Loading...

MO aivuruga Simba

MKUTANO Mkuu wa Simba ulivunjika jana baada ya rais wake, Evans Aveva kuzidiwa na hoja ya wanachama kutaka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji au Mo, akubaliwe kununua hisa.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam, wengi wa wanachama hao walitaka kujadili hoja moja tu ya Mo na zingine ziwekwe kando.


Wanachama wa klabu ya Simba wakimsindikiza rais wao, Evans Aveva (mwenye miwani) baada ya kuvunjika kwa Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Dar es Salaam jana.

Baada ya kuzidiwa na kelele za wanachama waliokuwa wakilitaja jina la Mo kila mara, Aveva aliamua kuizungumzia hoja hiyo, lakini bila kufikia muafaka aliamua kuvunja mkutano huo.

Alisema kuwa hoja hiyo itafanyiwa kazi na kuwafanya wanachama kulipuka kwa furaha wakilitaja kwa nguvu jina la Mo, na hapo ndipo Aveva alipopata nafasi ya kuuvunja mkutano huo.

Mo alipendekeza auziwe hisa za asilimia 51 kwa gharama ya Sh bilioni 21 huku zile zilizobaki 49 atawanunulia wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo ili iendeshwe kikampuni.

Wanachama wa Simba waliushinikiza uongozi wao kujadili hoja namba tisa iliyohusu Mo kununua hisa hizo na kuutaka viongozi wao waachane na hoja zingine zote na kuijadili hiyo ya hisa.

Kikao hicho ambacho kiliendeshwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi kilianza saa 2 asubuhi, ambapo wanachama wengi walifika wakiwa na ajenda ya kutaka kuuzwa kwa hisa na si vinginevyo.

Kwa sasa Simba inaonekana kusuasua katika vyanzo vyake vya mapato baada ya kujitoa kwa mdhamini, Kampuni ya Bia ya Kilimanjaro ambayo ilikuwa ikizidhamini Simba na Yanga na kwa sasa imesitisha udhamini wake kote.

Hali hiyo imesababisha msukumo mkubwa kwa wanachama kutaka mwekezaji wa muda mrefu katika kampuni hiyo, ambapo hoja hiyo ilitawala katika mkutano huo, hali iliyositisha kujadiliwa kwa hoja nyingine.

Ilielezwa na mwanachama mmoja katika mkutano huo kuwa kati ya hoja sita za msingi, ambazo ziliahidiwa na Rais Evans Aveva na kamati yake kabla ya kuingia madarakani ni moja tu ya ulipwaji wa mishahara ndio ambayo imefanikiwa.

Alihoji ni kwa nini Aveva na kamati yake wasijiuzulu uongozi, hali hiyo ilifanya wanachama kushangilia na kutaka mabadiliko hayo kufanyika, lakini hata hivyo Aveva alijikuta katika wakati mgumu alipotaka kuzuia hoja hiyo.

Baada ya mvutano wa dakika 15 wanachama walikubali kumsikiliza Aveva aliyetaka kujadiliwa kwa hoja nyingine muhimu kwanza, na ndipo akaruhusu kusikilizwa kwa ripoti ya mkaguzi wa mapato ya Simba.

Ripoti hiyo iliendelea kubainisha madudu katika matumizi ya fedha na kisha msomaji wake akashauri kuwa klabu hiyo inatakiwa kuwa na mapato ya kudumu na kushauri ujio wa mwekezaji, hapo ndipo wanachama walipoanza tena vurugu.

Safari hii wanachama walikataa kukaa kimya na kuendelea kushangilia wakitaja jina la Mo kila mahali wakiwa wanamaanisha Mohamed Dewji apewe hisa. Hali hiyo ilidumu kwa takribani dakika 20 kabla ya Aveva kukubali hoja hiyo ya uuzwaji wa hisa kuingizwa kuwa ni moja kati ya hoja za kujadiliwa na wanachama na kumaliza kikao.

Baada ya kuvunjika kwa kikao hicho Aveva alitolewa akiwa chini ya ulinzi mkali na kisha kupumzishwa ndani ya bwalo kabla ya kuondoka baada ya dakika 30.

Watu mbalimbali walitoa maoni yao kuhusu suala hilo, ambapo mwanachama mkongwe wa klabu hiyo Mzee Kilimoni alisema kuwa uuzwaji wa hisa sio shida ila inaonekana ni kama kuna nguvu imetumika kuwalaghai wanachama na kujikuta wakishabikia bila ya kuwa na hoja ya msingi.

Kwa upande wake mwanachama na aliyewahi kuwa kiongozi wa zamani wa Simba, Majaliwa Mbasa, Diwani wa kata ya Sumve mkoani Mwanza, alimlaumu Aveva kuwa ni kiongozi asiye na uwezo wa kutoa uamuzi.

Alisema kwa sasa Aveva hana mwelekeo, ameshindwa hata kuongoza kikao hicho na kumalizika kihuni huku akisisitiza kuwa Simba inahitaji mabadiliko ya kweli.


Source: Habari Leo
ZeroDegree.
MO aivuruga Simba MO aivuruga Simba Reviewed by Zero Degree on 8/01/2016 09:51:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.