Waziri wa mambo ya ndani asema, Kamatakamata hailengi Wakenya.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema operesheni inayoendelea ya kukamata wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume na sheria, haiwalengi raia wa Kenya kama inavyodhaniwa.
Agizo la kuwaondoa raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria lilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipotembelea makao makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Waziri Masauni alisema kumekuwapo na ongezeko la wageni nchini wanaoishi kwa vibali vya kufanya kazi za kitaalamu au wawekezaji, lakini wanafanya biashara zisizo na tija na wengine kufanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya na hivyo kuagiza waanze kusakwa na kurejeshwa kwao.
Utekelezaji wa agizo hilo ulichukuliwa kuwa unawalenga raia wa Kenya, ambayo ina vitega uchumi vingi na ambayo raia wake wana muingiliano mkubwa na Watanzania.
Lakini Waziri Kitwanga alisema fikra hizo ni tofauti na nia ya Serikali na kwamba operesheni hiyo itakuwa endelevu.
Alisema mpaka kufikia Ijumaa ya wiki iliyopita, raia 409 wa kigeni walikuwa wamekamatwa, na wengi ni kutoka nchi za India na China.
“Tunataka raia wa kigeni anayeingia nchini afuate utaratibu,” alisema Waziri huyo.
“Wapo wanaosema kuwa tunawalenga zaidi Wakenya, lakini kati ya raia hao 409 waliokamatwa, Wakenya ni wanane tu.”
Alisema raia kutoka Kenya wanaoishi nchini ni zaidi ya 6,000 na wote wana vibali, isipokuwa hao wanane ambao pia walibainika kujihusisha na uhalifu.
“Nchi za Afrika Mashariki zina makubaliano maalum ndiyo maana hakuna usumbufu kwa raia wa nchi za ukanda huo zaidi ya hao Wakenya tu,” alisema.
Mwaka jana kulikuwa na matukio kadhaa yaliyohusishwa na harakati za kigaidi. Vituo viwili vya polisi vya Mkuranga na Sitakishari vilivamiwa na watu waliopora silaha, wakati watu takriban 10 walikamatwa mkoani Morogoro wakiwa na vifaa ambavyo polisi walisema hutumiwa na watu hao.
Pia polisi walihitaji msaada wa askari wa Jeshi la Wananchi kupambana na vijana waliokuwa kwenye mapango ya Amboni Tanga, huku vituo watoto kadhaa wakibainika kufundishwa mafunzo ya kigaidi kwenye nyumba za mkoani Kilimanjaro.
Waziri Kitwanga alisema katika kuhakikisha mipaka na bandari inalindwa ipasavyo, wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wapo katika majadiliano ya kuanza kuweka polisi kulinda bandari, badala ya kampuni binafsi.
“Tunajadili idadi ya askari tutakaowatumia, tutawaweka sehemu gani, pia iwapo wavae sare au wawe kiraia,” alisema.
“Watanzania watambue kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anaishi kwa usalama na utulivu. Kila Mtanzania anaweza kutafuta haki yake lakini akumbuke kuwa upande mwingine kuna wajibu anaotakiwa kuufanya. Haki na wajibu viende sambamba.”
Kuvamiwa vituo vya polisi
Waziri Kitwanga pia alizungumzia tishio la vitendo vya ugaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, akisema matukio ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi, yana harufu ya ugaidi.
“Ugaidi haujakomaa Tanzania, na magaidi hawajawa na nguvu. Wanachofanya ni kuvamia kituo cha polisi, kuchukua silaha na kuzitumia kufanya uhalifu kupata fedha ili kuendesha maisha yao. Kuna dalili kubwa kwamba huu ni ugaidi,” alisema.
Alisema licha ya Serikali kuwakamata, wapo wanaoendelea kuingia nchini na ili kumaliza suala hilo ni lazima uwekwe mpango wa muda mrefu.
“Kwa sasa tunaendelea kujadiliana kuhusu mpango wa kutambua raia wetu na wanafunzi katika shule mbalimbali. Lazima tujue wangapi wameacha shule na wamekwenda wapi. Ugaidi ukikomaa katika nchi unakuwa tatizo kubwa,” alisema.
“Magaidi hawatengenezwi nchini, wanatoka hapa wanakwenda Somalia wanafundishwa na kisha wanarudi kufanya ugaidi. Lazima tutambue raia waliotoka Tanzania walikwenda nchi gani na kwa sababu gani. Bado tunajadiliana tuone tutaliendesha vipi jambo hili.”
Kitwanga alisema ili polisi iweze kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima iwe na mfumo imara kuanzia makao makuu hadi ngazi ya chini ya ulinzi shirikishi.
Alisema moja ya changamoto alizokumbana nazo baada ya kuteuliwa kuwa waziri ni dosari katika mfumo wa utendaji kazi.
Alisema nchi ina polisi 45,000 na kati yao wanaoishi kambini ni 10,000 tu na kwamba kuishi uraiani kunashusha nidhamu.
“Hii ni changamoto kwa sababu ukitaka kuwakusanya wote hutaweza maana wengi wanaishi uraiani. Kwa viwango vya kimataifa, askari mmoja anapaswa kulinda watu 350. Kwa Afrika askari mmoja analinda kati ya watu 500 hadi 700 lakini kwa Tanzania analinda watu 1,000 hadi 1,200,” alisema.
Source:Mwananchi
Waziri wa mambo ya ndani asema, Kamatakamata hailengi Wakenya.
Reviewed by Zero Degree
on
1/18/2016 10:52:00 AM
Rating: