Loading...

Hii hapa siri ya Nigeria kujenga mtambo wa umeme nchini Tanzania.

Mtambo wa umeme wa Egbin.
KAMPUNI ya Egbin Power Plc ya Nigeria imeeleza nia yake ya kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini Tanzania.

Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Dallas Peavey aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara hivi karibuni huko kuna sababu nyingi ambazo zimefanya wavutiwe kuwekeza Tanzania.

Kampuni hiyo ya Egbin, ambayo ni kampuni tanzu ya Sahara Group ya Nigeria imepanga kutumia kiasi cha Sh. trilioni 1.4 ili kujenga mtambo utakaotumia nguvu ya gesi.

Sahara Group ni kampuni kinara katika Afrika kwa masuala ya gesi na mafuta.
Peavey anasema wanaamini uwekezaji huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya umeme nchini Tanzania.

Anaeleza kuwa ujenzi wa mtambo huo ulikuwa unatarajiwa kuanza mara baada ya kupata kibali cha serikali.

"Tumepanga kujenga mtambo utakaozalisha megawati 450 za umeme. Tunachosubiri ni ruhusa ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco),” anaeleza Peaveley.

Baada ya kupata kibali hicho, vitu vikubwa vya msingi watakavyofanya ni kuchagua mahali utakapojengwa mtambo huo na mahitaji yake.

Uongozi wa kampuni ya Sahara tayari umekutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felischemi Mramba.

Peavey anaeleza kuwa ikiwa mtambo huo utaidhinishwa basi awamu ya kwanza ya ujenzi wake inaweza kuchukua miezi 12.

"Tunataka kutoa mchango wetu kuendeleza sekta ya umeme nchini Tanzania. Kwani tuna uzoefu na shughuli hizi kutokana na kazi zetu tunazofanya katika nchi nyingine za Afrika, Marekani na Ulaya,” anaongeza Peavey.

Hata hivyo, ofisa huyo anaeleza kusikitishwa na hatua ya serikali kuchelewa kuidhinisha mradi huo.

Habari za ndani kutoka ndani yua duru za serikali zinasema kutokana na dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kutaka kujenga uchumi wa viwanda iliamua kutangaza zabuni kwa kampuni za kuzalisha umeme.

Kampuni tatu inasemekana zilipita kwenye mchujo wa awali na kampuni inadaiwa zilibainika hazikuwa na uzoefu.

Nipashe haikuweza kuthibitisha taarifa hizo ingawa linafahamu kuwa serikali ina mkakati wa kuimarisha sekta ya nishati ili taifa lipate umeme wa bei nafuu.

Peavey anasema kuwa kampuni hiyo ya Egbin iko tayari kujenga mtambo.

Egbin pia inasimamia mtambo mkubwa zaidi wa umeme nchini Nigeria.

Kampuni hiyo inazalisha mtambo wa umeme wa gesi unaotoa megawati 1,320 kwenye gridi ya taifa ya Nigeria.
Ilinunua mtambo huo kutoka kwa Serikali ya Nigeria mwaka 2014.

Sababu za Wanigeria kutaka kuwekeza Tanzania Tanzania inakadiriwa kuwa watu wapatao milioni 45 lakini asilimia 30 tu ya watu wake ndio inadaiwa wanapata nishati ya umeme.

Watu walio wengi wanatumia zaidi kuni na mkaa kama nishati mbadala.

Kampuni ya Sahara inaamini nishati ya umeme ni umuhimu katika kusaidia kupiga vita umasikini nchini.

Pia kwa kuwa serikali iko katika kampeni ya kuigeuza nchi kuwa ya viwanda lazima pawepo umeme wa kudumu.

“Serikali ya Tanzania kama inataka kutekeleza kikamilifu azma yake ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda lazima pawepo nishati ya kutosha ya umeme,” anaongeza Peavey.

Peavey anasema kuwa pale watu walio wengi watakapokuwa wanaweza kupata umeme ina maana pia itakuwa hatua muhimu ya maendeleo kwa watu wake.

“Sisi Sahara tunaamini kuwa ikiwa tuleta umeme wetu tutakuwa tumeshiriki kwa kiasi kikubwa kupiga vita umaskini nchini Tanzania,” anaongeza Peavey.

