Loading...

Yanga kusuka au kunyoa leo

Kama ni kazi, basi Yanga inayo mbele yake! Timu hiyo inakabiliwa na majukumu matatu makubwa na
muhimu inapoikabili Medeama ya Ghana kwenye mchezo wa hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Jukumu la kwanza linaloikabili Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni kurejesha makali yake na kupata bao lake la kwanza kwenye hatua hiyo ya makundi, Kundi A kutokana na kutofunga bao lolote tangu ilipoingia hatua hiyo, ikiwa imefungwa 1-0 kwenye mechi zake mbili zilizotangulia dhidi ya MO Bejaia na TP Mazembe.

Jukumu la pili; Yanga, inalo deni la kuwafurahisha mashabiki kwa kupata ushindi wa kwanza tangu kuanza kwa hatua hiyo ya makundi baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo kwenye kundi hilo A la mashindano hayo.

Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola jijini, Dar es Salaam, Yanga imesubiri kwa dakika 270 za mashindano hayo ya pili kwa umaarufu barani Afrika bila kupata ushindi, sare wala bao.

Kitu cha tatu kinachowakabili wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mashindano hayo, ni kumaliza unyonge wa muda mrefu dhidi ya timu za Afrika Magharibi kila inapokutana nazo kwenye mashindano mbalimbali barani humo.

Ushindi wa mwisho iliopata timu hiyo dhidi ya timu kutoka ukanda huo wenye mataifa yaliyoendelea kisoka ulikuwa miaka 16 iliyopita ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam dhidi ya Cadets Club kutoka Mauritania kwenye lililokuwa Kombe la Washindi.

Kimtazamo, Yanga inacheza nyumbani na mashabiki wake ambao wanaweza kugeuka mtihani mkubwa zaidi kwa klabu hiyo ambayo washambuliaji wake, wakiongozwa na Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Mzambia Obrey Chirwa wanatakiwa kurekebisha makosa yote ambayo yamekuwa sababu yao kukosa shabaha na kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi ambazo timu hiyo imekuwa ikizitengeneza kwenye mechi zake.

Katika mechi zake kumi za mwisho ilizocheza timu hiyo, imefunga zaidi ya mabao matatu mara mbili pekee, ambayo ni sawa na asilimia 20, huku katika mechi nane ikifunga mabao chini ya matatu, sawa na asilimia 80.

Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm amekuwa akiwapa mazoezi maalumu ya kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma kwenye ngome na kupanda mbele.

Pluijm amekuwa akiwafundisha nyota wake kutokea pembeni na pia kupenya katikati.


Umakini unahitajika zaidi


Mbali ya ubutu kwa washambuliaji, safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo tayari imeruhusu mabao mawili hadi sasa inatakiwa kubadili umakini wake inapoikabili Medeama.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia dakika ya 31 hadi 45, kipindi cha kwanza, Medeama imekuwa ikifunga mabao mengi. Katika mabao 11 ambayo timu hiyo imefunga kwenye mechi zake za hivi karibuni, manne yamefungwa kwenye dakika ya 31 hadi 45 ya kipindi cha kwanza ambayo ni sawa na asilimia 36.36 ya mabao yote iliyofunga timu hiyo.


Wasemavyo wachambuzi


Mchambuzi na kocha, Joseph Kanakamfumu amesema Yanga bado ina nafasi kubwa ya kufanya vyema Afrika, ila inatakiwa kupambana kupata mabao akimshauri kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm ampumzishe kiungo, Haruna Niyonzima.

“Nafikiri,) Pluijm atamweka benchi Niyonzima, kisha Thabani Kamusoko asogee juu ili kucheza kama kiungo mchezeshaji na kiraka Mbuyu Twite acheze kama kiungo mkabaji.

“Kwa upande wa mawinga, wacheze Simon Msuva na Juma Mahadhi kwa sababu Niyonzima kwenye mechi za karibuni hana msaada mkubwa kwa timu.

“Anachelewesha mashambulizi, anakaa na mpira, hapigi pasi za mwisho tofauti na anavyocheza Kamusoko, “ amesema na kuongeza:

” Yanga ibadilike kwani wachezaji wengi wanapenda kupiga pasi za pembeni na siyo za kwenda mbele ili timu ishambulie, hilo linawagharimu mara kwa mara kwa sababu ukicheza pasi za pembeni, wapinzani wakikamata upande wa mawinga wako, ujue umekwisha.”

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe amesema wanachotakiwa kufanya Yanga ni kushambulia muda wote wa mchezo ili kupata mabao.


ZeroDegree.
Yanga kusuka au kunyoa leo Yanga kusuka au kunyoa leo Reviewed by Zero Degree on 7/16/2016 10:10:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.