea kufunga.

Msuva alitaka kwenda kupiga penalti hiyo, lakini mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma alimvuta kumrudisha nyuma ili kutoa nafasi kwa Yondani aliyefunga penalti hiyo na kuipa Yanga ushindi.

Vikosi: Yanga. Deo Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Salum Telela, Saimon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Malimi Busungu na Deus Kaseke/Issoufour Boubakar.

Ndanda: Jeremia Kisubi, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Kassian Ponela, Salvatory Ntebe, Jackson Nkwera, William Lucian, Hemed Khoja, Atupele Green, Kiggi Makasi na Braison Raphael.



Niyonzima aomba radhi Yanga

Kiungo Haruna Niyonzima ameomba msamaha kwa uongozi wa Yanga na kuwaahidi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwamba yaliyotokea hadi akasimamishwa kuitumikia klabu hiyo hayatatokea tena.

Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda aliomba msamaha huo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro.

Niyonzima alisema, “Ninauomba msamaha uongozi wa Yanga, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu pamoja na wanachama na mashabiki, ninaipenda timu yangu na ninapenda kuendelea kuitumikia Yanga.”

Alisema kilichotokea ni kutoelewana kimawasiliano na ofisi ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha kiasi cha kulifikisha suala hilo kwenye hatua hiyo.

Kwa upande wake, Muro alisema suala la Niyonzima limefika katika uongozi mkuu wa klabu, linashughulikiwa na lipo katika hatua nzuri.

Yanga ilitangaza kuvunja mkataba na Niyonzima baada ya nyota huyo kuchelewa kurejea nchini na kujiunga na wenzake baada kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Ethiopia mwezi Novemba mwaka jana.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wazee wa Yanga wamepinga kitendo cha uongozi wa Yanga kutaka kumsamehe kiungo huyo raia wa Rwanda kwa kile walichoeleza kuwa amejaa na dharau.

Akizungumza Makao makuu ya klabu hiyo jana, Hashimu Mhika alisema kitendo cha uongozi kutaka kumrejesha Niyonzima kimeleta mpasuko ndani ya Yanga na kwa sasa wanachama wamegawanyika na wao kama wazee hawajaridhia kiungo huyo kurudi kuichezea tena Yanga.



Source: Mwananchi
Yondani airudisha Yanga kileleni. Yondani airudisha Yanga kileleni. Reviewed by Zero Degree on 1/18/2016 06:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.