Loading...

Bilioni 100/- zayeyuka Hazina.

CAG, Profesa Juma Assad.
SIKU moja baada ya kutimuliwa kazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini ufisadi wa Sh. bilioni 100.5 ambao unaihusisha Hazina na Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Ufisadi huo ulibainika mjini hapa jana kwenye kikao cha kamati hiyo iliyokuwa ikipitia hesabu za Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2014/15 uliofanyika wakati ofisi hiyo ikiwa chini ya Waziri Mkuu.

Akipitia kitabu cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya hesabu za wizara hiyo, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM), alisema vitabu vya hesabu za Tamisemi vinaonyesha kwa mwaka huo wa fedha, ofisi hiyo ilipewa Sh. bilioni 286 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kwamba asilimia 99.9 ya fedha hizo zilitumika.

Alisema hesabu hizo pia zinajichanganya kwa kuonyesha kwamba, kati ya fedha hizo za maendeleo zilizotolewa na Hazina, Sh. bilioni 100.5 zilirudishwa kwenye mfuko mkuu huo wa serikali bila kutoa taarifa kwa Tamisemi.

Alihoji kama kiasi hicho cha fedha (Sh. bilioni 100.5) zilichukuliwa na Hazina, ina maana kwamba fedha zilizotumika ni Sh. bilioni 186, ambayo ni sawa na asilimia 53 na siyo 99 kama inavyoonekana kwenye vitabu vya wizara hiyo.

“Kwa maana hiyo, miradi ya maendeleo ambayo ni pamoja na elimu, afya na barabara ambayo ilikuwa inategemea fedha hizo haikufanyika, na hapa tuna taarifa ambayo imetoka Hazina inasema wao walishatoa fedha zote na zimetumika,” alisema Kakunda.

Akifafanua juu hoja ya taarifa ya Hazina na Tamisemi kukinzana juu ya kuchukuliwa kinyemela kwa fedha hizo, Kakunda alisema kwa kawaida kabla ya kutolewa na Wizara ya Fedha, kamati maalumu hukaa na kubariki kuzitoa.

Alisema endapo Hazina inataka kupangia majukumu mengine, fedha ambazo zimeshatolewa, kamati hiyo hukaa tena na kubadilisha matumizi yake jambo ambalo kwa upande wa fedha hizo za Tamisemi halijafanyika.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Musa Iyombe, alisema alipoanza majukumu yake kwenye ofisi hiyo, alielezwa kwamba fedha hizo zilitolewa na Hazina na baada ya muda zikachukuliwa tena na Hazina wenyewe.

Alisema baada ya hapo, alianza kuwaandikia Hazina barua ili watoe fedha hizo, lakini hawajajibu hata moja.

“Barua wamekuwa hawajibu hata moja, lakini wamekuwa wakirudisha fedha kidogokidogo, mara ya kwanza walileta Sh. bilioni saba na mara ya pili wakaleta Sh. bilioni 10, kwa hiyo, sasa tunawadai kama Sh. bilioni 83,” alisema.

Kutokana na majibu hayo, Kakunda alihoji tena kuhusu utaratibu uliotumika na Hazina kuzirudisha fedha hizo kidogokidogo ilihali taarifa waliyoiwasilisha bungeni inasema wao fedha hizo zote walishatoa na zikatumika.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM), alisema kinachoonekana kwenye hesabu za Tamisemi ni kwamba fedha hizo ziliingia na kutolewa na watu wachache ambao sasa wanafanya biashara na faida kuirejesha kidogokidogo.

Naye Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), alisema: “Hoja yetu hapa hizo fedha baada ya kurudishwa Hazina zilienda wapi? Mwenyekiti hapa tuwarudishe hawa wakatuletee taarifa zaidi kwa sababu hakuna kitu hapa,” alisema.

Wabunge hao pia walihoji sababu ya Hazina kutotaka kujibu barua za Tamisemi na kwamba hilo ni eneo jingine linaloongeza wasiwasi.

Kutokana na suala hilo kuzusha mvutano, Mbunge wa Malinyi, Dk. Haji Mponda (CCM), aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, aliwataka Tamisemi kutoka ndani ya kikao hicho ili kamati hiyo ijadiliane na kutoka na kauli moja.

Tamisemi waliporudi ndani, Dk. Mponda alisema kamati hiyo imekubaliana iwarudishe na wasijadili hesabu zao mpaka kwanza walete taarifa za kina juu ya muamala huo ulivyokuwa tangu fedha hizo kuingizwa na baadaye kutolewa.

Alisema wanaipa ofisi hiyo muda wa siku sita kuanzia leo kutafuta taarifa hiyo ili Septemba 7, mwaka huu iwakilishe taarifa sahihi kwenye ofisi za bunge.

“Mkishaileta, ndiyo tutawapangia ni lini mje tuendelee kupitia hesabu zenu,” alisema.

Source: Nipashe
Zerodegree.
Bilioni 100/- zayeyuka Hazina. Bilioni 100/- zayeyuka Hazina. Reviewed by Zero Degree on 9/02/2016 03:41:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.