Loading...

Kasoro 9 zilizotibua uundwa wa Katiba Mpya.

Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,Dk Ali Mohamed Shein wakiwa wamenyanyua katiba iliyopendekezwa baada ya kukabidhiwa mwanzoni mwa Agosti,2014 mjini Dodoma.

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akitafakari jinsi ya kumalizia mchakato wa Katiba Mpya, kuna kasoro kumi na moja zilikwamisha kuandika mkataba huo mpya baina ya Serikali na wananchi, kwa mujibu wa uchambuzi wa Mwananchi.

Mchakato huo, uliokumbwa na upinzani kutoka vyama vya siasa na wadau wengine, ulikwama wakati ukiwa umefikia hatua ya kupiga Kura ya Maoni kuridhia mabadiliko ya Rasimu ya Katiba yaliyochekechwa na Bunge la Katiba.

Akipokea Ripoti ya Uchaguzi Mkuu mwezi uliopita, Rais Magufuli alisema: “Serikali itashirikiana na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kuhakikisha kuwa mchakato wake (Katiba) unaendelea kama ulivyokusudiwa ili kuipeleka Tanzania mahali pazuri.”

Aidha, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema baada ya kukamilisha mpango wa kubadili uongozi kama ilivyo kawaida, “Tume ipo tayari kuendelea pale ilipoishia”.

“Sasa tunaangalia Sheria ya Kura ya Maoni ambayo kwa maeneo mengi imepitwa na wakati. Mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na kufikishwa bungeni halafu NEC na ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) zitaendelea na mchakato wa Kura ya Maoni,” alisema Lubuva.

Kwa kufuatilia mchakato mzima, Mwananchi imebaini kasoro 21 ambazo zilikuwa zinalalamikiwa katika kila hatua ya mchakato hadi ulipokwama kutokana na kutokamilika kwa kazi ya uandikishaji wapigakura.

Dosari katika uteuzi wa wajumbe

Mchakato huo ulianzia mguu mbaya baada ya Kikwete kujaza wanasiasa kwenye Bunge la Katiba. Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi walikuwa miongoni mwa wajumbe 629 wa Bunge hilo, jambo lililofanya wadau walalamikie kuwa mchakato huo unaweza kutofanikiwa.

Bunge la Muungano lilikuwa na wabunge 356, wakati Baraza la Wawakilishi lilikuwa na wajumbe 88.

“Wanasiasa wameuweka rehani mchakato wa kupata Katiba Mpya,” alisema rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria (TLS), Felix Kibodya alizungumza na Mwananchi Agosti 7, 2014.

“Kosa la kwanza tulilofanya ni kuruhusu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi kuwa wajumbe.

“Mwakani ni uchaguzi na ukiangalia wajumbe wengi wanalenga uchaguzi. Hata ukiangalia mchakato wenyewe, utaona haujahusisha zaidi wanasheria kama ilivyokuwa kwa wenzetu wa Kenya.”

Kutokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano kutawaliwa na wajumbe wengi wa CCM, vyama vya upinzani vilikituhumu chama hicho tawala kuwa kilikuwa kinaingiza ajenda yake na hasa baada ya habari kuvuja kuwa chama hicho tawala kilisambaza waraka uliowataka watu wake kuhakikisha muundo wa Muungano unaendelea kuwa wa serikali mbili.

Jambo hilo ndilo lililogeuza Bunge la Katiba kuwa uwanja wa siasa hadi wajumbe kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) viliposusia vikao wakati mjadala ukiwa sehemu ya kwanza.

Kikwete kujibu ripoti ya Tume

Wakati Bunge la Katiba linajiandaa kuanza vikao vyake, dosari ya pili ikajitokeza baada ya kubadili kanuni za awali zilizotaka Rais azindue chombo hicho kwanza na baadaye mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe ripoti. Wajumbe walikubaliana Jaji Warioba awasilishe kwanza ripoti yake, ndipo Rais ahutubie, kitu kilichopingwa bila mafanikio na wajumbe kutoka vyama vya upinzani.

