Loading...

Polisi wampania muuaji wa askari mwenzao.

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema halitasita kumchukulia hatua yeyote aliyehusika na mauaji ya Sajini Mensah Ponoi bishe, hata kama aliyetekeleza mauaji hayo yupo ndani ya jeshi hilo.


Sajini Mensah aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika Julai 22, mwaka huu, saa 2:00 usiku, akiwa eneo la kazi katika mataa ya kuongozea magari ya Sayansi Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili wa askari huyo jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro, alitoa agizo kwa askari kuhakikisha wanampata mhalifu aliyetekeleza mauaji hayo akiwa hai au amekufa.

“Hata kama mtu aliyefanya unyama huo yuko ndani ya familia ya jeshi, atashughulikia ipasavyo ili haki ipatikane,” alisema na kuongeza:

“Nimewaambia askari walio chini yangu wafanye kila liwezekanalo ili aliyehusika na tukio hilo la kinyama akamatwe mara moja akiwa mzima au akiwa amekufa ili haki itendeke.”

Mamia ya askari na wananchi walihudhuria shughuli hiyo iliyofanyika katika viwanja vya nyumba za polisi Kunduchi.

Kamanda Sirro alisimulia jinsi alivyopata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo la askari kupigwa risasi na kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini aliambiwa amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala na alipofika aliambiwa ameshafariki kutokana na kupigwa risasi kwa karibu.

Hata hivyo, aliwakumbusha askari wote kuhakikisha kuwa wanatenda haki wawapo kazini na kukataa rushwa ili hata siku ya mwisho wakati wa hukumu ya Mwenyezi Mungu waweze kwenda sehemu salama.

Msemaji wa familia hiyo, Robert Makule, alisema kifo cha ndugu yao kimewapa mshtuko mkubwa kwani wanapojaribu kuunganisha chanzo cha mauji hayo na maisha yake hawapati jibu.

Alisema wana imani kubwa na Jeshi la Polisi na wako tayari kutoa ushirikiano kwa hali yoyote ili haki ipatikane.

Naye Mbunge wa zamani wa Kinondoni na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Idd Azzan, alisema kitendo cha kuuawa kwa askari huyo kimewasikitisha kwani hawakudhani kama askari wa usalama barabarani anaweza kuuawa kinyama kiasi hicho.

Mwili wa Sajini Mensah jana ulisafirishwa kwenda kijijini kwao Marangu, wilayani Moshi, mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Polisi wampania muuaji wa askari mwenzao.  Polisi wampania muuaji wa askari mwenzao. Reviewed by Zero Degree on 7/27/2016 09:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.