Loading...

Zito atoa mrejesho wa utekelezaji wa Malengo 15 ya ACT yaliyoelezwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015.

Hali ya Utekelezaji wa Malengo 15 ya ACT Wazalendo
Manispaa ya Kigoma Ujiji 2015 - 2020.

Usuli

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 tulieleza malengo yetu kwa wananchi. Leo tunatoa mrejesho wa utekelezaji kama tulivyoahidi. Ifahamike kuwa huu ni mwaka wa kwanza wa Bajeti hivyo mambo mengi ni ' work in progress '. Bado kuna changamoto nyingi sana ikiwemo kuhakikisha kuwa Mpango kabambe wa mji wetu unakamilika na kutekelezwa.

UTEKELEZAJI wa Malengo

1. Kushirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha barabara zote za mkoa zinaunganishwa Kwa Lami. Barabara za Kigoma - Nyakanazi, Mwandiga - Kagunga na Simbo - Kalya ni mfano wa barabara hizo.

UTEKELEZAJI:

Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 tumefanikiwa kupata Mradi wa barabara ya Manyovu - Kasulu - Kibondo jumla ya kilometa 240. Benki ya Maendeleo ya Afrika itafadhili barabara hii na TANROADS itaigawa kwa kuweka wakandarasi 4 ili ikamilike kabla ya mwaka 2020. 


Barabara ya Mwandiga - Kagunga TANROADS Mkoa imeshatangaza zabuni za kuanza kuifungua na mchakato wa kupata mkandarasi umeanza. Pia Barabara ya Msimba - Ujiji ( Kasulu Road ) inajengwa Kwa Lami na kilometa nyengine 10 ikiwemo ya Mwembetogwa - Msikitini Kigoma zinajengwa Kwa Lami. 

Zabuni ya kujenga mzunguko ( roundabout ) ya Mwanga Sokoni tayari imetangazwa na kufunguliwa na ujenzi unaanza mwaka huu wa Fedha 2016/17.

2. Kuhakikisha kuwa Mitaa ya Manispaa inakuwa na miradi maalumu ya kujengwa mifereji na barabara za Lami na mawe Kwa lengo la kusafisha mji na kuzalisha ajira Kwa vijana. Pia kumaliza kero za miundombinu Mto Luiche kata ya Kagera [ kwa kujenga daraja na barabara kutokea Ujiji ]. ----

UTEKELEZAJI:

Mkandarasi wa kujenga mfereji wa Lubengela ameanza Kazi ya kukusanya vifaa ( mobilization ). Mtaa wa Rusimbi Ujiji na Barabara ya Shindika - Jihad - Katubuka na Barabara ya Mwami Rusimbi Gungu ipo kwenye Mpango wa kuwekwa Lami. 


Mradi wa kuweka Lami Mitaa ya MwembeNgoma - Kisangani - Msufini - Kwa Bella na barabara ya Kaya - Simu zinajengwa kwa lami. Manispaa imekubaliana kimsingi na Shirika la BTC la Ubelgiji kufanya upembuzi yakinifu na Usanifu wa kina wa Mitaa ya Mawe/pavements katika kata 8 za Manispaa. 

Barabara ya Ujiji - Kagera ikiwemo Daraja la Mto Luiche ni sehemu ya Mradi mkubwa wa Umwagiliaji katika Mto Luiche. Usanifu wa Barabara ya ufukweni kutoka Forodha ya Ujiji mpaka Katonga ( Kikamba ( Bangwe) - Ujiji Forodhani road ( planned) unafanyika mwaka 2016/17 na Barabara ya Bangwe - Ujiji ipo kwenye Mpango wa TANROADS. 

Mtaa wa Mzee Menge unawekewa ' pavement ' wote Kwa ajili ya Soko la Jioni ( Mzee Menge Street Night Market Project ). Barabara ya Msimba - Ujiji ( Kasulu road ) tumeiorodhesha kwenye miradi ya Barabara za ahadi za Rais za 10km za Lami katika mji wetu.

3. Kuboresha mazingira ya Biashara Kwa kuondoa kero ya ushuru Kwa wafanyabiashara wadogo Kwa mujibu wa Sheria ndogo za Manispaa, kuboresha Bandari zote na kujenga Bandari mpya(jetty) eneo la Forodha ya Ujiji ili kurudisha hadhi ya mji wa Ujiji. -------

UTEKELEZAJI:

Mamlaka ya Bandari ( TPA ) inatangaza zabuni ya ujenzi wa Jetty Forodha ya Ujiji Mwezi Agosti 2016, pia Bandari ya Kibirizi. Sheria ndogo tunazopendekeza Kwa Waziri wa TAMISEMI zinarekebisha kodi na tozo Kwa kufuta kabisa ushuru wa wanaotandika bidhaa chini. 


