Loading...

Vigogo wenye vyeti bandia presha juu.

WAKATI kazi ya kukagua uhalisia wa vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma ikiendelea kushika kasi nchini kote.

Imefahamika kuwa baadhi ya vigogo katika taasisi mbalimbali ni miongoni mwa maafisa wanaohaha kila uchao hivi sasa kutokana na hofu ya kubainika kuwa hawana sifa za kielimu kushika nafasi walizo nazo. 

Aidha, imeelezwa vilevile kuwa baadhi ya vigogo hao, wamelazimika kujisalimisha kwa viongozi mbalimbali wa kidini kwa nia ya kuombewa ili waepukane na kadhia ya kushughulikiwa kwa udanganyifu wa vyeti huku wengine wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji kwa minajili hiyo pia.

Taarifa ambayo Nipashe imezipata kutoka katika vyanzo vyake kwenye ofisi mbalimbali za taasisi za umma, imebaini kuwa hadi sasa, tayari baadhi ya maafisa wenye kushikilia nafasi nyeti kwenye taasisi mbalimbali za Serikali wamekosa amani na sasa kuhangaika kwao kila uchao kumewalazimu kutumia muda mwingi wakiwa nje ya sehemu zao za kazi kwa nia ya kushughulikia tatizo hilo, lengo likiwa ni kujiokoa kutokana na utata wa vyeti vyao vya shule na taaluma mbalimbali walizodai kusomea.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma hivi karibuni wakati wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako alisema Serikali imedhamiria kuboresha kiwango cha elimu nchini na kwamba, hatua mojawapo inayochukuliwa sasa ni kukagua uhalali wa vyeti vyote vya elimu kwa watumishi wa umma katika sekta ya elimu na sekta nyinginezo.

Alisema lengo la Serikali ni kuona kuwa elimu inayotolewa katika shule, vyuo na taasisi nyingine za elimu inakidhi vigezo kwa kutoa wahitimu wenye sifa.

" Tumekubali kwamba tuna changamoto… katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa kuanzia na hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono" Prof. Ndalichako alikaririwa akisema.

Kufuatia tangazo hilo la Prof. Ndalichako, ambalo linaendana pia na dhamira ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kusafisha uozo katika kila eneo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania, ndipo harakati za ukaguzi wa vyeti vya shule na vile vya kitaaluma zilipozidi kushika kasi na kuibua kitimtim cha aina yake kwa watumishi mbalimbali wanaodaiwa kujipatia ajira serikalini kwa njia za kiujanja-ujanja.

Hofu zaidi inadaiwa kujitwalia nafasi miongoni mwa watumishi walioingia kwenye mfumo wa ajira za Serikali kupitia ‘vimemo’ kutoka kwa wakubwa na pia matumizi ya nyaraka bandia.

Hadi sasa, taasisi mbalimbali za umma zimeshatangaza kuwapo kwa uhakiki kabambe wa vyeti vya watumishi wao, baadhi zikiwa ni halmashauri za wilaya, Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Hatua hiyo ni muendelezo pia wa operesheni nyingine nzito ya kuwabaini watumishi hewa katika taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa mfano, katika waraka mmojawapo wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara kwenda kwa wakurugenzi wengine, mameneja wa mikoa wa mfuko huo, maafisa wa wilaya na wafanyakazi wote, na ambao ulisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ukionyesha kuwa na kumbukumbu namba NSSF/HQ/C/03/7Vol.II/120, inakumbushwa kwamba kwa kuzingatia maelekezo ya awali kupitia waraka wa Juni 13, kila mmoja wao alitakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vyake halisi vya elimu na fani walizosomea kufikia Juni 24, 2016. Na kwamba, yeyote asiyefanya hivyo asingelipwa tena mshahara kuanzia wa mwezi Juni mwaka huu hadi hapo atakapotimiza sharti hilo la kuwasilisha vyeti.

