Loading...

Hans Pluijm afungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ].

KAMATI ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TTF) imeonesha makali baada ya kuwatia `pingu’ mechi tatu makocha wa Yanga na Azam, Hans-van-der-Pluijm na Zeben Hernandez na kuwapiga faini ya Sh 500,000 kila mmoja.

Aidha, kamati hiyo imekusanya jumla ya Sh milioni 15 kutokana na adhabu kwa wachezaji, makocha na timu za Ligi Kuu na zile za Daraja la Kwanza nchini.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Ahmad Yahaya imevuna fedha hizo ikiwa ni adhabu ya timu mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Pluijm ametiwa kitanzini kwa kosa la kutukana waamuzi wakati wa mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting, huku Hernandez akitiwa kitanzini baada ya kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi wakati timu yake ikicheza na Mbao FC ya Mwanza.

Katika mchezo wa Yanga na Ruvu Pluijm aliwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa na akaendeleza lugha za matusi kwa waamuzi hao mara baada ya mpira kumalizika, ambapo aliwafuata waamuzi kwenye vyumba vyao na kuwatolea lugha chafu.

Mbali na Plujim klabu ya Yanga pia imelimwa faini ya Sh 500,000 baada ya mashabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wanaingia vyumbani wakati wa mapumziko wakati wa mchezo huo.

Kwa upande wa Hernandez aliondolewa kwenye benchi la ufundi katika mchezo wao na Mbao baada ya kukataa kuheshimu mipaka ya eneo. “Adhabu hii utekelezaji wake utaanza mara tu ligi itakapoanza, klabu ndio zitakazowajibika kuhakikisha makocha hao wanatekeleza adhabu zao”.

Rungu hilo la kamati pia limeangukia kwa timu ya Simba ambayo imetakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 sambamba na Toto African ya Mwanza na kupewa onyo kali baada ya timu hizo zote kutumia mlango wa mashabiki kuingia uwanjani kitendo ambacho ni kinyume na kanuni ya 14 (14) ya Ligi Kuu.

Simba pia imelimwa faini nyingine ya Sh milioni 1 baada ya kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo kati yake na Prisons pamoja na kutumia mlango usio rasmi katika mchezo huo.

Hali kadhalika Prisons nayo imelimwa faini ya Sh milioni 1 kwa kutumia mlango usio rasmi katika mchezo huo na Simba. Pia Prisons imeadhibiwa baada ya gari la Jeshi la Magereza lenye namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu na kumuangushia kichapo na kumuumiza mlinzi wa geti.

Timu nyingine zilizoonja machungu na faini zao kwenye mabano ni Ruvu Shooting na Stand United (Sh 500,000) kila moja, Stand wachezaji wake waliingia uwanjani kwa mlango usio rasmi, huku Ruvu Shooting wakiwa ni wenyeji wa timu wakichelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15.

JKT Ruvu ambayo inapumulia mashine kwenye msimamo wa Ligi ikimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 13 wachezaji wake mlinda mlango Said Kipao, Samwel Kamuntu, Pela Mavuo na Paul Mhidze wamefungiwa mechi tatu na kutakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 kila mmoja.

Pia daktari wa JKT Ruvu Abdullah Yusuf naye ametiwa kitanzini kwa kufungiwa michezo mitatu na kutakiwa kulipa Sh 300,000 baada ya kutolea maneno machafu waamuzi.

ZeroDegree.
Hans Pluijm afungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ]. Hans Pluijm afungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania [ TFF ]. Reviewed by Zero Degree on 11/23/2016 10:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.