Maktaba inayoelea majini yatinga jijini Dar.
Maktaba hiyo inayoelea.
Wapo wanaoiita maktaba inayoelea. Maktaba hiyo ni pekee iliyowahi kuwafikia watu zaidi ya 44 milioni duniani tangu ilipoanza kuelea baharini miaka 40 iliyopita.
Hii ni meli kubwa ya kuuzia vitabu yenye jina la MV Logos Hope, ambayo kwa mara ya kwanza imetia nanga kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Ujio wake umekuwa gumzo miongoni mwa wengi hasa wapenda vitabu. Meli hii imegeuka kuwa kivutio cha kitalii na siyo maktaba tena japo lengo lake ni kusaidia katika kuhamasisha usomaji wa vitabu ili kuongeza ujuzi na maarifa mapya.
Huenda ikabadili utamaduni wa wasiopenda kusoma vitabu kuanza kupenda.
Mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne, Shule ya Seminari ya Kidugala, mkoani Njombe mwaka jana, Goodluck Frank anasema ujio wa MV Logos Hope utaongeza ari ya usomaji wa vitabu hasa kwa wasio na utamaduni wa kufanya hivyo.
“Sijawahi kutembelea maktaba ya kawaida kwa sababu vitabu huuzwa hata barabarani, lakini nashangaa tangu meli hii itie nanga jijini Dar es Salaam nimejikuta nikipata hamu ya kuanza kupenda kwenda maktaba. Kumbe vipo vitabu ambavyo siwezi kukutana navyo barabarani,” anasema Goodluck.
Anasema amefanikiwa kununua vitabu vitatu vya masomo ya sayansi vya kidato cha tano kwa bei ya Sh5,000 wakati bei yake halisi ya kitabu kimoja kwenye duka la vitabu ni kuanzia Sh35,000.
Kapteni wa meli hiyo, Dirk Colenbrander anasema kwa Afrika, Tanzania ni nchi ya kwanza kuwahi kutembelewa na kwamba maktaba hiyo inayoelea ina vitabu vya aina tofauti zaidi ya 5,000.
“Vipo vitabu vya michezo, uchumi, afya, mapishi, lugha, dini, sayansi, tamthilia, kamusi, atlasi na vingine vingi. Kila aina ya kitabu wapo wataalamu wanaohusika na wamekuwa wakiwasaidia wageni wanaotutembelea kulingana na mahitaji yao,” anasema Kapteni Colenbrander.
Veronica Mabena, mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam anasema amefanikiwa kununua vitabu vya mapishi ambavyo anaamini vitamwezesha kuboresha biashara yake ya mamalishe.
“Nilikuja kununua vitabu kwa ajili ya watoto wangu lakini nilipoona vipo vya mapishi imenibidi nibadilishe lengo baada ya kuhamasika, naamini nikisoma nitapata elimu itakayonisaidia kuboresha huduma yangu ya chakula,” anasema.
Meli hiyo inavyo vitabu vya fani mbalimbali vinavyokidhi mahitaji ya rika na viwango vyote vya elimu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Patrick Myovela anasema ubunifu wa wamiliki wa meli hiyo unapaswa kuigwa kwani unasaidia kuongeza ari ya kupenda kusoma vitabu.
“Kuna wengine ukitaka kumficha kitu weka kwenye mfumo wa maandishi, wengi wanaamini anayepaswa kusoma ni yule aliye shuleni kumbe kusoma ni kuongeza maarifa haijalishi upo wapi,” anasema. Myovela anasema uvivu wa kusoma unaifanya idadi ya watu wanaotembelea meli hiyo kuwa kidogo tofauti na matarajio yake.
Anasema anasema kusoma vitabu ni utamaduni na ni burudani kama burudani nyingine.
“Ukisoma kitabu utacheka peke yako, utasikitika, utalia na wakati mwingine utatabasamu na kujiona haupo peke yako. Utafarijika na kupata maarifa mapya,” anasema.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Jackson Benard anasema aliposikia ujio wa meli hiyo aliamua kufunga safari ili ajifunze kulikoni, maktaba iwekwe ndani ya meli?
“Nimenunua vitabu vitano vya masuala ya sayansi ya kilimo, vitabu hivi ni vizuri na nimevinunua kwa bei nzuri ukilinganisha na bei ya vitabu kwa soko la hapa nchini, kwa kweli nashauri wale wanaopenda kusoma, waitembelee meli hii kujipatia vitabu vya kuongeza ufahamu wao,” anasema Benard.