Kikwete akatumia nafasi hiyo kuzungumzia ripoti hiyo, huku akionya kuhusu muundo wa Muungano wa serikali tatu, kitu kilichoweka msingi kwa wajumbe kutoka CCM kujenga hoja za kutoachana na mfumo huo uliodumu kwa miaka zaidi ya 50.

“Tulitarajia Rais angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza kama mwenyekiti wa CCM na ameweka msimamo juu ya muundo wa Muungano,” alisema katibu wa muda wa Ukawa wa wakati huo, Julius Mtatiro baada ya Kikwete kuhutubia.

Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Mustapha Akoonay alisema wakati huo kuwa uwezekano wa kupatikana Katiba Mpya ulikuwa shakani kwa kuwa upinzani kwenye muundo utakuwa mkubwa zaidi.

“Kwa sasa itabidi kurudi kwa wananchi kupiga kura ya maoni kuhusu muundo wa Muungano,” alisema Akoonay alipozungumza na Mwananchi wakati huo.

Tume ya Warioba kuzuiwa

Wakati Tume ya Katiba ikitegemewa kuwa mshauri kwenye vikao vya Bunge hilo, wajumbe walipiga kura kuwazuia wajumbe wa Tume ya Warioba kuendelea kuwa na wajibu baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni.

CCM kuongoza wajumbe wake

Wakati Bunge la Katiba likitarajiwa kuwa la wajumbe wenye misimamo binafsi kutokana na maeneo waliyotoka, uzoefu na elimu yao, CCM iliitisha kikao cha Halmashauri Kuu na kuweka msimamo baada ya kuchambua Rasimu ya Katiba, hasa kwenye suala la muundo wa Muungano.

Wajumbe wengine, hasa kutoka vyama vya upinzani walipinga waraka huo wakisema utaharibu mwenendo wa Bunge. Suala hilo lilifanya Bunge litumie muda mwingi kujadiliana kuhusu upigaji kura, wajumbe wanaoonekana kutoka CCM wakisisitiza kura iwe ya wazi, wakati wapinzani wakisisitiza iwe ya siri.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari baada ya kikao cha Ukawa wakati huo kuwa wanataka kura ya siri kwa kuwa ndiyo itakayowafanya wajumbe wapige kura bila ya kuingiliwa.

Bunge kutozingatia maridhiano

Mwongozo wa CCM kutaka wajumbe kutoka chama hicho kufanya kama walivyoagiza, ulizua dosari nyingine; uamuzi kufanywa bila ya kujali maoni ya wachache kutokana na CCM kutumia kikamilifu wingi wao kwenye chombo hicho.

Baada ya Ukawa kususia, hakuna jitihada zilizofanyika kuwarejesha pamoja na kwamba Katiba ilihitaji maridhiano ya pande zote, suala la maadili likaondolewa kwenye tunu za Taifa, kanuni zikabadilishwa kulingana na utashi wao na hata Rasimu ikafanyiwa marekebisho, hali iliyoweka mazingira ya wajumbe wasiokubaliana na mwenendo huo, kususia vikao.

“Kwanza, kilichotokea wajumbe walisahau kufanya kama ilivyokuwa kwenye Tume. Sisi tuliweka pembeni itikadi za vyama na kuweka mbele utaifa, lakini Dodoma watu walianza siasa na kuanza kushindana,” alisema Jaji Warioba wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha ITV Mei 6, 2014.

“CCM imeamua kupitisha yao na wengine wanatafuta njia ya kuzuia wasipate uwingi wa kura na kuna uwezekano bila ya maridhiano tutapata matatizo katika mchakato. Lazima kuwe na maridhiano.”

Sitta akusanya maoni mengine

Wakati vikao vikiendelea huku wajumbe kutoka vyama vya upinzani wakizidi kukosoa kuwa CCM imeteka mchakato na kuingiza ajenda zake, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta alianza mchakato wake wa kukusanya maoni kutoka vikundi vilivyokuwa vikienda mjini Dodoma.

Kwa kuwa Tume ya Warioba iliwasilisha ripoti iliyotaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu, suala la serikali za mitaa liliachwa chini ya serikali za Tanganyika na Zanzibar.

Lakini Sitta alikusanya upya maoni ili Serikali za Mitaa zirejeshwe kwenye Serikali ya Muungano ambayo kwa Tanzania Bara inashughulikia pia masuala yasiyokuwa ya Muungano. Suala hili liliwapa nguvu wapinzani kuwa Rasimu ya Katiba ilikuwa inazidi kuchakachuliwa.

Serikali kuchukua mamlaka ya NEC

Dosari nyingine iliyoonekana mwishoni mwa mchakato huo ni Serikali kuchukua mamlaka ya NEC ya kutangaza tarehe ya kupiga Kura ya Maoni, jambo lililozidisha imani ya wapinzani kuwa NEC iliporwa mamlaka yake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, mwenyekiti wa NEC kwa kushirikiana na wa ZEC ndiyo wanaopewa mamlaka ya kutangaza tarehe na kusimamia mchakato wa kupiga kura.

Lakini aliyetangaza tarehe kwa mara ya kwanza ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyesema itafanyika Machi 30, 2015 lakini siku chache baadaye Kikwete akiwa ziarani China alithibitisha tarehe hiyo.

Suala hilo lilimziba mdomo Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva aliyekataa kutoa ufafanuzi wa chombo gani hasa kinatakiwa kitangaze.

Kubadilisha msimamo wa pamoja

Licha ya kuwa nje ya Bunge la Katiba, wajumbe kutoka vyama vya upinzani bado walikuwa na matumaini kuwa hali ingetengemaa na uamuzi wa Rais kukutana na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambacho kinahusisha vyama vya siasa, uliimarisha imani hiyo.
Katika kikao hicho walikubaliana mambo kadhaa yakiwamo ya kuahirishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya hadi baada ya Uchaguzi Mkuu na badala yake iboreshwe Katiba iliyopo ili uchaguzi ufanyike kwa uhuru na utulivu.

Wapinzani walifurahia makubaliano hayo, lakini Serikali haikutekeleza. Badala yake mchakato uliendelea hadi Katiba Inayopendekezwa ikapitishwa na wajumbe wengi wa CCM.

Oktoba 8, 2014 wakati Kikwete alipokabidhiwa Katiba Inayopendekezwa, alitoa hadithi ya jini lililookolewa kutoka kwenye chupa na likataka kummeza kijana aliyelitoa nje ya chupa.

Hadithi hiyo iliwalenga wapinzani ambao mapendekezo yao yangemeza mchakato pale ulipokuwa umefikiwa.

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha EATV, Nape Nnauye ambaye alikuwa msemaji wa CCM wakati huo, alisema chama hicho kitaendelea kuheshimu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012, sura ya 83 inayoelekeza Kura za Maoni ipigwe ndani ya siku 84 baada ya Bunge kuvunjwa, hali iliyoondoa uwezekano wa Kura ya Maoni kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi.

Serikali kutojipanga

Wakati Bunge la Katiba likiamini kuwa kazi ya kuandika Katiba Mpya imeshakamilika na kusubiri upigaji kura, Serikali haikuwa tayari.

Mabilioni ya fedha yalishatumiwa na Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na bado yalihitajika mengine kununulia vifaa vya kuandikisha wapigakura, kugharimia uandikishaji wapigakura na kugharimia Kura ya Maoni; Serikali ilikuwa kwenye mtihani.

Uandikishaji wapigakura ukawa unasuasua kutokana na uchache wa vifaa vya kielektroniki na haikuwa ajabu ilipotangazwa kuwa kazi hiyo ya kupiga kura ya maoni imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena ili kupisha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, vyote vikihitaji mabiliano ya fedha.

Katika kikao cha pamoja cha viongozi wa Ukawa na waandishi wa habari, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alihoji uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika ndani ya muda uliopangwa, yaani Aprili 30, 2015 wakati kazi ya uandikishaji ilikuwa inaenda mrama.

“Pamoja na kutangaza siku ya kupiga kura, bado uandikishaji katika Daftari la Wapigakura haujaanza kwa sababu wanasubiri vifaa,” alisema Profesa Lipumba.

“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration (BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7,500. Tume inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika kweli?”

Wakati akikabidhi Ripoti ya Uchaguzi Mkuu, Jaji Lubuva alipendekeza kufanyike marekebisho kadhaa ya kisheria kabla ya kuendelea na hatua zilizobaki. Alitaja vipengele vya kuzingatia wakati wa kuhuisha Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013 kuwa ni tarehe ya Kura ya Maoni, muda wa kampeni kwa ajili ya kura hiyo na uundwaji wa kamati za Kura ya Maoni.

Mapendekezo hayo yanamaanisha kuwa mchakato uendelee pale ulipoishia, lakini wanasheria na wadau wengine wanapingana na maoni hayo.

Akizungumzia kauli ya Rais ya kufufua mchakato wa Katiba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Bunge la Katiba halikufikia muafaka kutokana na Ukawa kujitoa.

Dk Kijo-Bisimba alisema ili kuondoa sintofahamu iliyokuwapo, unahitajika mjadala wa kitaifa ambao utaruhusu kukubaliana kwenye masuala kadhaa, kabla wataalamu wa sheria hawajamalizia na kupata katiba inayohitajika.

Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile alisema endapo rasimu iliyotolewa na Jaji Warioba haitorejeshwa kwa majadiliano kabla ya maridhiano, “Watanzania tutakuwa kama tumedhulumiwa. Ilikuwa na hoja nyingi nzuri kwa watu tofauti”.

Mwambipile alibainisha hofu yake kuwa ni uwezekano wa kuja kuwa na malumbano na mijadala mirefu wakati wa uundaji wa sheria ambazo zinategemea katiba ya nchi. Kwa maoni yake, Katiba Inayoendekezwa iliyokabidhiwa kwa marais Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein mwishoni mwa mwaka jana, “inatoa haki hapa na kunyang’anya pale”.

Mwanasheria huyo alifafanua kuwa kwa uamuzi wa Serikali kwamba mwendelezo wa mpango huo utaanzia kwenye Sheria ya Kura ya Maoni ni sawa.

“Lakini watendaji wanatakiwa kuona namna ya kutafuta muafaka baina ya pande zenye mtazamo tofauti kabla ya hatua hizo za mwisho kukamilishwa,” alisema.

Mkurugenza mwenza wa kampuni ya uwakili ya Appex, Frank Mwalongo alisema kwa kuwa BMK lilipoteza uelekeo baada ya kuwa na wanasiasa wengi waliozua malumbano yasiyo na msingi wakati wa kuijadili Rasimu ya Katiba, analo la ziada; Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iangaliwe ili kuruhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iendelee kuwapo.

“Utata wowote uliojitokeza bungeni unapaswa kufafanuliwa na wataalamu hawa wa Tume ya Warioba,” alisema Mwalongo.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura alisema: “Rasimu ya Warioba ndiyo tuliyoitolea maoni. Kutoitumia ni kuweka pembeni mapendekezo ya wengi.”

Jaji Warioba alipopigiwa simu ili kupata maoni yake, alisema atatoa neno pale mchakato huo utakapoanza.

Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Warioba na mtetezi mkubwa wa Rasimu ya Katiba ambaye kwa sasa ni mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole alikubaliana na msimamo wa Warioba.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa tathimini jumla ya taasisi hiyo imebaini kwamba mchakato umeshidwa kujenga muafaka wa kitaifa unaohitajika, hivyo kusababisha Katiba Inayopendfekezwa kuwa na kiwango duni cha maridhiano ya kitaifa.

“Zaidi ya kugusiwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Bunge mwishoni mwa mwaka 2015, haijaonekana nia wala dalili za Serikali kutaka kurejesha mchakato wa Katiba Mpya,” alisema Kibamba.

“Ndiyo maana Jukata tunaungana na Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika hoja kuwa mjadala wa kitaifa unahitajika sasa. Bila Katiba Mpya yenye misingi imara ya utawala bora. Utumbuaji majipu na ‘Hapa Kazi Tu’ zinaweza kuwa kaulimbiu zisizoeleweka kwa Watanzania.”


Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Kasoro 9 zilizotibua uundwa wa Katiba Mpya. Kasoro 9 zilizotibua uundwa wa Katiba Mpya. Reviewed by Zero Degree on 7/11/2016 05:09:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.