Waraka mwingine mmojawapo kati ya nyingi zilizosambaa kutoka kwa wakuu wa taasisi mbalimbali za umma kwenda kwa maafisa na wafanyakazi wengine wote ni ule uliotolewa Julai 25, 2016 na Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata.
Kupitia waraka huo, wafanyakazi wote wa TRA wametakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vyao halisi kwa wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu katika maeneo yao kufikia Agosti 15, 2016.

“Yeyote atakayeshindwa kutii agizo hili atawajibika mwenyewe,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa Kamishna wa TRA kwenda kwa wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya maafisa wa Serikali walisema kuwa mchakato huo wa uhakiki wav yeti unaoendelea nchi nzima kutokana na agizo la Serikali kwa watumishi wa umma, ni pigo jingine kubwa kwa watu waliozoea kuishi kwa mipango ya kiujanja na kupeana ajira kwa kujuana bila kujali sifa kufuatia hatua nyingine inayoendelea kuwaumbua wengi ya kukomesha upotevu wa mabilioni ya fedha za umma kupitia misharaha iliyolipwa kwa watumishi hewa.

“Hili la ukaguzi wa vyeti ni pigo jingine kubwa kwa watumishi walioingia kwenye mfumo kwa kubebana huku wakitumia vyeti vya bandia… ni tatizo kubwa lililodumu kwa muda mrefu na hivyo wapo watu walioshika nafasi za juu kwa kutumia vyeti vilivyojaa utata wanaohaha wasijue la kufanya,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kuongeza:

“Ofisini kwetu wapo mabosi kama wanne hivi ambao hivi sasa hawana amani hata kidogo na ofisini hakukaliki tena… ni kwa sababu walipata nafasi walizo nazo kwa njia za kubebwa. Wakubwa wetu wanajua na wengi tunatambua siri zao zikiwamo za kutumia majina ya watu wengine, lakini sasa mwisho wao unanukia. Wengi tunasubiri kuona kama watasalimika.”

Aidha, vyanzo zaidi vya Nipashe vimeeleza kuwa baadhi ya vigogo wa nafasi mbalimbali na pia watumishi wengine wa kawaida wamelazimika kujiweka karibu na viongozi wao wa dini huku wengine wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji ili kujinusuru na operesheni hiyo.

“Kuna bosi wetu mmoja hivi sasa kila mara yuko nje ya ofisi akihangaikia suala hilo kwa njia mbalimbali… wengine wanasema ameshasafiri kwenda Sumbawanga, Bagamoyo na pia Tanga kwa ajili ya kutafuta msaada wa waganga wa tiba za jadi ili ukaguzi huu usimuondoe kazini.

Yaani ni shida sana kwa wenzetu walioingia kwa kughushi kwa sababu baadhi wamedumu kwa muda mrefu na kupata vyeo vikubwa kwa sababu ya uzoefu wao kazini,” chanzo kingine kiliiambia Nipashe.

Vyanzo vya Nipashe vimedai vilevile kuwa miongoni mwa vigogo wanaotapatapa, ni pamoja na wale ambao waliingia kwa vyeti vya kufoji lakini wakatumia nafasi zao kazini kujiendeleza kwenye vyuo mbalimbali na kuhitimu.

Hali hiyo ya hofu kwa vigogo wa kundi hilo inatokana na ufafanuzi mwingine uliokaririwa hivi karibuni kutoka kwa Prof. Ndalichako, ukieleza kuwa watumishi waliomaliza vyuo huku wakiwa hawana sifa pia hawatasalimika.

“Wafanyakazi waliosoma vyuo vikuu bila ya kuwa na sifa wajiandae kung’olewa,” alisema Prof. Ndalichako na hivyo kuibua hofu pia kwa watumishi walioajiriwa kwa vyeti visivyo na sifa ya kuhalalisha ajira zao, lakini wakajiunga katika vyuo mbalimbali na kujiendeleza.