Kapteni Colenbrander anasema idadi ya watu wanaotembelea meli hiyo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku tangu iwasili jijini Dar es Salaam.
Serikali ya yalonga
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako anasema ujio wa meli hiyo utumike kama somo kwa watanzania.
Anasema mkakati wa kupambana na umaskini nchini, utawezekana ikiwa Watanzania watajenga tabia ya kupenda kusoma vitabu.
Anawataka watunzi, wachapishaji, wasambazaji na wafanyabishara wa vitabu kuwa wabunifu ili kuhamasisha jamii ijenge tabia ya kupenda kusoma.
Anasema maarifa na utaalamu mwingi umejificha kwenye vitabu na kwamba ili kuupata ni lazima Watanzania wakubali kutenga muda wao kwa ajili ya kuvisoma na siyo vinginevyo.
“Kuna wakati umaskini huwa unasababishwa na kutojua njia za kupambana nao, ni vyema tujifunze kupitia ujio wa meli hii kwamba elimu inayopatikana kwenye vitabu ni kubwa na inaweza kusaidia katika harakati za mapambano ya umaskini,” anasema.
Anatumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania hasa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani kuitembelea Mv Logos ili wapate fursa ya kusoma na kununua vitabu.
“Ni wakati wenu mnaojihusisha na vitabu kutumia fursa hii kujifunza namna ya kusambaza tamaduni za Kitanzania kwenye nchi nyingine kupitia meli hii,” anasema.
Kwa upande wake mkurugenzi wa meli hiyo, Seelan Govender anasema maisha ya mwanadamu yanaweza kubadilika kutokana na mafunzo yanayopatikana ndani ya vitabu mbalimbali vya kiada na ziada.
Ndani ya meli
Kapteni Colenbrander anasema pamoja na vitabu ndani ya meli hiyo kuna mgahawa na vinapatikana vyakula tofauti vya asili kutoka mataifa mbalimbali duniani ili kuvutia watu waitembelee na kukutana na vitabu.
“Kuna burudani mbalimbali kama vile, muziki, ngoma, bendi, pamoja na kuzungumza na wafanyakazi zaidi ya 400 wa meli hiyo wanaotoka mataifa zaidi ya 40, duniani kote,” anasema.
Anaeleza kuwa wafanyakazi hao wamekuwa wakionyesha mitindo tofauti ya kiasili kutoka zaidi ya mataifa 40, jambo linawafanya wengi kupenda kuitembelea.
Anasema ikiwa mtu atatembela meli hiyo kwa ajili ya burudani, atakutana na vitabu ambavyo akitupia macho atatamani kusoma, hivyo kuamua kununua.
Maisha ya wafanyakazi
Maajabu ni kwamba wafanyakazi wa meli hiyo wanajitolea kufanya kazi hiyo. Wanaishi kama ndugu huku kila mmoja akiona mwingine ni wa thamani kwake.
“Wafanyakazi wote wanachukulia hii kuwa ni huduma, wanaishi na kufanya kazi ya kuwahudumia watu duniani kote,” anasema Kepteni Colenbrander.
Wao wanaona kazi hiyo ni huduma kama zilivyo huduma nyingine hivyo hawahitaji kulipwa mishahara ila kuwaongezea watu ujuzi na maarifa kupitia vitabu.
MV Logos Hope
Meli hiyo inaendeshwa na taasisi ya msaada iliyoanzishwa nchini Ujerumani tangu mwaka 1970, mpaka sasa imefanikiwa kuzifikia nchi 150 kwa ajili ya kuuza vitabu.
Vitabu vyake vinakuswanywa kutoka nchi tofauti na waandishi tofauti.
Kepteni Colenbrander anasema baada ya kuondoka Dar es Salaam, MV Logos Hope inatarajiwa kuelekea mjini Maputo, Msumbiji na baadaye Durban, Afrika Kusini.
Meli hiyo inamilikiwa na shirika lisilo la kiserikali la Kijerumani la ‘Gute Bucher fur Aller’ GBA lenye maana “Vitabu Vizuri kwa Wote.”
ZeroDegree.
Maktaba inayoelea majini yatinga jijini Dar.
Reviewed by Zero Degree
on
2/01/2016 05:47:00 PM
Rating: