Loading...

Serikali yajibu hoja mbili za Kitwanga ndege za ATCL

SIKU chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kuponda aina ya ndege mpya zinazotarajiwa kununuliwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), serikali imetetea uamuzi huo.

Kitwanga, ambaye 'alitumbuliwa' na Rais John Magufuli Mei 20 kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa na kujibu swali lililoelekezwa kwenye wizara yake, Agosti 24, mwaka huu wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipokutana na ATCL na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), aliziponda ndege hizo kutokana na kile alichodai hazina mwendo wa kasi, huku akishangaa kununuliwa kwa fedha taslimu wakati duniani kote ndege zimekuwa zikinunuliwa kwa mkopo.

Mbunge huyo wa Misungwi (CCM) alikwenda mbali zaidi kwa kuhoji uwezo wa kampuni iliyouza ndege hizo akidai Tanzania itakuwa mteja wake wa kwanza.

UFAFANUZI WA SERIKALI

Hivi karibuni, serikali imetangaza kununua ndege nne katika kipindi cha mwaka huu wa fedha kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga hapa nchini zitakazogharimu Dola za Kimarekani milioni 46.

Serikali kwa kuanzia imetoa asilimia 40 ambazo ni sawa na shilingi 39,937,939,200 kwa ajili ya ununuzi wa ndege mbili za awali ambazo zimelipwa Kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.

Azma hiyo ya serikali ya kununua ndege mpya inatokana na ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli kutaka kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kulipatia mtaji ili lianze upya kutoa huduma hiyo kwa Watanzania.

Ujio wa ndege hizo utaimarisha huduma za usafiri wa anga na kuongeza ushindani katika utoaji wa huduma za anga hapa nchini kati yake na kampuni binafsi za ndege zinazotoa huduma hiyo kwa sasa.

Mara baada ya ndege hizo kuwasili hapa nchini zitaanza kutoa huduma ya usafiri wa anga hapa nchini kabla ya kupanua wigo wake wa utoaji wa huduma katika ngazi ya ukanda wa Afrika Mashariki na baadaye katika anga nyingine za kimataifa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (MB) aliwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha hivi karibuni alisema kuwa Shirika la ATCL lina ndege moja aina ya Dash 8-Q300 na ndege ya kukodi aina ya CRJ 200.

“Kwa sasa ATCL ina ndege moja na ndege nyingine ni ya kukodi ambazo zinawezeshwa na Serikali kutoa huduma za usafiri wa anga kati ya Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Kigoma na Moroni Comoro” alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa aliongeza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na kampuni ya ATCL na wadau wengine imekwishaainisha ndege mbili zinazofaa kununuliwa ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 78 na baadaye ndege nyingine mbili kubwa zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria 155 ambazo zitanunuliwa kwa kipindi cha mwaka huo wa fedha.

Mchakato wa ununuzi wa ndege hizo mbili ambazo zitanunuliwa katika awamu ya kwanza ulihusisha wawakilishi wa viwanda vya ndege vya Boeing ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani alisema kuwa ndege hizo ambazo zinatarajiwa kununuliwa zitatumia anga la Tanzania ambapo hivi sasa anga hilo linatumiwa na ndege zinazotoka nje ya Afrika, hivyo upatikanaji wa ndege hizo utasaidia kutoa fursa kutua kwenye anga za nchi jirani.

“Muda si mrefu tutapata ndege mbili mpya, mwakani tutaongeza nyingine mbili, Serikali imejipanga kufufua Shirika la Ndege na kubadilisha mfumo wa uendeshaji ili liweze kujiendesha lenyewe,” alisema Mhandisi Ngonyani.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,William Budoya, amesema kuwa msukumo wa kununua ndege hizo ni jambo la muda mrefu kuanzia Serikali ya Awamu wa Nne 2005-2015,na katika kuendeleza utekelezaji wa juhudi hizo Serikali ya Awamu ya Tano imetoa msisitizo na kulipa kipaumbele suala hilo.

Aidha, Afisa Mawasiliano huyo amesema kuwa ndege zitakazonunuliwa ni aina ya Bombadier kutoka kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.

Serikali ilichagua kampuni ya Bombadier Inc kwa sababu iliainisha mchanganuo wa biashara ambao ulishauri kuanza na ndege ndogo, kwa kuangalia soko la ndani baadaye ndege zinaweza kuongezwa kwa kuangalia soko la kimataifa.

Aliongeza kuwa ndege hizo zinatarajia kufika nchini ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, na kwa kuanzia zitaanza kutoa huduma kwa safari za ndani ya nchi.

Aidha, alisema kuwa Serikali imemteua mshauri mwelekezi ambaye ataweka manejimenti imara katika uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi walio na weledi na wenye utayari wa kufanya kazi kwa ufanisi.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Serikali yajibu hoja mbili za Kitwanga ndege za ATCL Serikali yajibu hoja mbili za Kitwanga ndege za ATCL Reviewed by Zero Degree on 8/31/2016 08:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.