Soko jipya la Jioni Mtaa wa Mzee Menge linaanzishwa kutoa fursa ya Wafanyabiashara wadogo kufanya biashara bila bugudha. Shirika la PSPF linaanza ujenzi wa Soko la Mwanga ambapo ndani yake kutakuwa na Mnada wa Kimataifa wa Asali. Baada ya Soko la Mwanga kukamilika, Soko la Mjini Kigoma litabolewa na kujengwa Shopping Mall. Soko la Ujiji lina Mradi maalumu wa kujenga Kituo cha Kikanda cha Biashara ( trading and logistical center - Ujiji City Project ). 

Mradi huu utakaotokana na uwekezaji kutoka nchini China utawezesha ujenzi wa maduka 3000, Warehouses na nyumba za makazi. Lengo la Mradi huu ni kuwezesha Ujiji kuwa eneo ( a Hub ) la wananuzi wa bidhaa kutoka Nchi za Maziwa Makuu badala ya watu hao kusafiri kwenda Mashariki ya mbali. 

Kupitia Miradi ya LIC inayofadhiliwa na Serikali ya Denmark, Manispaa inatarajia kuweka mazingira bora ya biashara Kwa kuondoa vikwazo ili Wafanyabiashara waweze kuwekeza, kufanya biashara na kuzalisha ajira nyingi Kwa wananchi. Manispaa pia inatengeneza ' masterplan ya mji ' ili kuupanga vema. 

Katika mipango ya muda Mfupi Manispaa imeanza mchakato wa kuomba kuongeza eneo lake ili kukidhi haja ya ongezeko la watu na shughuli za uchumi. Manispaa imeomba kuongeza kata za Mwandiga, Simbo, Msimba na Ziwani zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma ili ziingizwe Manispaa.

4. Kuhamasisha vikundi vya Wananchi kama wavuvi, kina mama, wakulima wa bustani, waendesha vyombo vya usafiri na kuviunganisha na mifuko ya hifadhi ya jamii Kwa kuchangia sehemu ya michango yao ili wapate mafao ya kama mikopo nafuu na Bima ya afya. 50% ya Bajeti ya Mfuko wa Mbunge itachangia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Manispaa. ----

UTEKELEZAJI:


Baraza la Madiwani limepitisha Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Manispaa Kwa ajili ya utekelezaji. Mwaka 2016/17 Fedha za Mfuko wa Mbunge zimesaidia kuondoa changamoto ya madawati. Fedha zitokanazo na 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri zitatumika kuchangia vikundi vya Vijana na Wanawake kwenye Hifadhi ya Jamii na kuwawezesha kupata Mikopo. 

Manispaa imefanya mazungumzo na Benki ya Dunia ili wachangie katika Skimu hii Kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wa Manispaa wanakuwa na Bima ya Afya. Manispaa bado inaendelea kufanya mazungumzo na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kupata Mfuko mwafaka wa Kuendesha Skimu hii. Skimu hii, pamoja na mambo mengine, itaongeza uwezo wetu wa kuweka Akiba Kwa ajili ya uwekezaji wa ndani ili kukuza uwezo wetu wa uzalishaji ( productive capacity ).

5. Kushirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kuanzisha Benki ya Kigoma ili kuwezesha Wafanyabiashara wa Kigoma kukuza mitaji yao na hivyo kupanua [ Biashara ] zao. ----

UTEKELEZAJI:

Bado hatujachukua hatua zozote. Baada ya Skimu ya Hifadhi ya Jamii kuanza rasmi Manispaa ya Kigoma itaweza kuanzisha Benki ya Jamii ( community Bank ) na kualika Halmashauri nyengine mkoani na Vyama vya Ushirika kuwa wanahisa na hivyo kutimiza malengo yetu.

6. Kusimamia kikamilifu kuanza Kwa Mradi wa kufua umeme Kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto Malagarasi ( Igamba III ) na kumaliza kabisa tatizo la umeme wa uhakika mkoani Kigoma. ------

UTEKELEZAJI:


Bajeti ya mwaka 2016/17 imetenga Fedha Kwa ajili ya kuanza kutekelezwa Kwa ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Igamba III ( Malagarasi Hydro Power ). Hata hivyo Manispaa inafanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa Maendeleo ili kuweza kuwa na Mradi mkubwa wa Umeme mbadala Kwa ajili ya kuendesha mitambo ya Maji na kuwezesha kila nyumba kuwa na umeme. Mipango hii ikikamilika tutatoa Taarifa kwa wananchi.

