Loading...

Yanga yajibu mapigo ya Mo.

MTU mzima hatishiwi nyau! Yanga imewasikia Simba wakijitapa kutangaza mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yao kwa lengo la kumpa hisa, Mohamed Dewji ‘Mo’ na wao wameamua kujibu mapigo kwa kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama wote mwishoni mwa wiki hii ili kupanga mikakati mipya ya klabu hiyo.


Licha ya kwamba Wanajangwani hao hawajaweka wazi ajenda za mkutano huo, lakini inaonyesha nao wanakwenda kuweka mambo sawa ili timu yao nayo iendane na wakati kama walivyofanya wapinzani wao hao wa jadi.


Habari za ndani ambazo hazikuweza kuthibitishwa mara moja, zinasema ajenda zitakazokwenda kujadiliwa Jumamosi ni tano ambazo ni mapitio ya ripoti ya mkutano uliopita, maendeleo ya klabu, udhamini wa Kampuni ya Quality Group, suala la uwanja pamoja na mengineyo.

Mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wanachama ambao wanatamani kujua nini kinakwenda kujiri, utafanyika Jumamosi hii katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga, Dar es Salaam.

Mkutano huo unakuja ikiwa ni siku chache baada ya mahasimu wao, Simba kukubali mabadiliko kutoka klabu na kuendeshwa kwa mfumo wa hisa ambapo tayari Mohamed Dewji ‘Mo’, ametoa ofa ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh bilioni 20.

Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na ambayo imethibitishwa na Kaimu Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit, inawataka wanachama kufika kwenye mkutano huo Jumamosi.

Simba walifanya mkutano wao mkuu mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo idadi kubwa ya wanachama walikubali mabadiliko ya mfumo ambao bila shaka unamwezesha Mo kuichukua timu na sasa Yanga nao wanataka kujibu mapigo.

Licha ya kwamba mashabiki wa Simba wameanza kutembea kifua mbele na kuanza kuwaringia wenzao, kigogo mmoja wa Yanga ameibuka na kusema Wekundu hao wa Msimbazi wataendelea kuwa ‘Wa mchangani’ na hawataweza hata siku moja kuwasogelea Wanajangwani hao.

Moja ya mambo aliyoyazungumza kigogo huyo ni kwamba kwa sasa hivi Kampuni ya Quality Group ndiyo inayoidhamini Yanga, ikiwamo vifaa vya michezo kama jezi na kwamba vibosile wengine wameahidi kuendelea kuisapoti timu hiyo.

“Kama kuna shabiki yeyote wa Yanga ambaye ameingiwa na kiwewe kuhusu Simba kutaka kumpa Mo timu namwambia wala hilo lisimuumize kichwa kwani sisi ndio baba wa soka hapa nchini.

“Wakati hao Simba wakijipapatua leo sisi tulishajipanga mapema sana hivyo hayo wanayoyafanya wamechelewa na hapa kama unavyotuona kwa sasa tunapata huduma kutoka Quality Group ndiyo maana unaona jezi zetu zina jina la kampuni hiyo.

“Mbali na hilo bado wapo vibosile wengine wapo nyuma yetu sasa kama kuna mtu anaiona Yanga itakuwa masikini na kupitwa na Simba atakuwa anajitesa mwenyewe,” alisema kigogo huyo.

Alisisitiza kwamba, kudhihirisha kuwa Yanga haina shida yoyote ndiyo maana inaendelea kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa tofauti na mahasimu wao hao (Simba) huku akitamka wazi kuwa msimu ujao ubingwa bado utatua mikononi mwao.

“Wao Simba hata wafanyeje hawawezi kutuzidi kwa kitu chochote na hii itaendelea kujidhihirisha msimu ujao kwani tutatwaa tena ubingwa na kubwa kuliko yote tutawafunga kila tutakapokutana nao,” alisema.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo kwa sasa wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika na mwishoni mwa wiki ijayo watacheza na Mo Bejaia ya Algeria Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Credits: Dimba
ZeroDegree.

Yanga yajibu mapigo ya Mo. Yanga yajibu mapigo ya Mo. Reviewed by Zero Degree on 8/03/2016 10:41:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.