Loading...

Mke wa Waziri achomoka ATCL.

MKE wa waziri mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tano (jina lake limehifadhiwa kwa sasa) aliyekuwa akifanya kazi Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ameacha kazi.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya shirika hilo vililiambia Nipashe jana kuwa mke huyo ambaye amedumu ATCL kwa zaidi ya miaka 20, aliandika barua ya kuacha kazi ghafla.

Kuacha kazi kwa mtumishi huyo (jina limehifadhi kwa sasa) kumekuja siku chache tangu Rais John Magufuli, bila kutaja jina, kusema anashangaa kuona wake wa baadhi ya mawaziri wake wanafanya kazi katika shirika ambalo halifanyi kazi vizuri.

Rais Magufuli aliyasema hayo Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizundua ndege mbili mpya ambazo zimenunuliwa na serikali kwa ajili ya 'kulifufua' shirika hilo.

Baadhi ya wafanyakazi ndani ya shirika hilo wakizungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa majina yao jana, walithibitisha mke huyo wa waziri kuandika barua hiyo ya kuacha kazi ikiwa ni siku chache baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vya habari vilisema katika barua yake hiyo, hakuainisha sababu za kufanya hivyo.

Watoa habari hao walisema mke huyo wa waziri aliyekuwa akifanya kazi katika moja ya vitengo nyeti, alichukua uamuzi huo ambao haukutarajiwa na wafanyakazi wenzake.

“...Hakuwa na cheo kikubwa na hadi anafikia uamuzi huo hakuonyesha dalili yoyote usoni, labda amekasirishwa na jambo fulani, alikuwa kawaida ndiyo maana nasema uamuzi aliouchukua haukutegemewa na yeyote na umetushtua kwa kweli,” kilisema moja ya vyanzo hivyo.

Aidha, habari zilidai kuwa wakati akizungumza na wafanyakazi wenzake, mama huyo aliwashukuru kwa ushirikiano waliompa na alisema mumewe (waziri), alimchumbia akiwa tayari anafanya kazi katika shirika hilo.

Gazeti hili lilizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, Mhandisi Patrick Itule, ambaye alisema bado ofisi yake haijapokea taarifa zozote za kuacha kazi kwa mke huyo wa waziri.

“Sina taarifa za kuacha kazi kwa mke wa (anataja jina la waziri huyo) kwa sababu kutoka asubuhi sikuwapo ofisini na sasa hivi natokea uwanja wa ndege kuelekea ofisini," alisema Itule. "Hata kama ni kweli masuala ya mtu kuacha kazi ni mambo binafsi, ni vizuri ukamtafuta mhusika.”

RIPOTI YA CAG

Aprili 24, mwaka huu, alipokuwa akiwasilisha bungeni ripoti zake za mwaka wa fedha 2014/15, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, alisema ATCL linaendeshwa kwa hasara likiwa na wafanyakazi zaidi ya 300.

Alisema linahitaji mageuzi makubwa ya kuwa na menejimenti imara itakayokuwa na mpango madhubuti wa kulifufua.
Alisema shirika hilo limekuwa halina faida kwa serikali zaidi ya kuitia hasara ya kulipa wafanyakazi mishahara wakati hakuna kazi zinazofanyika.

"Naongea haya nikiwa ninajiamini kwa sababu ninayafahamu vizuri. ATCL ina ndege mbili tu lakini ukienda pale kuna wafanyakazi zaidi ya 300, wote wanalipwa mishahara, hakuna kodi inayopatikana pale," alisema. Akifafanua zaidi kuhusu ndege mbili za ATCL, Profesa Assad alisema siku hiyo kuwa hata hizo zilizopo nazo hazifanyi kazi na kwamba shirika hilo lilitakiwa kuwa na wafanyakazi wachache na ofisi mbili tu.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mke wa Waziri achomoka ATCL.   Mke wa Waziri achomoka ATCL. Reviewed by Zero Degree on 10/05/2016 02:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.