7.
Kuhakikisha Mradi mkubwa wa Mpunga katika Bonde la Mto Luiche unaanza ili kuzalisha ajira katika Kilimo na Viwanda vya Mazao ya kilimo. ---

UTEKELEZAJI:
Serikali ya Kuwait imekubali kufadhili Mradi huu wenye thamani ya US$ 15 milioni ikiwemo Miundombinu ya barabara na madaraja kuelekea kwenye Mradi.

8. Kumaliza tatizo la fidia Kwa waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma [ Gombe-Mahale International Airport ] na miradi ya Bandari Kavu Kibirizi na Katosho.

---- UTEKELEZAJI:

Zabuni ya ujenzi wa jengo la abiria ( passenger terminal ) na barabara za kuingia Uwanja wa Ndege wa Kigoma tayari zimeandaliwa na kupelekwa European Investment Bank Kwa ajili ya kupata kibali. Zabuni ya kuongeza Urefu wa Uwanja kufikia mita 3000 ili ndege kubwa ziweze kutua bado Kwa sababu ya changamoto ya fidia. Wananchi wanasema fidia ni ndogo. Changamoto hiyo pia ipo Kwa fidia za Bandari Kavu ya Katosho. Tunaendelea na juhudi ya kupata mwafaka ili miradi hii ianze kutekelezwa.

9. Kusimamia uanzishwaji wa Viwanda kupitia KiSEZ. Tutaanza na Viwanda vya mazao ya Mawese/Michikichi na viwanda vya kuchakata Samaki kufuatia kuboresha Uvuvi. ----

UTEKELEZAJI:

Miradi hii inategemea sana kumalizika Kwa tatizo la umeme. Hata hivyo chini ya miradi ya LIC inayofadhiliwa na Serikali ya Denmark, Mradi wa Uvuvi unaanza kuboreshwa na miradi ya uzalishaji wa Michikichi kupitia sekta binafsi. Manispaa pia imepitisha kanuni za mabwawa ya kufuga samaki ili kuwekeza kwenye mabwawa yaliyopo ndani ya Manispaa.

10. Kuendelea kuwatetea watu wa Kigoma dhidi ya unyanyasaji kuhusu uraia wao na kukomesha kabisa manyanyaso hayo Kwa kuhakikisha kuwa kipaombele cha vitambulisho vya uraia kinakuwa mji wa Kigoma. ----

UTEKELEZAJI: ni Kazi endelevu

11. Kuanzisha timu ya soka ya manispaa na kuhakikisha inafika ligi kuu. Hii litaenda na kuanzidhwa Kwa shule Maalumu ya Michezo (sports academy) ili kukuza vipaji vya Soka.

---- UTEKELEZAJI:


Hivi sasa kuna timu ya Kigoma ya Mvuvumwa FC ambayo ipo daraja la kwanza. Tunadhani ni vema kuiunga mkono timu hiyo ili kuiwezesha kupanda daraja kufika ligi kuu badala ya kuanzisha timu mpya. Manispaa ina mazungumzo na Klabu ya Azam Kwa ajili ya kufungua Tawi la Academy yake katika uwanja wa Kawawa, Ujiji. 


Manispaa pia inafanya mazungumzo na wafadhili kuanzisha Mwami Ruyagwa Youth Park ( MRYP) katika eneo la Mwanga Community Centre ili kutoa mafunzo ya Michezo mbalimbali Kwa vijana na kuibua vipaji.

12. Kukuza Utalii ili kuzalisha ajira Kwa vijana wengi zaidi wa mkoa wa Kigoma. ----

UTEKELEZAJI:

Manispaa inajenga Tourist Information Centre katika eneo la Kigoma Mjini mbele ya Soko la Kigoma Kwa kushirikiana na TANAPA.

13. Kufuatilia kikamilifu na kumaliza kabisa changamoto ya wavuvi kuvamiwa na kuporwa Mali zao.

UTEKELEZAJI: 


ni Kazi endelevu

14. Kukamilisha mradi mkubwa wa Maji ili kumaliza tatizo la maji; kupitia Hifadhi ya Jamii kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu; na kusimamia kikamilifu uboreshwaji wa elimu katika manispaa - kuboresha Chuo cha VETA, Kuanzisha High School 2 na kuboresha Shule za Msingi. -----

UTEKELEZAJI:

Mradi wa Maji unakamilika na tunatarajia kuwa ifikapo Mwezi Oktoba Mradi wa Maji Kigoma utakuwa umekamilika. Hivi sasa mabomba yanatandazwa. Changamoto kubwa itakuwa ni gharama za nguvu ya umeme kuendesha mitambo hii. 