“Hii Serikali ya awamu ya tano haitabiriki… kila siku wanaibuka na njia za kukomesha mambo ya hovyo yaliyozoeleka na kuchukuliwa kuwa ni jambo la kawaida katika jamii yakiwamo haya ya watumishi wasiokuwa na sifa za kielimu au kutumia vyeti bandia… matokeo yake ndiyo haya ya baadhi ya watu kujisalimisha kwa waganga wa kienyeji, lakini sidhani kama yupo atakayepona kwa kufanya hivyo, muhimu ni kujisalimisha na kusubiri hatua zitakazochukuliwa, ila wengi wataumbuka,” afisa mmoja wa ngazi za chini katika idara moja nyeti ya Serikali aliiambia Nipashe na kuongeza:

“Sisi wenzangu na mie hatuna hofu… tatizo kubwa lipo kwa mabosi wetu wasiokuwa na sifa kwa sababu walizoea kuishi kifalme kwa nafasi wasizostahili. Hawa ndiyo wanaohaha kwa viongozi wa dini na pia kwa waganga wa kienyeji ili wasaidiwe kuepukana na aibu ya kutumia vyeti bandia ili kupata utukufu.”

Mtumishi mwingine wa halmashauri moja jijini Dar es Salaam aliiambia Nipashe kuwa yeye amefurahishwa na hatua hiyo ya Serikali, akiamini kuwa sasa heshima ya elimu itarudi.

“Kama unavyojua, miaka ya nyuma hakukuwa na mkazo wowote kutoka kwa viongozi wa juu kuhusiana na suala hili. Wapo watu wana vyeti kutoka katika vyuo visivyotambulika lakini bado wameishia kupandishwa vyeo na sasa ni mabosi wakubwa sana… wapo watu wanatumia vyeti vya kughushi, wapo wenye kutumia vyeti vya wafu, wapo walionunua vyeti mitaani na kila aina ya vituko. Suala hili la ukaguzi ni muhimu sana ili kila mtu apate ajira kulingana na kiwango chake cha elimu,” aliongeza afisa mwingine wa halmashauri.

Akifafanua zaidi, afisa mmoja wa nafasi ya juu katika taasisi moja ya kiuchunguzi alisema mpango huo wa kuwasaka watumishi wenye kutumia vyeti bandia na kuwachukulia hatua ni muhimu kwa ustawi wa taifa kwa sababu taifa lilikuwa likielekea gizani.

“Ilifikia mahala hadi watungaji wa sheria pale bungeni walikumbwa na tuhuma za kuwa na watu wanaotumia vyeti vya kufoji, wapo mawaziri walikuwa wakinyooshewa vidole kwa tatizo hili na pia kuna watu wanazo hadi Phd (shahada za uzamivu) za vyuo bandia. Katika hali kama hiyo, hakuna namna nyingine isipokuwa ni kutekeleza kwa vitendo mpango huu wa serikali. Sote tunapaswa kuunga mkono jambo hili,” mmoja wa maafisa wa Serikali aliiambia Nipashe.

“Kuna vijana wazuri tu wanamaliza vyuoni lakini wanakosa ajira kwa sababu ya kuwapo kwa kundi la watu hawa wanaotumia vyeti bandia. Wapo tunaofurahia sana jambo hili lakini wapo pia baadhi ya vigogo wanatapatapa mno kwa kujua kuwa siku zao zimefikia ukingoni, lakini hakuna njia nyingine ya kukomesha hili tatizo isipokuwa ni hiyo ya kuwabaini wahusika na kuwang’oa hata kama wanshikilia nafasi za juu za uongozi, ” aliongeza afisa huyo.

MATANGAZO KUPOTEA VYETI

Katika uchunguzi wake kuhusiana na athari za kuwapo kwa operesheni hiyo, Nipashe imebaini kuongezeka ghafla kwa matangazo ya kupotea kwa vyeti vya elimu katika vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumzia hali hiyo, mwalimu katika shule moja ya sekondari iliyopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema kuwa kuongezeka kwa matantgazo ya upotevu wa vyeti ni matokeo ya ukaguzi unaoendelea nchini kote.

