Loading...

WINGU ZITO lazidi kutanda Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na waandishi
Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na waandishi wa habari . 

Zanzibar. Wingu zito linaendelea kutanda kwenye anga za siasa visiwani hapa baada ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kusema mchakato wa kupanga bajeti kwa ajili ya marudio ya uchaguzi umekamilika, huku CUF ikishangazwa na kupinga tamko hilo.

Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na katibu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad wako kwenye mazungumzo ya kujadili kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais, wawakilishi na madiwani na hadi sasa hawajatoa tamko la maendeleo ya mazungumzo yao.

Lakini viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa taarifa za kuwataka wafuasi wao wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, huku CUf ikisema inachosubiri ni kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi wa Rais na haiku tayari kurudia uchaguzi.

Kauli nyingine ya namna hiyo ilitolewa jana na juzi na Balozi Seif alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema kwa kuwa matokeo ya uchaguzi yalifutwa basi ni wazi kuwa hakuna utaratibu ambao utakaofanyika wa kuyamaliza matokeo yaliobaki isipokuwa kurudia uchaguzi upya.

“Tuache kusikiliza maneno ya porojo bali nawaambia suala la kurudia uchaguzi lipo kama kawaida na kilichobaki sasa ni kusubiri amri ya Tume (ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)) kutangaza siku ya uchaguzi huo,” alisema Balozi.

“Kwa upande wetu CCM tupo tayari kushiriki uchaguzi huo. Hata kama CUF hawatashiriki, sisi hawatubabaishi.”

Kwa upande wa mazungumzo yanayofanyika Ikulu kwa kuwashirikisha viongozi wa wakuu wa Serikali, Balozi alisema kuwa hajui nini kinaendelea hadi sasa, lakini akawataka wananchi wasubiri taarifa rasmi mazungumzo hayo yatakapomalizika.

“Kikubwa zaidi nilichokisikia mimi katika mazungumzo hayo ni suala la kudumisha amani na utulivu ila kwa upana zaidi tusubiri mazungumzo hayo yatakapomalizika taarifa itatolewa kwa wananchi wote,” alisema.

Lakini kwa mara nyingine, CUF walipinga vikali kauli hiyo wakisema hawako tayari kurudia uchaguzi.

Kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Ismail Jussa alisema matamko hayo yanashangaza wakati bado mazungumzo yanaendelea.

Jussa alidai kuwa kuna timu imejifungia mahali inafanya hujuma na inampotosha Dk Shein.

Kuhusu sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif alisema kutoshiriki kwa viongozi wa CUF hakutaathiri sherehe hizo.

Alisema kamati ya maadalizi ya sherehe na mapambo tayari imeshajipanga vya kutosha na kilichobaki ni ufanikishaji wa maadhimisho hayo ambayo shamrashamra zake zilitarajiwa kuanza jana.

Alisema madhimisho hayo yapo kama kawaida na mwaka huu wamepanga siku ya kwanza ya shamrashamra zake kuitumia kufanya usafi wa mazingira ya mji wa Zanzibar.

Alisema kuwa shamrashamra nyingine za maadhimisho hayo zitaendelea kama kawaida kwa kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.


Source: Mwananchi

Comment & Share this story!!
WINGU ZITO lazidi kutanda Zanzibar. WINGU ZITO lazidi kutanda Zanzibar. Reviewed by Zero Degree on 1/03/2016 12:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.