Tumeanza mazungumzo na wadau ili kuweka Solar Panels za kuzalisha umeme wa kutosha kuendesha mtambo na ziada kuuza TANESCO. Shule ya Buronge High School inaanza 2016/17 na itafuatiwa na Shule ya Kichanga Chui. Lengo letu ni kukamilisha High School 3 za Manispaa mpaka ifikapo mwaka 2019. Hata hivyo, tuna Mradi maalumu wa kuibadili Shule ya Msingi Kigoma ( Aghakan ) kuwa High School ya masomo ya Sayansi tu na kuhamisha Shule ya Msingi Kigoma kwenda eneo la jirani na makazi ya Mkuu wa Mkoa. 

Madawati ya Shule za Msingi na Sekondari yametengenezwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu inafanyika. Mwezi Septemba 2016 kutakuwa na Tamasha kubwa la kuchangisha zaidi ya tshs 300 milioni Kwa ajili ya kumaliza kabisa changamoto ya Madawati. 

Tamasha Hilo litaendeshwa na Mwanamuziki mkubwa nchini mwenye asili ya mkoa wa Kigoma. Tunafanya jitihada za kupata Ujiji Technical School yenye uwezo wa kudahili wanafunzi 5000. Upande wa Afya, Manispaa inatumia teknolojia Kudhibiti upoteaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya. Mfumo huu uliandaliwa na mvumbuji kijana mwenye asili ya Kigoma ndg. Bukhary Kibonajoro.

15. Kuanzisha na kuendesha Jukwaa la viongozi wa Dini ili kuendeleza mahusiano mema Kati ya waumini wa dini mbalimbali. ---

UTEKELEZAJI:

lilianza kutekelezwa tangu wakati wa kampeni. Kila mwaka Mara 2 tutakuwa tunakutana na Viongozi wa dini ili kujadili changamoto mbalimbali za mji wa Kigoma Ujiji. Kabla ya mwisho wa mwaka tutafanya Mkutano wa mwisho wa mwaka na Viongozi wa Dini katika Manispaa.

Hitimisho

Manispaa yetu bado inakabiliwa na Changamoto lukuki lakini kubwa kuliko yote ni changamoto ya uchumi - uzalishaji na ajira. Mzunguko wa Fedha kwenye mji bado ni mdogo sana kutokana na uzalishaji mdogo kwenye Kilimo na Uvuvi, kukosekana Kwa Viwanda hasa Viwanda vya kuongeza thamani ya Mazao ya Kilimo na Uvuvi na biashara ya Kimataifa kutochangamka licha ya Kigoma kuwa mpakani na Nchi nyengine na kuwepo Kwa Bandari ya Kigoma. Tusipokabiliana na changamoto hizi jitihada za kujenga Miundombinu hazitakuwa na maana sana. 


Mradi wa Ujiji City ( trade and logistical Hub ) utaweza kuongeza biashara ya Kimataifa na hivyo mzunguko wa Fedha. Vile vile Mradi wa Umwagiliaji Delta ya Mto Luiche utasaidia kukuza uzalishaji katika Kilimo na Viwanda vidogo. Kuna haja ya kuongeza juhudi katika Viwanda vya Mawese na Mazao yake kama sabuni nk na pia uzalishaji wa mbogamboga. Vile vile sekta ya Utalii inaweza kuwa chachu kubwa ya Maendeleo ya Manispaa.

Manispaa pia imejiunga na Mpango wa kuendesha Serikali Kwa uwazi ( OGP ) ili kuwezesha kuboresha utawala bora. Lengo la Manispaa ni kuweka mikataba yake yote wazi, kuweka wazi mchakato wa Bajeti ya Manispaa na kuendesha sekta za Elimu, Afya na Ardhi Kwa namna ambayo wananchi wanashiriki Kwa ukaribu mkubwa na kuwajibisha Viongozi.

Shabaha yetu ni kuwa Manispaa ya mfano nchini Tanzania.

Zitto Ruyagwa Zuberi Kabwe, Mb
Kigoma - Ujiji
9/8/2016.



ZeroDegree.
Zito atoa mrejesho wa utekelezaji wa Malengo 15 ya ACT yaliyoelezwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Zito atoa mrejesho wa utekelezaji wa Malengo 15 ya ACT yaliyoelezwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Reviewed by Zero Degree on 8/09/2016 09:47:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.