Pamoja na kuwa watu wengi wa Tanzania hawapati nishati ya umeme lakini bado imejaliwa kuwa na vyanzo mbalimbali vya umeme.
Tanzania imejaliwa kuwa na gesi asilia, vyanzo vingi vya maji, upepo, makaa ya mawe na madini ya urani.

Peavey anaeleza kuwa uongozi wa kampuni ya Sahara unaamini kwa kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini Tanzania ina maana itakuwa imeshiriki katika kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania.

Tanzania haijaweza kutumia vyanzo vyake vingi vya umeme vilivyopo nchini.

Kugunduliwa kwa gesi ya Mtwara imekuwa kichocheo kikubwa kwa kampuni ya Sahara kuvutiwa kuja kuwekeza nchini.
Wachumi wanaamini kuwa ikiwa gesi hiyo itatumiwa vizuri itaifanya Tanzania kupiga hatua kubwa kiuchumi.

Ndio maana kampuni hiyo ya Sahara wameona watumie nafasi hiyo ya kuja kutoa mchango wao katika sekta ya umeme kwa kutumia rasilimali hiyo.

Gesi asilia iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka 1974 kwenye kisiwa cha Songo Songo, mkoani Lindi kabla ya kufuatiwa na gunduzi nyingine katika maeneo ya Mtwara Vijijini (Mnazi Bay, 1982 na Ntorya, 2012), Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008), Bonde la Mto Ruvu (Pwani, 2015) na Bahari ya Kina Kirefu (2010 – 2014).

Mpaka sasa Tanzania ina akiba ya gesi asilia iliyothibitishwa kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.27 huku tafiti nyingine zikiendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini na tayari ugunduzi wa mafuta nao umefanyika katika Bonde la Ziwa Rukwa.

Rasilimali hiyo ya gesi asilia inaweza kutumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo kuzalisha umeme, malighafi ya kuzalishia mbolea na kemikali, nishati viwandani, majumbani na kwenye taasisi mbalimbali ambapo tayari ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme wa gesi katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam umekamilika tangu mwaka 2015.

Kukamilika kwa miradi hiyo kunaleta matumaini kwamba, tatizo la kukatika ovyo kwa umeme linaweza kupungua kama siyo kumalizika kabisa, kwani umeme utakaozalishwa utaingizwa kwenye gridi ya taifa na kusambazwa nchini kote.
Kuna mito mbalimbali, ambayo inaweza kutoa megawati nyingi za umeme.

Pia kuna makaa ya mawe, ambayo yapo kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Tanzania pia ina fursa ya kuwekeza kwenye umeme wa upepo na hasa maeneo ya Makambako na Singida.

Ina uwezo wa kufuata nyayo za nchi nyingine za Afrika kama Morocco, Tunisia na Misri.

Hata hivyo, kampuni hiyo ya Sahara inataka kuwekeza Tanzania kutokana na amani na utulivu vilivyopo nchini.

Peavey anaamini pia Tanzania imekaa sehemu nzuri kijiografia na kitovu muhimu kwa uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Historia ya Kampuni za Egbin na Sahara Mtambo wa Egbin ndio unaongoza kwa kutoa umeme mwingi zaidi nchini Nigeria.

Unazalisha kiasi cha megawati 1,320 kutokana na vitengo sita vyenye uwezo wa kutoa megawati 220 kila moja.
Mtambo huo uko kwenye eneo la Ijede, ambalo liko kilomita 40 kutoka jiji la Lagos.

Mtambo huo ulijengwa mwaka 1985 baada ya kuasisiwa na Rais wa wakati huo wa Nigeria, Ibrahim Babangida.
Pamoja na kuwa mtambo huo unatumia gesi lakini baadhi ya mitambo yake inatumia mafuta.

Hata hivyo, serikali ya Nigeria iliamua kubinafasisha kampuni hiyo mwaka 2013, ambapo sasa inaendeshwa kwa ubia wa kampuni ya Sahara group na kampuni ya umeme ya Korea (Kepco).

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Hii hapa siri ya Nigeria kujenga mtambo wa umeme nchini Tanzania. Hii hapa siri ya Nigeria kujenga mtambo wa umeme nchini Tanzania. Reviewed by Zero Degree on 10/19/2016 09:37:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.