Akieleza zaidi, mwalimu huyo alisema kadri anavyoamini, ni kwamba miongoni mwa wale wanaotangaza kupotelewa vyeti, wapo wenye kukabiliwa kweli na tatizo hilo na pia, wapo wengi wao ambao wameibuka sasa ikiwa ni njia mojawapo ya kujaribu kujitetea kwa waajiri wao kuhusiana na sababu za kutokuwa na vyeti hivyo.

“Kuna watu wameajiriwa bila ya kuwa na sifa. Hawana vyeti vya kweli lakini waliajiriwa kwa kubebwa… sasa njia pekee ya kujiosha ni hiyo ya kudai kuwa wamepoteza vyeti vyao. Hata hivyo, sidhani kama hilo litawasaidia kwa sababu siku zote, penye ukweli uongo hujitenga,” mwalimu huyo alisema.

BABU LOLINDO AFUNGUKA

Baadhi ya viongozi wa kidini na pia waganga wa kienyeji wamezungumzia madai ya kuwapo kwa vigogo wanaomiminika kwao kwa nia ya ‘kusaidiwa’ ili kulinda vibarua vyao licha ya kuwa na vyeti vya bandia vya elimu.

“Ni kweli, watu wa aina hiyo wanakuja lakini siyo wengi sana, wengi wanaonekana ni watu wenye nafasi za juu kwa sababu ya muonekano wao na maelezo yao … inaelelekea hali ni mbaya lakini hakuna njia rahisi ya kuwasaidia zaidi ya kuwapa moyo tu kwamba wawe na subira,” mmoja wa waganga wa kienyeji jijini Dar es Salaam aliiambia Nipashe juzi.

Mchungaji Ambilikile Mwasapila wa Kijiji cha Samunge, Loliondo -- maarufu kwa jina la ‘Babu wa Loliondo’ -- aliiambia Nipashe kuwa yeye hajawahi kufuatwa na mtu yeyote anayetaka kupata huduma ya kinga dhidi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yake kutokana na kughushi vyeti vya elimu.

Hata hivyo, Babu wa Loliondo aliongeza kuwa yeyote mwenye nia hiyo asijisumbue kwenda kwake kwa sababu kamwe hawezi kumsaidia mtu anayekwenda kinyume cha nia ya Rais Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano, katika kukabiliana na vitendo viovu vikiwamo hivyo vya watu kujipatia ajira kwa kutumia vyeti bandia au kubebwa na ndugu zao.

“Hao watu wakigundulika wafukuzwe tu. Hawastahili kwa sababu licha ya kuiibia serikali, lakini pia wanamuibia Mungu,” alisema Babu wa Loliondo aliyewahi kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na ugawaji wa kikombe cha dawa uliovutia maelfu ya watu kijijini kwake Samunge.

Aidha, akifafanua zaidi, Babu wa Loliondo alisema kadri anavyofahamu yeye, watu hao wenye vyeti bandia wanajisumbua bure kutafuta kuombewa na viongozi wa dini kwa sababu hakuna muujiza unaoweza kutokea sasa ili kubadili vyeti bandia kuwa halisi na sababu kubwa ni moja tu, akisema: “Mungu hawezi kusaidia mwanadamu katika kufanya vitendo viovu… jambo hilo halimpendezi Mungu na hivyo hakuwezin kukawa na muujiza kwa namna yoyote ile,” alisema na kuongeza:

“Akija yeyote hivi sasa sasa kuhitaji nimsaidie kwa masuala ya vyeti bandi, nitatamuelekeza kufanya toba kwa Mungu kwanza ili asamehewe.”

Source: Nipashe(IPPMedia)
ZeroDegree.
Vigogo wenye vyeti bandia presha juu.  Vigogo wenye vyeti bandia presha juu. Reviewed by Zero Degree on 7/30/2016 10:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.