Loading...

Lembeli: Siondoki Chadema

SIKU moja baada ya Mbunge wa zamani wa Kahama Mjini, James Lembeli kuibuka katika mkutano wa Rais John Magufuli, amesema hana mpango wa kurudi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Lembeli alijiengua CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika kile alichodai kuchoshwa na vitendo vya rushwa vilivyokithri ndani ya chama hicho tawala.

Juzi, akiwa katika mkutano wa Rais Magufuli uliofanyika Kahama, aliitwa na mkuu huyo nchi aweze kuwasalimia wananchi.

Alisema: “Iwapo Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli atakisafisha chama hicho basi na mimi ninaweza kurudi katika chama hicho kwa lengo la kuwahudumia wananchi”.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa kitendo cha mwanasiasa huyo kuibuka katika mkutano huo, tafsiri yake ni kwamba amerejea ndani ya chama chake hicho cha zamani.

Akizungumza jana, Lembeli alisema msimamo wake uko pale pale.

Alisisitiza kwamba hana mpango wa kurejea CCM mpaka Rais Magufuli atakapoweka sawa mazingira ya chama hicho tawala.

“Msimamo wangu niliutoa pale uwanjani na Rais mweyewe akasikia kwamba siwezi kurudi CCM wakati mazingira bado ni yale yale.

“Na nilisema uwanjani pale unapomkaribisha mtu unategemea jibu la ndiyo au hapana… jana (juzi) nilimwambia Rais hapana, siwezi. Watu wa Kahama wananifahamu zaidi ya mtu mwingine yeyote.

“Msimamo wangu wanaufahamu ni wapi niliko wanapafahamu na ndiyo maana nilipokaribishwa kusalimia umati mkubwa karibu wote waliokuwapo pale walishangilia kwa nguvu moja bila kujali huyu ni nani wala nani…kwa hiyo msimamo wangu uko pale pale,”alisema Lembeli.

Lembeli ambaye aliongoza Jimbo la Kahama kwa miaka 10, alisema kama angekuwa amemweleza Rais Magufuli kuwa amerudi, angetangaza katika mkutano huo.

“Mimi hizi biashara za watu kuandika vitu vya uongo wanaweza wakaendelea nazo kwa sababu kama ningekuwa nimemweleza Rais kuwa nimerudi angetangaza pale pale,”alisema Lembeli.
Akiwa katika mkutano huo juzi, Rais Magufuli alimtaka Lembeli kurejea ndani ya CCM kwa kuwa chama aliko kwa sasa ndiko walipo mafisadi.

“Wana Kahama tambueni kuwa Lembeli ni rafiki yangu wa siku nyingi na kuwapo kwake hapa ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na ninakushauri urudi Tanzania kwani ulikokwenda umepotea.

“Ninakuomba Lembeli urudi kundini mimi ninakujua unavyowapenda wananchi wako wa Kahama.

“Ukirudi sitakukata mkia kwa sababu huko ulikokwenda umepotea njia, mimi ndiye mwenyekiti ninayewapinga wasaliti ambao asubuhi wapo CCM, jioni wapo upinzani,”alisema Rais Magufuli.

Credits: Mtanzania
ZeroDegree.
Lembeli: Siondoki Chadema Lembeli: Siondoki Chadema Reviewed by Zero Degree on 8/02/2016 09:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.