Kocha Guardiola atua Manchester City.
Manchester, England. Kocha Pep Guardiola amekubali kusaini mkataba wa miaka mitatu wa kuifundisha Manchester City kuanzia msimu ujao.
Kocha huyo mwenye miaka 45, kwa sasa anaendelea kukinoa kikosi cha Bayern Munich na atachukua nafasi ya Manuel Pellegrini, ambaye ataondoka City Juni 30.
Taarifa ya klabu ya City ilisema kocha wa kimataifa wa Chile, Pellegrini, ambaye sasa ana miaka 62, ametoa ushirikiano katika suala hilo akiridhia kumpisha Guardiola.
Klabu hiyo ya jijini Manchester ilisema makubaliano yao na kocha huyo wa zamani wa Barcelona, Guardiola yaliyoanza tangu 2012 yalifikia muafaka jana mchana.
Roberto Mancini alikuwa kocha wa City wakati mazungumzo ya kutaka kumchukua Guardiola yakianza, ambaye pia aliwapa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka huo.
Pellegrini alichukua nafasi ya kocha huyo wa Italia, Mancini 2013 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la Ligi mara mbili msimu uliofuata.
Ameshinda mechi 64 kati ya 99 za Ligi Kuu akiwa kocha wa timu hiyo hadi jana, rekodi ambayo inazidiwa na Jose Mourinho pekee, ambaye ameshinda mechi 73 kati ya 99 za ligi hiyo akiwa kocha wa Chelsea. City imetwaa mataji manne ikiwa chini ya Pellegrini.
Kwa sasa City wapo katika hatua ya fainali ya mashindano ya Kombe la Ligi, wakiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu inayoendelea leo, wakati Leicester City ikiongoza.
Miamba hiyo ya Manchester pia imeshavuka katika hatua ya tano ya Kombe la FA na itacheza na Chelsea, pia ikiendelea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya timu 16 bora.
ZeroDegree.
Kocha Guardiola atua Manchester City.
Reviewed by Zero Degree
on
2/02/2016 05:06:00 PM
Rating: