Loading...

Usain Bolt hajaacha kitu Rio de Janeiro.

HANA mpinzani! Unaweza kusema hivyo kwa mwanariadha kutoka nchini Jamaica, Usain Bolt, ambaye amezidi kuweka rekodi kwenye michuano ya Olimpiki nchini Brazil.

Amekuwa akiweka rekodi mara kwa mara na hakuna mpinzani ambaye ameweza kuzivunja rekodi zake, hivyo katika michuano hiyo ambayo imemalizika jana nchini Brazil, bingwa huyo wa mbio amefanikiwa kuchukua medali ya dhahabu katika hatua ambayo alishiriki.



Tunaweza kusema kuwa huu ni wakati wake ambao anaweza kuwaaga mashabiki wake wa riadha, kwa kuwa hakuna wa kushindana naye zaidi ya kuvunja rekodi zake.

Kama kungekuwa na mshindani wake ambaye anampa wakati mgumu kwenye mchezo huo, basi bado angeendelea na ushindani kwa ajili ya kuweka rekodi dhidi ya mpinzani wake, lakini kwa hali ya sasa ni bora akasema kwaheri riadha ili kuweza kuwapa nafasi washiriki wengine wakatamba.

Hata hivyo, mwenyewe aliwahi kusema kuwa ana mpango wa kustaafu mwakani 2017, lakini hata sasa anaweza kubadilisha maamuzi yake na kustaafu mwaka huu kwa kuwa hakuna medali ambayo amebakisha kwenye riadha.

Bolt alianza kuonesha makeke yake tangu mwaka 2008 katika michuano ya Olimpiki nchini China, katika mbio za mita 100, 200 na mbio za kupokezana vijiti, alifanya vizuri katika mbio hizo na kutwaa medali.

Hata hivyo, mwaka 2009, katika michuano ya dunia ya Championships, ambayo ilifanyika nchini Ujerumani, nyota huyo aliendeleza ubabe wake kama ilivyo mwaka 2008.

Mwaka 2011, kwenye michuano ya Championships jijini Daegu, Korea ya Kusini, alishiriki kwenye mbio za mita 200 na kupokezana vijiti na alifanikiwa kufanya vizuri katika mbio zote.

Hakuishia hapo, mwaka 2012, kwenye michuano ya Olimpiki jijini London, hakuwa na mpinzani kwenye mbio za kupokezana vijiti, mita 100 na mita 200, zote alikusanya medali zake.

Mwaka 2013 kwenye michuano ya dunia ya Championships, ambayo ilifanyika jijini Moscow, nchini Urusi, aliendeleza ubabe wake kwa mita 100, mita 200 na mbio za vijiti na alifanya hivyo hivyo mwaka 2015, kwenye michuano ya dunia ya Championships, Beijing nchini China.

Mwaka huu amemaliza kwa kurudia yale yale ambayo aliyafanya London au Urusi kwa kushinda mbio zote ambazo alishiriki, hivyo ni wazi kwamba hadi sasa hana mpinzani tangu ameanza kuonesha moto wake.

Kitu ambacho kilikuwa kinamfanya aendelee kushiriki michuano mbalimbali ni kutaka kuvunja rekodi zake mwenyewe na si kushindana na mpinzani yake yeyote kwa kuwa hakuna mtu ambaye ana kasi zaidi yake kwa kipindi cha sasa katika mbio anazoshiriki.

Hivyo inaonekana kuwa uwezo wake kwa sasa unaanza kushuka japokuwa kila siku anachukua medali, lakini kasi yake imekuwa tofauti na miaka mitatu iliyopita.

Mwaka huu katika mbio hizo za mita 200, Bolt alikuwa na lengo la kutaka kuvunja rekodi yake mwenyewe ya sekunde 19.19 ambayo aliiweka mwaka 2009, lakini kasi yake imeonekana kushuka na hatimaye kutumia sekunde 19.78 lakini bado alikuwa yeye ni mshindi.

Bolt ambaye jana alitimiza umri wa miaka 30, anakutana na vijana wenye umri wa miaka 26 kama vile Yohan Blake kutoka nchini Jamaica, hivyo Blake anaweza kumsumbua Bolt baadaye kutokana na umri kuanza kuchoka.

Hata hivyo, Bolt mwenyewe anaamini kuwa umri wake unamfanya kasi ipungue, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa miaka miwili mbele Bolt akampata mshindani wake ni bora akafanya maamuzi mapema ya kustaafu mchezo huo huku akiwa tayari ameweka rekodi kubwa kwa kipindi hiki.

Kama atashindwa kuchukua maamuzi mapema, basi anaweza kutia doa katika historia yake, hata hivyo wapo wapinzani wake ambao wanatamani bingwa huyo astaafu mchezo huyo ili na wao waweze kuweka historia zao.


ZeroDegree.
Usain Bolt hajaacha kitu Rio de Janeiro. Usain Bolt hajaacha kitu Rio de Janeiro. Reviewed by Zero Degree on 8/23/2016 10:21:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.