Loading...

Atakayemrithi Vicent Agban atajwa.

MIONGONI mwa mijadala inayoendelea hivi sasa kwa wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba, kufuatia kupoteza michezo mwili ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Bara mzunguko wa kwanza, ni pamoja na udhaifu wa kipa namba moja wa kikosi hicho, Vicent Angban.

Angban, raia wa Ivory Coast, anatajwa kuonyesha kiwango kibovu katika mechi hizo na kusababisha timu yake kuchapwa kwa bao 1-0 na timu ya African Lyon, kabla ya kutandikwa tena 2-1 katika mechi ya kumaliza mzunguko wa kwanza, dhidi ya Prisons ya Mbeya, iliyochezwa Jumatano iliyopita.

Kufuatia mapungufu hayo, kocha wa makipa wa Wekundu hao wa Msimbazi, Adam Abdallah, maarufu kama ‘Meja Luu’, ameweka bayana majina ya makipa ambao anaamini kama watakuwemo katika kikosi chao katika mzunguko ujao, basi lango lao halitakuwa na madhara.

Amewataja makipa hao kuwa ni raia wa Uganda Frank Muhonge, anayekipiga katika Klabu ya Stand United ya Shinyanga na Youthe Rostand, ambaye ni raia wa Cameroon, anayechezea klabu ya African Lyon.

Amewaelezea makipa hawa wana utulivu wanapokuwa golini na vilevile wanaonyesha kumudu mikiki mikiki pale timu yao inapocheza na kikosi chenye washambuliaji wenye kasi.

Hata hivyo, amemtetea Angban, licha ya kudaiwa kupungua uwezo wake, lakini bado alihitaji kupumzika kutokana na kucheza mechi zote 15 katika ligi hiyo tangu ilipoanza.

Kuhusu kipa namba mbili wa Simba, Manyika Peter, alisema bado anaweza kuwa na manufaa kwa timu, lakini kitendo cha kumuweka benchi kwa kipindi kirefu kimemtoa nje ya mchezo.

Licha ya majina hayo, Wekundu hao wa Msimbazi pia wanamtaja kipa Abbas Pira, aliyewahi kuchezea klabu mbalimbani nchini Uingereza, ambaye ameonyesha nia ya kujiunga na klabu hiyo, endapo atafikia makubaliano na uongozi.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alikataa kuzungumzia suala lolote la kuacha au kusajili mchezaji kwa kipindi hiki, akidai kwamba hilo ni jukumu la kamati ya usajili, ambayo itafanya kazi na kisha kuwasilisha ripoti kwake na hivyo yeye kuyafanyia kazi.

Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, ikiwa kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 35, baada ya kucheza michezo 15, ikishinda 11, kutoa sare michezo miwili na kupoteza miwili.

ZeroDegree.
Atakayemrithi Vicent Agban atajwa. Atakayemrithi Vicent Agban atajwa. Reviewed by Zero Degree on 11/13/2016 01:32:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.