Loading...

Kamari janga jipya.

Ni JANGA kubwa. Ndivyo unavyoweza kusema, kutokana na kundi kubwa la vijana wakiwamo wazee na wanawake kugeukia mchezo wa kubahatisha ambapo kila kukicha vituo vya kamari ya soka na michezo mingine maarufu kama ‘kubeti’ vimekuwa vikiongezeka.

Mchezo huo ambao umekuwa ukikusanya idadi kubwa ya mashabiki hutumia fedha kwa kubashiri mechi za mpira mbalimbali za mataifa ya nje na kushinda kiasi kikubwa cha fedha.

Kushamiri kwa mchezo huo kumekuja miezi michache baada ya tamko la Rais Dk. John Magufuli, kupiga marufuku mchezo wa ‘Pool Table’ asubuhi huku akitaka vijana watafute shughuli za kufanya ikiwemo kilimo, badala ya kupoteza muda katika mchezo huo.

Agizo hilo la Rais Magufuli, alilitoa Mei 16, mwaka huu alipokuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa, ambapo kwa sasa makundi hayo yamegeukia mchezo wa ‘kubeti’.

Kamari hiyo kwa sasa imekuwa ikiwateka watu wa jinsi na rika zote na sasa imeshika kasi, huku vituo vya kuchezesha vikichipuka kama uyoga katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam na mikoani.

Takwimu za Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu Tanzania, zinaonesha kuwa kwa nchi nzima kuna vituo vya kubeti 2,684 huku Mkoa wa Dar es Salaam pekee ukiwa na vituo 1,344.

Kundi kubwa la wanafunzi, vijana na wafanyakazi wamekuwa wakicheza kwa kutumia simu zao za mkono au mitandao jambo ambalo linaweza kuwa hatari kwa nguvu kazi ya taifa.

Vituo maarufu ni Premier Betting na Meridian Betting, ambavyo vyote vipo katika ushindani mkubwa wa kuchezesha mchezo huo na kuvuta watu wengine jijini.

Gazeti hili lilifanya utafiti kwa zaidi ya wiki moja na kutembelea maeneo ya Mwenge, Magomeni, Kariakoo, Tandale, Tandika, Manzese, Mikocheni, Msasani na Temeke na kukuta makundi ya watu wa jinsia zote na rika mbalimbali wakiwa na makaratasi huku wakibashiri mechi mbalimbali kwa viwango tofauti vya fedha.

Pamoja na hatua hiyo inaelezwa kuwa zaidi ya asilimia 45 ya watu hushiriki mchezo huo kwa njia mbalimbali ikiwemo kununua katarasi maalumu maarufu kwa jina la ‘mkeka’, mitandao na hata kwa njia ya simu.

Alipotafutwa kwa siku juzi na jana Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Abbas Tarimba, alimtaka mwandishi wa habari hizi kufika ofisini kwake akiwa na kitambulisho ndipo anaweza kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo.

Mabilioni yakusanywa

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Abbas Tarimba alinukuliwa na mtandao wa Blog ya Jaizmela Leo pamoja na gazeti la Nipashe ambapo alisema kuwa michezo hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwenye bodi hiyo na kuongeza mzunguko wa fedha unaozidi Sh bilioni 1.4 kwa mwezi.

Alisema michezo hiyo ya kubahatisha inafanya vizuri, kwani mapato yake kwa bodi hiyo hufikia Sh bilioni 14 kwa mwaka.

“Huu mchezo umekuwa na mchanago mkubwa katika pato la Taifa kwa mwaka 2012/13 hadi Desemba 2015 Shilingi bilioni 14.0 zilikusanywa na pia kutoa ajira zaidi ya 7,000 kwa watu wa rika mbalimbali,” alisema Tarimba.

Mkurugenzi huyo wa michezo ya kubahatisha, alisema kuwa sheria ya michezo ya kubahatisha inakataza mtoto chini ya umri wa miaka 18 kushiriki mchezo huo.

Kutokana na hali hiyo aliwataka wamiliki wa vituo vya kamari hizo kufuata kanuni zilizoainishwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini.

Tarimba alisema matatizo kadhaa yanayojitokeza kwenye michezo hiyo ni pamoja na malalamiko ya kutotendewa haki kwa wachezaji.

Bajeti ya Serikali

Akiwasilisha bajeti ya mwaka 2016/17 katika Bunge la Bajeti Juni 9 mwaka huu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, inatarajia kukusanya kodi itakayofikia Sh bilioni 34.72, sawa na ongezeko la asilimia 26.35 ikilinganishwa na Sh bilioni 27.48 inayotarajiwa kukusanywa katika mwaka wa 2015/16.

Kutokana na hatua hiyo bodi hiyo imejipanga kuendelea kusimamia vema sekta ya michezo ya kubahatisha nchini na kuhakikisha kwamba inaendelea kuendeshwa kwa mujibu wa sheria.

“Bodi inatarajia kuchangia kiasi cha Shilingi bilioni 2.17 kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina katika mwaka 2016/17 hii ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 50.69 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 1.44 ya mwaka wa 2015/16,” alisema Waziri Dk. Mpango

Kauli za wachezaji

Mmoja wa wachezaji wa mchezo huo aliyehojiwa na gazeti hili, Said Simion mkazi wa Magomeni Mwembe Chai, alisema alianza kucheza mchezo huo mwaka jana na amefanikiwa kushinda mara nyingi.

“Nimeshawahi kushinda na kufanikiwa kupata Sh 200,000 mara mbili, na pia nimeshinda na kupata Sh 500,000 mara tatu lakini kwa hizi fedha ndogo za 10,000 hadi 50,000 huwa nazipata kila wakati,” alisema

George Silawa ambaye amekuwa akibeti kupitia Kampuni ya Meridian, alisema ingawa anakosa mara moja moja, lakini mara nyingine amekuwa akishinda na kujipatia fedha ambazo huziingiza kwenye biashara yake ya duka.

Mmoja wa wapiga debe katika eneo la Manzese, Kalama Kalama (26), alisema huwa anakusanya fedha zake na kwenda kucheza kamari hiyo kwa kubashiri ‘mkeka’.

“Binafsi huu mchezo huwa naupenda sana maana kuna siku nilipata Shilingi 10,000 lakini nikafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana na nikienda kubeti huwa napata hadi Shilingi 70,000 na nikipata hutenga hata Shilingi 20,000 kucheza tena kwa siku inayofuata kwani ninakuwa na kianzio.

“Nina miaka miwili nacheza betting, kabla hata mchezo huu haujachukua umaarufu nilikuwa nacheza karata kamari,” alisema Kalama

Muuza mitumba Ally Kisukuna ambaye ni mfanyabiashara wa Mwenge, alisema kwa miaka mingi anashiriki mchezo huyo.

“Nacheza betting nina muda ila sijawahi kushinda. Sichezi kila siku ila ninapojisia,” alisema

Namna unavyochezwa

Wakala wa bahati nasibu ya Premier, iliyopo Msasani Albert Franchesco, alinukuliwa na gazeti moja (si MTANZANIA) alieleza jinsi kamari hiyo inavyochezwa na kwamba kushinda kunahusisha bahati na kuijua soka, wachezaji na timu zao.

“Ili kushiriki, mchezaji lazima uchukue ratiba ya timu zote. Huu ni kama mtihani wenye maswali. Maswali hayo huwa na namba ambazo kwenye kamari ni kama ‘code’.

“Kwa kawaida kila timu ina ‘code’ yake, unachotakiwa kufanya ni kuangalia pointi za timu kisha unazijumlisha pointi hizo pamoja na kiasi cha fedha unachoweka.

“Baada ya kuchagua timu zako, unapeleka karatasi yako kwa wakala ambayo huchapishwa na kutolewa kitu kinachoitwa ‘mkeka’. Baada ya kupata mkeka, unasubiri timu hizo zicheze na baada ya hapo timu zako zote ulizochagua zikishinda basi utajipatia fedha ambazo ni jumla ya kiasi cha fedha na idadi ya pointi za timu ulizochagua,” alisema

Kwa upande wake Meneja Uendeshaji wa Premier Betting, Javier Diaz Del Rio, ambayo huchezesha mchezo huo hususan kwa ligi za Ulaya kama ligi ya kuu za England, Hispania, Ujerumani na Ufaransa, alisema kampuni hiyo hutoa zawadi hadi Sh bilioni 2 kwa mwezi.

“Fedha zetu huwa tunatoa papo kwa papo, mteja anaweza kuchukua kwa wakala wetu kama ni kiasi kidogo au kwenye matawi yetu mengine kama ni kiasi cha kati ila kwa kiasi kikubwa wanakuja kuchukua makao makuu,” alisema Rio

Lugha inayotumika

Ubashiri huo katika michezo hiyo unajulikana zaidi kwa jina la ‘mikeka’ itakumbukwa kwamba mkeka ni kitu kama jamvi kinachoshonwa kutokana na kili na hutumika kwa kazi mbalimbali kama vile kukalia au kutandika kitandani.

‘Sports Betting’ iliitwa mikeka kutokana na karatasi zinazobandikwa katika ukuta wa matangazo katika kituo cha michezo ya kubahatisha ikionyesha mechi mbalimbali zinazotarajiwa kuchezwa.

Kwa Tanzania kuna makampuni zaidi ya 10 ya michezo ya kubahatisha ambapo baadhi ni Premier Betting, Gaming Africa (Meridian), Gateway Gaming (M Bet), New Africa Casino, Play Master na Dunia Investiment (iPlay8).

Source: Mtanzania
ZeroDegree.
Kamari janga jipya. Kamari janga jipya. Reviewed by Zero Degree on 8/03/2016 10:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.